The House of Favourite Newspapers

Mama Aliyeuawa kwa Jembe, Nyumba Yake Yaezuliwa Bati

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida wanandugu wa mwanamke Roza Fungwa, mkazi wa Kitongoji cha Magharibi kilichopo katika Kijiji cha Mwibagi, Kata ya Kyanyari, Wilaya ya Butiama mkoani Mara anayedaiwa kupigwa na kuuawa kwa jembe na mumewe aitwaye Fungwa Busia Aprili Mosi mwaka huu, wameamua kugawana watoto wa mwanamke huyo kwa ajili ya kuwalea na kisha kuezua mabati ya nyumba alimokuwa akiishi mama huyo.

 

Mwanamke huyo anadaiwa kuzikwa na mumewe huyo kusikojulikana kwa madai ya kumzuia mtoto wao wa kike (14), asiolewe na mzee wa miaka 60, hivyo mume kukasirika.

 

Mdogo wa mwanamke huyo, Ikunga Majige alisema kwamba wanandugu hao waliamua kuchukua uamuzi huo wa kuezua bati na kuwachukua watoto baada ya kuona wanateseka na hawana tena mtu wa kuwatunza. Alisema walijitahidi kutafuta mahali alipozikwa mama huyo bila mafaniki na baba yao anayetuhumiwa kufanya mauaji hayo bado anashikiliwa na polisi.

 

Majige alidai kuwa baada ya kumtafuta dada yake huyo ili kujua amezikwa wapi bila mafanikio, waliamua kugawana watoto wake na pia kuezua mabati ya nyumba alimokuwa akiishi kwa madai kuwa yeye na kaka yake mkubwa ndio walioyanunua na kumjengea dada yao huyo baada ya kuona analala kwenye nyumba ndogo isiyokidhi.

 

Aidha katika hatua nyingine Majige alieleza kwamba, mara baada ya kukosa mahali alipozikwa dada yake wanandugu wameamua kugeukia upande mwingine wa pili wa kupigiwa ramli na waganga wa kienyeji maarufu kama Sangoma ili waelekezwe mahali ulipozikwa mwili wa ndugu yao huyo.

 

Ikunga alidai kuwa, tayari wameishakwenda kwa sangoma watatu kupigiwa ramli lakini cha kushangaza ni kuwa kila sangoma aliyewapigia ramli hutoa matokeo tofauti na mwingine, hivyo kuachana nao.

 

“Ramli hizo za waganga zimezidi kuichanganya familia yetu kutokana na kutofautiana, hivyo tunashindwa kuelewa ni mganga yupi anayesema ukweli juu ya mahali alipo mpendwa watu huyo ili kama ameuawa walau tuupate mwili huo tuuzike ili watoto wake wawe wanaliona kaburi la mama yao,” alisema.

 

Hata hivyo, Ikunga alieleza kwamba familia zote mbili ya mke na ile ya upande wa mwanaume zinaamini kuwa mwanamke huyo aliuawa na mumewe kutokana na maelezo ya watoto ambao walidai kushuhudia tukio.

STORI: GREGORY NYANKAIRA,MARA

Comments are closed.