The House of Favourite Newspapers

Mama, baba lishe washiriki maadhimisho siku ya afya ya mazingira

0

Kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa Chama Cha Maafisa Afya (CHAMATA) ,Baraka Mhina, aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo Emmanuel Mwandepa (anayezungumza katikati) na Ofisa Afya wa Manispaa ya Ilala, Fatuma Maduhu.

Meza kuu ikisikiliza risala iliyokuwa ikisomwa kutoka kwa washiriki wa maadhimisho hayo.

Baadhi ya akina mama lishe na baba lishe wakiwa kwenye maadhimisho hayo.
Maadhimisho yakiendelea ukumbini hapo.

Sehemu ya akina mama lishe wakifuatilia maadhimisho hayo.

MAMA lishe wakishirikiana na baba lishe kupitia Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, jana wameadhimisha siku ya Afya ya Mazingira nchini.Maadhimisho hayo yamefanyika katika ukumbi wa Arnatougoulou uliopo maeneo ya viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, ambapo mama lishe na baba lishe walipata fursa ya kushiriki maadhimisho hayo.

Akisoma risala kwa mgeni rasmi, Katibu wa Chama Cha Maafisa Afya Manispa ya Ilala (CHAMATA), Sophia , alisema kuwa siku ya Afya ya Mazingira Duniani huadhimishwa kimataifa Septemba 26 kila mwaka na shughuli mbalimbali za kijamii hufanyika.

Alisema kuwa siku hiyo hapa nchini haijawahi kuadhimishwa kwa mujibu wa kalenda ya kitaiafa, hivyo wameona umuhimu wa kuiadhimisha siku hiyo kwa mara ya kwanza hapa nchini ili kuweza kuikumbusha jamii kuhusu majukumu yake katika afya ya mazingira.

Akiendelea kusoma risala hiyo, Ntomola alisisitiza kuwa shughuli za afya ya mazingira zimekuwa zikikosa nafasi ya kutosha kwa kutotangazwa na kutofanyika katika maeneo mbalimbali katika jamii. Hali hiyo husababisha shughuli hizo kukosa kipaumbele na hivyo majukumu ya afya ya mazingira kudorora, kuleta athari nyingi za kiafya zikiwemo, uchafu wa mazingira, milipuko ya magonjwa kama kipindupindu, homa ya matumbo, malaria, minyoo, hata homa ya ini.

Aliongeza kuwa CHAMATA kwa kushirikiana na Chuo Cha Maafisa Afya wa Mazingira kilichopokatika Hospitali ya Muhimbili (MUHAS) kilitoa mafunzo maalum kwa mama na baba lishe wapatao 200 kwa ajili ya kuwajengea uwezo kwenye maeneo ya usafi binafsi. Usafi wa mazingira ni pamoja na kuandaliwa vyakula, usafi wa vyombo vya chakula, usalama wa maji, kufahamishwa madhara yatokanayo na matumizi ya vyakula vilivyoandaliwa katika mazingira hatarishi.

Aidha alisema mashirika na wadau wengine pia wanayo fursa ya kujitokeza kusaidia kundi kama hilo muhimu katika jamii hasa ikizingatiwa kwamba magonjwa mengi ya kuambukiza yanayosumbua jamii yetu yanasababishwa na ulaji wa vyakula na maji yasiyo salama.

Maadhimisho hayo yalikuwa na kauli mbiu isemayo ’Afya na maisha bora kwa mtoto’ huku mgeni rasmi, Emmanuel Mwandepa, akiahidi kufuatilia kwa karibu katika ngazi ya wizara ili maadhimisho yajayo yaingizwe kwenye kalenda ya taifa na kuweka vipaumbele na bajeti kwa kipindi kijacho kwa manufaa ya Afya ya Mazingira na jamii kwa ujumla.

(NA DENIS MTIMA/GPL)

 

Leave A Reply