The House of Favourite Newspapers

MAMA Ajifungua, Amkimbia Mtoto Kimaajabu

MARA: Inasikitisha! Wakati watu wengi wakilia kukosa mtoto, Maria Samsoni (18), mkazi wa Kijiji cha Ogembo nchini Kenya, amekamatwa na Polisi wilayani Serengeti, Mkoa wa Mara kwa tuhuma za kutelekeza mtoto mchanga mwenye umri wa wiki moja kwa kile kinachodaiwa kuwa ni ugumu wa maisha.

 

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu akiwa nje ya Kituo cha Polisi Mugumu, Maria alisema alijifungua Mei 25, mwaka huu lakini baada ya kujifungua alijikuta katika mazingira magumu na kuwaza kwamba mtoto huyo ataishije, ndipo akaamua kumtelekeza katika nyumba ya mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Chacha Kisore, mkazi wa mjini Mugumu.

 

“Nilikuja Tanzania mwaka 2013 nikitokea Kenya na huku nilikuja kumsalimia bibi yangu lakini maisha tuliyokuwa tunaishi hayakuwa mazuri, nikaamua kuondoka nitafute kazi ili nipate nauli ya kurudi kwetu, ndipo nikapata huu ujauzito, nilipojifungua nikajikuta napata wakati mgumu wa kumlea mtoto ndio maana nikamtelekeza,’’ alisema Maria.

 

Akisimulia kwa masikitiko makubwa, alisema mwaka jana alikutana na kijana mmoja aliyemlaghai kwa kumpa shilingi 2,000 kisha alimpeka katika shamba la mihogo na kujamiiana naye ndipo alipopata ujauzito huo.

 

“Nilipopata mimba nilisaidiwa na mama mmoja ambaye nilikuwa namfanyia kazi lakini mateso yalizidi nikatoroka na siku ya kujifungua nilijifungulia njiani nikawa wa kutangatanga na mtoto wangu hadi siku hiyo nilipoamua kumuacha na kwenda kutafuta nauli ili nirudi kwetu,” alieleza Maria.

 

Akisimulia tukio la kuachiwa mtoto huyo, Annastazia Chacha (18) alisema Juni 2, mwaka huu, majira ya saa 12 jioni ndiyo siku alitelekezewa mtoto huyo. Alisema akiwa nyumbani kwao, alisikia mtu akibisha hodi na alipotoka nje na kufungua mlango akamkuta dada mmoja na mtoto mchanga akaomba maji ya kunywa.

 

“Nilimpa maji akanywa kisha akaniambia ‘naomba kujisaidia’, nikamuonyesha sehemu ya kwenda haja alipoenda akatokomea, hakurudi tena na nilipoenda kumuangalia sikumuona, wazazi wangu waliporudi nikawaeleza hali halisi,’’ alisimulia Anna.

 

Naye mama yake Anna, Elizabeth Chacha, alisema siku ya tukio akiwa anatoka katika mihangaiko yake alifika nyumbani majira ya saa moja usiku na kumkuta binti yake akiwa na mtoto mchanga na alipomuuliza ni wa nani, akamjibu ametelekezewa na mtu asiyemfahamu.

 

“Nilihisi kama utani nikaingia ndani nikaweka mizigo yangu nikarudi kumuuliza tena mtoto wa nani? Ndipo akanieleza kuwa kuna mtu alikuwa anatokea kliniki akapita hapa akaomba maji akampa, akauliza choo akamuelekeza ndio hakurudi tena,’’ alisema mama huyo na kuongeza:

 

“Nililala na mtoto mchanga, ilifika hatua akawa analia tuu usiku, sikuwa na jinsi ya kumhudumia chakula ikanibidi nimpe maziwa na chai ya rangi walau atulie kwa sababu alikuwa analia sana.” Asubuhi kulipokucha, walimpeleka kituo cha polisi na kuandika maelezo lakini walishauriwa wakae na mtoto huyo huku taratibu za kumtafuta mama wa mtoto zikiendelea.

 

Elizabeth alisema, walishirikiana na mumewe kupiga simu kwa ndugu zao wa vijijini kuomba msaada wa kumpata mama wa mtoto ndipo walipopata taarifa kutoka kwa ndugu yao kuwa kuna mtu ameonekana Kijiji cha Kebosongo akiwa kama mzazi lakini hana mtoto.

 

“Mume wangu alifuatilia na kuwaomba wamlete ili tumtambue kama ndiye na kweli tumefika hapa kituoni na binti yangu amembaini kuwa ndiye kutokana sura na mavazi aliyoyavaa na kanda mbili alizokuwa amevaa,’’ alifafanua.

 

Liliani Nyambuche ambaye ni Kamanda wa Polisi Dawati la Jinsia Magumu, alisema wamemkamata mtuhumiwa na amefunguliwa jalada na atakuwa chini ya ulinzi wakati upelelezi wa kesi yake ukiendelea.

STORI: JACQUELINE OISSO, UWAZI

Comments are closed.