MAMA ALALA NA NYOKA SIKU 14

MAMA mmoja aliyefahamika kwa jina la Asha Mohammed mkazi wa Boko Chama jijini Dar amejikuta katika mateso mazito kufuatia kupooza miguu na masikio yake kutosikia ambapo katika harakati za kutibiwa alijikuta akilazwa na nyoka chumbani kwa siku 14.  Akisimulia mkasa mzima ulivyokuwa mama huyo alisema, alizaliwa akiwa mzima lakini mwaka 2001 miguu ilianza kumsumbua baada ya kutoka kujifungua mtoto wa kwanza.

“Mimi nilizaliwa nikiwa mzima wa afya kabisa, lakini mwaka 2001 nilipopata mimba ya mtoto wangu wa kwanza ndio nikaanza kuugua miguu. Nilienda hospitali wakanitibu na kunipa dawa lakini kadri siku zilivyozidi kwenda ndivyo hali yangu ilivyozidi kuwa mbaya.

“Baada ya muda kidogo kupita nilipata ujauzito wa mtoto wangu wa pili na baada ya kujifungua ndio likazuka tena tatizo lingine la masikio. “Masikio yakaanza kuniuma, nikawa napata tabu kusikia ikabidi niende hospitali. Baada ya vipimo madaktari wakaniambia inatakiwa inunuliwe mashine ambayo itakuwa inanisapoti kuweza kusikia vizuri.

“Nilirudi nyumbani na kumwambia mume wangu kwa sababu mimi sikuwa na pesa ya kununua hiyo mashine ambayo inauzwa 200,000. Hata hivyo mume wangu hakuonesha kunijali. “Ikabidi ndugu zangu wanichangie na kufanikiwa kununua mashine ambayo niliitumia kwa miaka kadhaa lakini baadaye ikaacha kufanya kazi, nikawa nikiivaa sisikii kitu,” alisema mama huyo.

Akaongeza kuwa, hali ilizidi kuwa mbaya zaidi baada ya kujifungua mtoto wa tatu ambapo miguu ilizidi kupooza na hapo ndipo walipoanza kuhangaika hospitali mbalimbali bila mafanikio. “Ilifika wakati nilienda kwa waganga wa kienyeji nako bila mafanikio. Niliwahi kwenda kwa mganga mmoja huko Tanga. Nikakaa huko wiki mbili, nakumbuka nilikuwa nalala peke yangu kwenye chumba kimoja chenye giza, mimi nalala chini halafu juu kuna nyoka mkubwa ananiangalia.

“Nilikuwa naogopa sana lakini mganga akanihakikishia kwamba nisiogope kwani huyo nyoka hawezi kunidhuru kwa chochote na kulala kwake juu ndio ananilinda. “Ikafika wakati nikawa nimeshazoea ile hali ya kulala na yule nyoka na baada ya wiki mbili kuisha niliondoka pale bila mafanikio yoyote.

“Baada ya kuhangaika sana kwa waganga bila mafanikio, nikaona niende kwenye maombi lakini nako sikupata mafanikio, hali yangu bado ni mbaya, kutembea ndiyo hivyo kwa shida na masikio nayo hayafanyi kazi.

“Nawaomba Watanzania wanisaidie katika mambo matatu, kwanza nipone hii miguu, pili nisaidiwe pesa ya kununulia mashine ya kunisaidia kusikia na tatu nipate hata pesa ya mtaji ili mwanangu mkubwa angalau afanye biashara tutape pesa ya kula,” anasema mama huyo kwa masikitiko huku akiitaja namba yake ambayo unaweza kumtumia chochote kuwa ni 0789143003.


Loading...

Toa comment