The House of Favourite Newspapers

HATIMAYE! ‘Malkia wa Tembo’ Ahukumiwa Jela Miaka 17 – Video

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu washtakiwa watatu akiwemo raia wa China, Yang Feng Glan (66) maarufu kama ‘Malkia wa Tembo’, kifungo cha miaka 15 jela kila mmoja na miaka miwili au faini ya Shilingi zaidi ya Bilioni 27.

 

Hukumu hiyo imetolewa leo Jumanne, Februari 19, 2019 mahakamani hapo baada ya watuhumiwa hao kutiwa hatiani kwa makosa ya Uhujumu Uchumi na kujihusisha na Ujangili wa Tembo na kufanya biashara haramu ya nyara za Serikali ikiwemo kukamatwa na vipande 860 vya meno ya tembo, sawa na kuuawa kwa Tembo 430 wenye thamani ya Tsh Bilioni 13.9.

 

Akisoma hukumu hiyo Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi amesema washitakiwa hao wanastahili adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine kutokana na kufanya ubinafsi kwa kutumia Mali ya Taifa kwa manufaa yao.

 

”Ushahidi unaonyesha jinsi gani washtakiwa wote watatu walivyosaidiana kuhakikisha wanatafuta meno ya tembo sehemu mbalimbali na kuyasafirisha.  Ushahidi wote unaonyesha jinsi gani nyinyi (washtakiwa) mmefahamiana kwa muda mrefu, ” alisema Shaidi akifafanua kwamba ushahidi umetolewa na watu 11 wakiwemo watu waliosafirisha meno hayo.

 

Pamoja na adhabu hiyo mahakama pia imeamuru shamba la pilipili manga na nyumba ya mtuhumiwa namba tatu iliyopo eneo la Maili Saba wilayani Muheza mkoani Tanga, mali zote zilizohusika kuhifadhi Meno ya Tembo ikiewemo nyumba kutaifishwa.

 

Mbali na Glan, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 21/2014, ni Watanzania wawili, Salvius Matembo na Philemon Manase ambao walikamatwa na maofisa wa wanyama pori mwaka 2015 na walikuwa wakitetewa na mawakili Nehemia Nkoko na Hassan Kiangio

BREAKING: MALKIA WA TEMBO AHUKUMIWA MIAKA 15 JELA, DPP AFUNGUKA – VIDEO

Comments are closed.