The House of Favourite Newspapers

Mama aliwa na mamba mbele ya wanaye!

0

STORI: Stephano Mango, Wikienda

Ruvuma: Inauma sana! Mwanamke Sharifa Makunganya, mkazi wa Kijiji cha Tulingane Kata ya Lukumbule wilayani Tunduru mkoani hapa, anadaiwa kuliwa na mamba wakati akioga kandokando ya Mto Ruvuma, tukio ambalo lilitokea mbele ya wanaye.

Habari zilizopatikana wikiendi iliyopita kutoka Tunduru na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, ACP Zuberi Mwombeji zilisema kuwa, tukio hilo lilijiri mchana wakati Sharifa akitokea shambani na wanaye wawili wakielekea nyumbani.

Kamanda Mwombeji alifafanua kuwa, wakati Sharifa akioga ili aende nyumbani akiwa msafi, ghafla alikamatwa na mamba kisha kuzama naye mtoni na kwamba hadi sasa bado hajaonekana hivyo jitihada zinafanywa kumpata kama yupo hai.

ACP Mwombeji alisema kuwa, kikosi cha polisi na askari wa wanyama pori wameshafika eneo la tukio hivyo taarifa kamili itapatikana watakaporejea ofisini.

Hata hivyo, kamanda huyo alitoa wito kwa wananchi wanaoshi jirani na Mto Ruvuma kuungana na polisi na askari wa wanyama pori kumsaka mamba aliyemkamata Sharifa na ameonya watu wenye tabia ya kuoga kwenye mto huo waache mara moja kwani una mamba wengi.

Leave A Reply