MAMA AMPOTEZA MWANAYE MWAKA WA 20 SASA, ‘NISAIDIENI APATIKANE’

HII siyo filamu bali ni kweli, ule msemo wa ‘Uchungu wa mwana aujuaye ni mzazi’, unamaanisha kwa mama huyu aliyejitambulisha kwa jina la Martha Kifunda ambaye anasema amekuwa akimtafuta mwanaye wa kiume kwa miaka 20 sasa.

 

Kwa sasa mzazi huyo ambaye sasa amekuwa akisumbuliwa na msongo wa mawazo ambao unasababisha kuanza kupata ugonjwa wa kupooza upande mmoja, anamtafuta mwanaye aliyeondoka nyumbani mwaka 1999 ambaye jina lake ni Robert Gerard Kiama Pius.

 

“Hadi leo naikumbuka siku ya mwisho aliyoniaga, tulikuwa tukiishi Tanga, kauli yake, muonekano wake, upole wake, bado navikumbuka hadi muda huu, naomba kumwambia mwanangu popote alipo, mimi mama yake namtafuta, kama ameshakufa basi nataka nijue tu ili nafsi yangu itulie,” anasema Martha.

 

Akizungumza na gazeti hili wiki iliyopita akiwa Kibaha mkoani Pwani kwa ndugu zake alikofikia kwa ajili ya matibabu akitokea Tanga, anasimulia:

“Nilikuwa naishi na mwanangu Tanga, alipohitimu kidato cha nne Shule ya Kwemvumo ipo Mombo, kuna wakati aliondoka na kwenda kumtafuta baba yake ambaye mara ya mwisho nilisikia alikuwa Magu mkoani Mwanza akiwa ni mwalimu katika Shule ya Nasa.

 

“Mimi ndiye nilimpa nauli na baraka zote za kwenda kumtafuta, lakini alirejea baada ya kumkosa. Tukaendelea kuishi kama kawaida, kutokana na maisha kuwa magumu kuna siku aliniaga kuwa anakwenda Dar es Salaam kutafuta maisha.

“Ilikuwa mwaka 1999, kweli alisafiri hadi Dar na kufikia kwa ndugu zangu hawa (anaoishi nao sasa) wakati huo walikuwa wakiishi Kiwalani, akakaa hapo kwa siku mbili, baadaye napo aliaga kuwa anakwenda kutafuta maisha, tangu hapo hatujawahi kumuona tena.

“Jina kamili la mwanangu ni Robert Gerard Kiama Pius lakini kuna wakati alikuwa akitumia jina la Robert Kifunda, hilo Kifunda ni jina la kwetu upande wa mama. Aliamua kwenda kumtafuta baba yake mara ya kwanza ili amsomeshe kwa kuwa mimi nilikuwa sina uwezo huo kwa alipokuwa amefikia.

 

“Huyo baba yake ambaye alikuwa akimtafuta anaitwa Pius Pascal Hung’wani Shilungu, naye sijui alipo kwa kuwa tulipotezana miaka mingi na wala sina taarifa za ndugu wala rafiki yake yeyote.

“Nimeshajaribu mara nyingi kutamfuta hata huyo kwa baba yake lakini hadi leo naye sijawahi kumpata na sijui naye kama yupo hai au ameshatangulia mbele ya haki.”

 

Mwanao alikuwa ni mtu wa aina gani?
“Alikuwa mpole na hakuwa mtu wa kujichanganga na vijana wa mtaani na hakupenda makundi. Ni mtoto wangu wa kwanza, mdogo wake yupo anaitwa Rogecy na anafanya kazi huko Longido.

 

Robert aliwahi kuwasiliana na wewe baada ya kuondoka?
“Hajawahi kunitafuta tena, naumia sana, yawezekana huu ugonjwa wa kupooza ni njia ya mimi kumpata mwanangu, kwani naomba kama anasoma au kama kuna mtu yeyote ambaye atasoma haya maandishi unayoandika, basi amjulishe kuwa mimi mama yake ninamtafuta sana.

 

“Huu ni mwaka wa 20, sijakata tamaa, Mungu ni mkubwa naamini nitampata, naomba msaada kwa yeyote anayefahamu awasiliane na mimi au familia yangu.

 

“Namba yangu ni 0717 948519, namba za ndugu zangu ambazo pia wanaweza kuwasiliana nazo ni 0715 795465, 0658 764141 au 0714 899393.”

Kwa yeyote ambaye anamfahamu Robert au anataarifa zake zozote pia anaweza kuwasiliana na mwandishi wa habari huu kupitia namba 0713393542.

Na John Joseph.

 

EXCLUSIVE: BARNABA Siilaumu BASATA…Sipendi kuhujumu mtu yoyote

Loading...

Toa comment