MAMA ASIMULIA GARI LA SERIKALI LILIVYOMKATA MIGUU

INASIKITISHA! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya mama mmoja, Amina Isumaili Jola (59), Mkazi wa kijiji na Kata ya Nyengedi, Wilaya ya Lindi, kufunguka kwa kueleza kwamba binadamu kabla hujafa hapa duniani bado hujaumbika.  

 

Mama huyo alisema hayo alipozungumza na mwandishi wa gazeti hili hivi karibuni kijijini Nyengedi kufuatia kukatwa miguu yake baada ya kugongwa na kupondwa na gari la Serikali la Idara ya Maliasili mjini hapa.

 

Akisimulia mkasa huo mama huyo alikuwa na haya ya kusema: “Mimi niliyekuwa najitafutia riziki kwa kutumia nguvu zangu, leo nimekuwa mtu wa kusaidiwa, hakika mwacheni Mungu aitwe Mungu. “Sitaweza kuyasahau mateso haya hadi mwisho wa maisha yangu yote nitakayoishi hapa duniani, nikijiangalia sina mtoto hata mmoja baada ya watoto wangu watatu niliojaliwa kupewa na Mungu kutangulia mbele za haki.”

 

Jola ambaye kwa sasa ni mlemavu asiyeweza kutembea baada ya kupoteza viungo , kufuatia kukatwa miguu kulikosababishwa na ajali ya kugongwa na gari ndogo aina ya Tyota Land Cruser la Idara ya Maliasili Lindi vijijini akiwa kwenye harakati za kujitafutia maisha miaka sita iliyopita.

 

Akisimulia kwa kina mama Jola alisema anakumbuka alipata ajali hiyo saa 5:0 asubuhi januari 20, mwaka 2012 akiwa kwenye pikipiki akitoka nyumbani kwake Kijiji cha Nyengedi kwenda Kata ya Rondo katika shughuli zake za kufuatilia biashara zake.

 

Alisema wakiwa wanakwenda Rondo njiani walikutana na gari dogo na kumfanya dereva wake wa pikipiki kuchukuwa tahadhari kwa kusimama kando ya barabara kulipisha gari hilo lipite na wao waweze kuendelea na safari lakini ghafla wakagongwa.

 

‘’Nilipoteza fahamu kwa siku tatu lakini baada ya kurudiwa na fahamu niliambiwa kwamba gari lile ilikuwa inampeleka Meneja wa Idara ya Misitu (jina tunalihifadhi) kwenda mkoani Mtwara kuwahi usafiri wa ndege,’’alisema Bi Jola.

 

Alifafanua kuwa baada ya kugongwa na kupoteza fahamu, wasamaria wema waliokuwa wakipita katika barabara hiyo ya walimsaidia kwa kufikishwa Hospitali ya Nyangao alikokuwa amelazwa na kupatiwa matibabu yaliyoenda sanjari na kukatwa miguu baada ya kubainika imepondekapondeka kwa kukanyagwa na gari hilo.

 

Alisema alipozinduka baada ya siku tatu tangu apate ajali hiyo, askari Polisi wawili walifika hosptali alikolazwa na kumchukuwa maelezo, lakini kwa vile alikuwa katika masikitiko ya kukosa miguu yake hakuweza kufahamu walikuwa na lengo gani.

 

Mama huyo anaeleza akiwa bado yupo Hospitalini,kupitia kwa majirani zake alipata taarifa kuwa dereva aliyemgonga na kusababisha ulemavu wa kudumu katika maisha yake amehukumiwa kulipa faini ya Sh,50,000/-. ‘’Nimeshangazwa mno, inakuwaje mshitakiwa amepewa hukumu wakati mimi mlalamikaji sikuitwa kutoa maelezo yangu mahakamani,’ alilalamika Bi Jola.

 

Alisema baada ya kutoka hospitalini, yeye na baadhi ya ndugu na majirani walilazimika kwenda Ofisi ya Idara ya Maliasili Lindi kukutana na uongozi ili kuona namna ya kumsaidia kuendesha maisha yake ambapo walimuahidi kumjengea nyumba ndogo ya vyumba vitatu, kumfungulia biashara na kumpatia baiskeli ya magurudumu matatu.

 

“Pamoja na ahadi zote hizo niliambulia kupatiwa baiskeli iliyonunuliwa kutoka viwanda vidogovidogo (Sido) lakini ahadi  nyingine sikutimiziwa naomba usiku na mchana Rais John Magufuli atembelee hapa na nipate nafasi ya kumuambia uonevu huu,” alisema mama huyo huku akifuta machozi.

 

Meneja Maliasili Misitu, Wilaya ya Lindi, Gasper Mweta, alipoulizwa juu ya madai hayo, amekiri gari la idara anayoingoza kumgonga Jola miaka sita iliyopita lakini hakuwa tayari kuzungumzia utekelezaji wa ahadi walizotoa.

Stori: SAID HAUNI, Lindi


Loading...

Toa comment