The House of Favourite Newspapers

Mama: Nateseka miaka 10 kitandani

0

DAR ES SALAAM: Nateseka jamani! Hiyo ni sauti ya unyonge iliyoonesha kukata tamaa iliyotoka kinywani mwa Zaituni Mgeni (43) mkazi wa Kibada, Kigamboni jijiji Dar baada ya kuugua ugonjwa wa ajabu uliosababisha mguu wake wa kushoto kuvimba na kushindwa kutembea kwa takriban miaka 10.

Akizungumza na waandishi wetu ndani ya chumba kimoja anachoishi na mwanaye, Zaituni alisimulia kuwa alianza kupatwa na tatizo hilo tangu mwaka 1990 ambapo alitokwa na kipele ambacho kilionekana kukua kadiri siku zilivyosonga mbele na baadaye mguu huo ulizidi kuvimba na kumsababishia ashindwe kutembea hivyo kulazimika kushinda ndani kwa takriban miaka 10.

“Nilianza kuhisi kuwashwa tangu mwaka 1990 nikajua ni kipele cha kawaida, muda ulivyozidi kwenda mbele nikaona maumivu yanazidi kuongezeka. Nilikwenda Hospitali ya Zakhem na baadaye Hospitali ya Temeke lakini madaktari waliniambia sina tatizo.

“Baadaye nilikwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili nikaonana na daktari ila hakunipima zaidi ya kuniangalia na kusema hakuna tatizo.

“Mwaka 2016 mguu ulizidi kuuma na uvimbe kuzidi kuwa mkubwa wa kutisha na mguu kujikatakata pingilipingili kama unavyoona (akimuonesha mwandishi).

“Mwezi Januari niliamua kwenda tena Muhimbili nikaonana na daktari ila sikupata vipimo vyovyote zaidi ya madaktari kuuangalia mguu na kushauri nikatwe, nikaomba muda wa kufikiria kuhusu kukatwa kwani maisha ninayoishi ni ya shida sasa nikikatwa tena mguu naona kama matatizo yataongezeka. Mpaka leo sijajua nini hatma yangu,” alisema Zaituni.
Zaituni amewaomba Watanzania wamsaidie kwa hali na mali ili aweze kupata matibabu ya kina.

“Nawaomba Watanzania wenye kuguswa na tatizo langu wanisadie niweze kupata huduma ya matibabu, yeyote aliyeguswa na tatizo langu anaweza kuwasiliana na mimi kwa namba 0679 525295 jina kamili ni Zaituni Mgeni.”

Leave A Reply