The House of Favourite Newspapers

MAMA AIBUKA NA MAPYA YA WEMA

Miriam Sepetu

DAR ES SALAAM: Baada ya mwanaye kukaa kimya kwa muda mrefu, mama mzazi wa muigizaji Wema Sepetu, Miriam Sepetu ameibuka na mapya yanayomhusu bintiye huyo.

 

Mama Wema alifunguka hayo juzi Jumanne baada ya mwanahabari wetu ‘kumvutia waya’ na kumtaka amzungumziye binti huyo ambaye kwa sasa amekuwa kimya huku akionekana kufanya mambo ya maendeleo ikiwemo kufungua duka lake la nguo lililopo maeneo ya Kinondoni jijini Dar.

 

Mama Wema alisema, kwanza anamshukuru Mungu kwamba anamuona Wema anabadilika, anafanya mambo ya maendeleo tofauti na kipindi cha nyuma ambacho alikuwa akizungukwa na watu wasiofaa. “Wale watu waliomzunguka hawakuwa sahihi, alikuwa na msururu wa watu wakufuata tu mkumbo, wanafuata tu kama mkia vile,” alisema mama Wema.

 

Bi mkubwa huyo ambaye si mtu wa mchezo mchezo linapokuja suala la kuongea mbele ya wanahabari, alisema kitendo cha Wema kuanzisha duka lake ni moja kati ya mafanikio ambayo hata mashabiki wake wanapenda kumuona nayo licha ya kuwa amekuwa akipingwa mara kwa mara na baadhi ya watu.

 

“Wema anapendwa, hata hawa unaowaona kila siku wanampinga kwenye mitandao ya kijamii sio kwamba wanampinga, wanampenda sema Wema anakuwa hajui tu. “Walimpinga hata katika suala hili la duka lakini namshuru Mungu amefanikiwa, amelifungua tayari na leo (juzi) amenialika niende kuona.

Mimi huyu ni mwanangu, nampenda sana na ndio maana hata afanye nini bado nitaendelea kuwa naye bega kwa bega, naamini kabisa sasa hivi ameachana na marafiki wasiofaa na amebadilika,” alisema mama Wema. Kwa upande mwingine mama Wema alipoulizwa na mwanahabari wetu kuwepo kwa madai mtandaoni kuwa bintiye amechumbiwa, alikanusha taarifa hizo na kusema anayezieneza atakuwa na sababu zake binafsi.

 

“Mjinga huyu anayesambaza, hakuna kitu kama hicho sijaletewa posa wala nini,” alisema. Wema tangu amwagane na jamaa wake aitwaye PCK ambaye picha zao za faragha zimemsababishia msala mahakamani, amekuwa kimya huku akifanya mambo chanya tofauti na zamani.

Stori: Imelda Mtema, Amani

Comments are closed.