MAMA ROMMY APEWA TALAKA POLISI

DAR ES SALAAM: MAMA yake DJ Rommy Jones, Shani Swedy anadaiwa kuzua kasheshe la aina yake alipokuwa akidai talaka yake hivyo suala hilo kutinga na kumalizikia Polisi, Gazeti la Ijumaa limenasa ubuyu mwanzo mwisho.

 

TUJIUNGE NA CHANZO

Kwa mujibu wa chanzo makini, Shani ambaye ni mama mkubwa wa staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, aliolewa na jamaa anayefahamika kwa jina la Ajazi Jabir, mkazi wa Magomeni- Mikumi jijini Dar, lakini baadaye mwanaume huyo alikutana na mwanamke mwingine akamuoa na kukata mawasiliano na Shani.

 

“Unajua Shani ni mkubwa sana kwa Ajazi, amemzidi karibu miaka tisa hivi na hata ukiwaangalia, mwanamke ni mkubwa kuliko mwanaume. Hivyo inaonekana mwanaume alipompata mwanamke wa saizi yake ambaye ni Rutty Kevella, akaamua kumuoa na kuachana na mama Rommy ambaye kimtazamo ni kama mtu na kiben’teni wake,” kilidai chanzo hicho makini.

 

FULL VITUKO

Chanzo hicho kilizidi kuweka wazi kuwa, kwa kuwa Ajazi hakumpa talaka Shani, maisha yao yamekuwa ya kugombanagombana mara kwa mara. “Yaani Shani inaonekana ni kama hajakubaliana na kuachwa, kuna wakati anakuwa anaitaka talaka, lakini kuna wakati anasema haitaki bali anamtaka mumewe,” kilisema chanzo hicho.

SIKU YA TUKIO SASA

Kikisimulia siku ya tukio lililotokea hivi karibuni nyumbani kwa Ajazi, chanzo hicho makini kilieleza kuwa, Ajazi akiwa na mkewe nyumbani majira ya saa 2:00 usiku, Shani alifika nyumbani hapo na kuanza kufoka akidai anamtaka mumewe.

 

“Ilikuwa hatari nakuambia, mama kaja amecharuka kwelikweli, sasa Ajazi na mkewe waliokuwa ndani walishindwa kutoka kwa sababu hawakujua amekuja na silaha gani. Alipoona Ajazi hatoki, alianza kumsema sana mke mdogo na kumuambia atahakikisha na yeye anaachika katika hiyo ndoa na akamtishia kabisa maisha yake mke mdogo.

 

“Wakati akiendelea kutukana, Ajazi na mkewe wakamuacha asemee weee baadaye walipohakikisha ameondoka, wakaenda kutoa taarifa Polisi Magomeni usiku huohuo.

 

SHANI AITWA POLISI

“Shani akapigiwa simu usiku huohuo na Polisi akafika kituo cha Polisi sasa wakati anahojiwa na Polisi alikuwa mkali kwelikweli na kutishia kuwa anajulikana. “Alipoulizwa kwa nini amekwenda kufanya fujo nyumbani kwa watu na shida yake ilikuwa ni nini, mara alisema alimfuata mumewe anamhitaji, mara akasema anataka talaka,” kilisema chanzo hicho.

 

USHAURI WATOLEWA

Baada ya kusikiliza pande zote, Polisi walilazimika kuwashauri mke mkubwa apewe talaka ili jambo hilo liishe ikapangwa suala hilo lifanyike kituoni hapo siku iliyofuata. “Sasa kesho yake Shani hakufika pale Polisi, lakini bahati nzuri mume alishaandika talaka hiyo na kufika nayo pale kituoni na ikashauriwa itumwe kwa mshenga halafu Shani ataarifiwe akaichukue,” kilisema chanzo.

MKE MDOGO AFUNGUA MASHITAKA

Chanzo kiliendelea kueleza kuwa, baada ya ishu ya talaka kukamilika Polisi walimshauri mke mdogo afungue mashitaka kwa ajili ya usalama wake kutokana na vitisho alivyopewa na Shani. “Ikabidi mke mdogo afungue mashitaka kwa usalama wake maana Shani aliapa kula naye sahani moja ikiwa ni pamoja na kuhakikisha anaachika kwenye ndoa,” kilidai chanzo hicho.

 

MUME AZUNGUMZIA VURUGU

Gazeti la Ijumaa lilizungumza na Ajazi ambaye alithibitisha kumpa talaka mwanamke huyo baada ya kumfuata usiku nyumbani kwake na kufanya vurugu. “Ni kweli alikuja, akafanya vurugu, tukaenda Polisi, lakini nimeshampa talaka yake,” alisema Ajazi.

 

MKE MDOGO ANASEMAJE?

Baada ya kumalizana na mume, Gazeti la Ijumaa lilizungumza na mke mdogo ambaye ndiye anaishi na Ajazi kwa sasa ambapo alieleza jinsi Shani alivyofika nyumbani kwake na kufanya timbwili kabla hawakumfikisha Polisi. Alisema pamoja na kumalizana naye Polisi kwa talaka, lakini bado Polisi walimshauri afungue jalada la kesi ambalo lilisomeka MAG/RB/1420/2019 KUTISHIA KUUA KWA MANENO.

ATOA POVU KAMA LOTE…

“Ameshanifanyia mambo ambayo kila nikikumbuka naumia sijawahi hata siku kumtukana, ameshaniambia yeye mtu mzima, lakini simfikii yeye kwa sura yake alikuwa anamaanisha mimi mbaya mimi sijui usafi akaona haitoshi, nimeumia sana maana yeye mkubwa kwangu na ananizaa mimi yaani hayapiti maneno kila siku mara mimi nimemuua sijui nani.

 

“Najua ndiyo yeye mwezangu ana uwezo familia yao mimi choka mbaya nitaongea nini ila naumia sana Mungu ndiye atanilipia mume wangu ananipenda kwa dhati na sijamfanyia chochote ili anipende hivi mwanaume amekuacha miaka minne wewe bado unamfuata, kisa talaka kweli?

 

“Sasa talaka ameshapewa, mimi sitaki tena maneno na yeye ameshasema atanionesha, atafanya juu chini niachwe ila namwambia hakuna mwanzo ulikosa kuwa na mwisho, kama Mungu akiandika iwe itakuwa tu na kama hajaandika mimi kuachana na mume wangu basi sitaachana naye, afanye afanyavyo namtegemea Mungu yeye binadamu tu, ikitokea nimeachwa nitaachika sitamganda mwanaume kama gundi,” alisema Ruthy.

 

MKE MKUBWA ANENA

Alipopigiwa simu mke mkubwa kuhusu suala hilo hakutaka kuzungumza zaidi ya kusema yeye alichokuwa anakihitaji ni talaka na kwa kuwa ameshapewa, basi hana mpango nao tena. “Mimi nilikuwa nahitaji talaka yangu bwana hayo mambo mengine hayana ukweli wowote bwana,” alisema na kukata simu. Alipotafutwa Kamanda wa Polisi wa Kinondoni, ACP Mussa Taibu simu yake iliita bila kupokelewa.


Loading...

Toa comment