The House of Favourite Newspapers

Mama, Mwana Jela Miaka 40 kwa Kukutwa na Vipande 8 vya Nyumbu

0
Mahakama ya Wilaya ya Itilima, Simiyu.

MAHAKAMA ya Wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu, katika kesi yake ya kwanza kuitolewa hukumu tangu izinduliwe Novemba 25, 2022 na Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahimu Juma imewahukumu watu wawili ambao ni Mama na mtoto wake kutumikia kifungo cha miaka 20 kila mmoja baada ya kukiri kosa katika kesi ya uhujumu uchumi iliyokuwa inawakabili.

 

Ikiwa ni kesi ya kwanza ya uhujumu uchumi kusajiliwa na kutolewa hukumu kwenye Mahakama hiyo, lakini pia ikiendeshwa kwa muda mfupi wa saa moja na kutolewa hukumu baada ya washtakiwa kufikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza na kukiri kosa.

 

Kija Matu (60) na Mayunga Juma (30) ndiyo waliokumbana na adhabu hiyo baada ya kukiri kosa la kukutwa na nyara za serikali ambazo ni vipande 8 vikavu vya mnyama aina ya Nyumbu kinyume cha sheria vikiwa na thamani ya Sh. Milioni 1,517,100.

 

Katika kesi No. 1 ya mwaka 2022 ya uhujumu uchumi, kabla ya hukumu hiyo washtakiwa walisomewa mashtaka yao na Mwendesha mashtaka mkaguzi msaidizi wa polisi kutoka ofisi ya mashtaka Jaston Haule.

 

Walikutwa na nyara za serikali kinyume na kifungu cha 86 (1) (2) (c) (iii) cha sheria No. 5 ya mwaka 2009 ya uhifadhi wa wanyamapori kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

 

Mwendesha mashtaka huyo akielezea mahakama, alisema kuwa sheria hiyo ikisomwa kwa pamoja na kifungu cha 57 na 60 (2) cha sharia ya uhujumu uchumi sura ya 200 kama ilivyofanyiwa marejeo 2022.

 

Jaston alisema kuwa washtakiwa wote wawili mnamo Desemba 05, 2022 majira ya saa 4:00 usiku katika Kijiji cha Laini ‘B’ Wilayani Itilima mkoa wa Simiyu walikamatwa na kufanyiwa upekuzi na kukutwa na vipande hivyo 8 vikavu vya Nyumbu.

 

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa wote wawili walikiri kosa na Hakimu mkazi mfawidhi Robert Kaanmwa aliyekuwa anasikiliza kesi hiyo kutoa adhabu ya kwenda jela kwa kila mmoja kutumikia kifungo cha miaka 20.

Derick Milton, Simiyu.

Leave A Reply