The House of Favourite Newspapers

Mama adaiwa kujigeuza kunguru, anaswa na mali za wizi

0

Na Mwandishi Wetu, Risasi Jumamosi
Mbeya: Jeshi la Polisi jijini hapa limetumia takriban saa nne kumkamata mama aliyedaiwa kujigeuza kunguru katika hali ya mauzauza kisha kumnasa na mali zinazosadikiwa kuwa ni za wizi.

Kwa mujibu wa shuhuda wetu, tukio hilo lililokusanya umati mkubwa, lilijiri juzikati kwenye Mtaa wa Mapelele, Kata ya Ilemi jijini hapa, kuanzia saa 4:00 asubuhi hadi saa 8:00 mchana ambapo polisi walisaidiana na wananchi kumkamata mama huyo aliyekuwa amejifungia ndani kwake.

Ilielezwa kwamba polisi walifika nyumbani kwa mama huyo katika mtaa huo, baada ya kutuhumiwa kumjeruhi jirani yake, Anitha Simon kwa madai ya kumuibia pea mbili za kandambili.

Akizungumzia tukio hilo, mtoto wa kaka wa mtuhumiwa ambaye ndiye aliyefanikisha zoezi la kumkamata, Venance Mwalindile alidai yeye ni chifu katika ukoo wao na kwamba alikerwa na tabia za shangazi yake huyo.

Mwalindile alieleza kuwa ilikuwa kazi ngumu kumkamata mama huyo anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 45 hadi 50 kwani akiwa amejificha chumbani kwake, alijigeuza ndege aina ya kunguru lakini alifanikiwa kumkamata baada ya kumnyonga kunguru huyo ndipo aliporudi katika hali yake ya kawaida na kumkabidhi kwa polisi.

Akizungumzia tukio hilo, mwenyekiti wa mtaa huo, Charles Kasyupa alisema kuwa wamekuwa na vikao vya mara kwa mara kuhusiana na matukio ya wizi na ugomvi ya mtuhumiwa huyo lakini kumekuwa hakuna mwafaka.

Ilisemekana kuwa baada ya kukamatwa mama huyo, polisi walifanya upekuzi kwenye nyumba yake na kukuta vitu kibao vinavyodhaniwa ni vya wizi vikiwemo redio, magodoro, runinga, mabeseni, viti na spika vya kanisani, mafuta, sukari, nguo na vitu vingine ambavyo idadi na thamani yake haikuweza kufahamika mara moja.

Baada ya kumkamata, polisi walisomba vitu vilivyokutwa ndani ya nyumba ya mama huyo na kumpeleka na vitu vyake kwenye Kituo Kikuu cha Polisi cha Kati kwa ajili ya uchunguzi zaidi na sheria kuchukua mkondo wake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi alithibitisha kukamatwa kwa mama huyo na kwamba jeshi lake linaendelea na uchunguzi ambao utakapokamilika, atatoa ripoti kamili ya tukio hilo.

Leave A Reply