The House of Favourite Newspapers

MAMA AMFANYIA UNYAMA MWANAWE!

KUWEKA nia ya kuchemsha maji ya moto kwa kiwango cha nyuzi joto 100 ili uyatumie kumwagia mtoto wako unayemtuhumu kuiba chupa mbili tupu za soda sijui kitendo hicho kinafaa kuitwa unyama au kuna lugha nyingine?  

 

Uwazi gazeti la mikasa na matukio limenasa hivi karibuni habari ya mama mmoja aitwaye Jeny Auma, Mkazi wa Kwa Morombo jijini hapa, akituhumiwa kumjeruhi vibaya mtoto wake wa kufikia kwa kumchoma na maji ya moto mwilini.

 

Kwa mujibu wa chanzo chetu; kisa cha mama huyo kutuhumiwa kufanya unyama huo ni kudai mwanaye aliyetajwa kwa jina la Joseph Baraza ‘12’ kauza chupa mbili za soda ambazo thamani yake ni shilingi 600.

 

“Kwanza alianza kumtukana na kumpiga, akaona haitoshi akachemsha maji akamwagia, kitendo hicho kimetuuma sana sisi kama wazazi,” kilidai chanzo chetu kinachoishi karibu na mama huyo anayetuhumiwa.

 

Joseph amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru kwa ajili ya matibabu baada ya kujeruhiwa vibaya kwa maji hayo ya moto sehemu za shingoni na mgongoni. Akizungumza na Uwazi akiwa hospitalini hapo, Joseph alidai kuwa, mama huyo amekuwa akimtesa na kumfanyia vitendo vya ukatili.

 

“Siyo mimi tu, hata watoto wake aliowazaa nao anawatesa tu, kuna wakati huwa anatupiga kwa zamu huku akitutishia kutuchoma moto,” alidai Joseph. Joseph alisema tukio hilo lilitokea Jumapili, Novemba 26, majira ya jioni, ambapo mama huyo anadaiwa kuandaa maji ya moto na kuanza kumvizia mwanaye huyo ili amuunguze nayo.

 

“Nilikataa kunywa chai baada ya kugundua aliniwekea mtego, nilijua nikikaa atanifanyia kitu kibaya, nilishtuka na kuanza kutoka nje. “Nilipofika getini ile nataka kufungua geti nilishtukia kitu cha moto kinaniingia mwilini kuanzia shingoni hadi mgongoni nilipata maumivu makali sana,” alisema Joseph.

 

Aliongeza kuwa, baada ya tukio hilo alikimbilia kwa jirani ambako alipata msaada wa kumpeleka hospitalini.

Baadhi ya majirani, Solomon Chatale na Zainabu Jumanne waliliambia Uwazi kuwa, wamesikitishwa na tukio hilo huku wakidai kuwa, si mara ya kwanza kwa mama huyo kuwafanyia ukatili watoto wadogo.

“Kabla ya hapo amewahi kumwagia maji ya moto mtoto wake wa kiume aitwaye Doto, mwingine alimvunja mkono kwa kipigo, alidai Zainabu. Naye Chatale aliiomba serikali kuchukua hatua kali kwa mama huyo ambaye kwa sasa ametoweka na hajulikani alipo na polisi wanaendelea kumsaka ili afikishwe kwenye vyombo vya sheria.

 

Kamanda wa polisi Mkoa wa Arusha Ramadhani Ng’anzi amesema, bado polisi wanamsaka mama huyo na wamemtaka popote alipo ajisalimishe kituo cha polisi kwani vyombo vya dola vina mkono mrefu na kwamba lazima atakamatwa. Hata hivyo baadhi ya watu walimtuhumu baba wa mtoto Joseph kuwa, ameshindwa kuwa mlezi bora wa familia yake.

 

“Huwezi kuwa baba kwenye nyumba halafu kila siku unakuta mkeo kawafanyia watoto unyama unakaa kimya, maana yake nini, mimi nashauri mwanaume naye ahojiwe na polisi,” alisema jirani mmoja ambaye hakupenda jina lake liandikwe.

STORI: JOSEPH NGILISHO, ARUSHA

Comments are closed.