MAMA WA KANUMBA KUBURUZWA KORTINI

DAR ES SALAAM: BALAA jipya! Mama wa aliyekuwa msanii maarufu wa filamu nchini marehemu Steven Kanumba, Flora Mtegoa anatarajiwa kupandishwa mahakamani; chanzo kikitajwa ni mali za mwanaye.

 

Akizungumza kwa njia ya simu akiwa nyumbani kwake Shinyanga, baba wa marehemu Kanumba, Charles Kanumba aliliambia Amani kuwa, anamshtaki mzazi mwenzake huyo kutokana na kumaliza mali za mwanaye ikiwemo magari na fedha kiasi cha shilingi milioni 15.

 

Fedha hizo zinadaiwa kulipwa kwa Kanumba kutoka Kampuni ya Steps Entertainment aliyokuwa akifanya nayo kazi.

“Ninachotaka ni kupata haki yangu kama baba, maana mama Kanumba asingeweza kupata mtoto bila mimi, mali zote kama magari, ofisi na fedha amekula mwenyewe amemaliza, wiki hii natarajia atapandishwa mahakamani na nimemtuma mwanangu jijini Dar es Salaam ili alishughulikie hilo zoezi.

“Kingine naomba huyo mama asitumie jina la Kanumba maana siyo la kwake hivyo atumie la huko kwao,” alisema baba Kanumba kwa hasira.

 

Kwa upande wa mtoto wa baba Kanumba anayejulikana kwa jina la Mijanael Charles Kanumba aliyetumwa kuja Dar kushughulikia malalamiko ya baba yake alisema, tayari wameshapeleka shauri la mirathi Mahakama Kuu ambako walielekezwa waende Bodi ya Filamu na Steps.

 

“Tulifika Steps na mwanasheria wetu tukaambiwa tayari mama Kanumba ameshapewa milioni 15 alizokuwa akidai Kanumba hivyo wiki hii tutarudi tena mahakamani kufungua kesi ya madai dhidi ya mama Kanumba. “Kwa kuwa amemaliza fedha na mali zote za Kanumba mwenyewe itabidi auze hata nyumba ili wagawane sawa na baba maana hakumzaa mwenyewe marehemu Kanumba,” alisema Mijanael.

 

MSIKIE MAMA KANUMBA

Ili kuleta usawa wa habari, Amani lilimtafuta mama Kanumba ili kumsikia anasemaje kuhusiana na kupandishwa mahakamani kwa tuhuma za kula mali za marehemu mwanaye ambapo alisema, uamuzi wa baba Kanumba ni mzuri sana ili kumaliza mgogoro na maneno ya kila kukicha.

“Kama kweli Kanumba ni mwanaye basi aende mahakamani kwa sababu mpaka anakufa alikuwa hajui anaishije na hata baada ya kufa alikataa msiba usifanyike nyumbani kwake Shinyanga na mpaka sasa ni miaka saba hajawahi kuona kaburi la huyo anayedai kuwa ni mwanaye.

 

“Mahakama ndiyo itakayoamua haki, yeye ataenda na vithibitisho vyake kama kweli Kanumba ni mwanaye na aliwahi kumsaidia chochote na mimi nitaenda na vyangu na kama aliwahi kunioa na kunitolea mahari hapo ndipo atakapoeleza, naamini tutakata mzizi wa fitina na kuondokana na kero hii ya kila siku maana nimeshachoka,” alisema mama Kanumba.

 

TUJIKUMBUSHE

Kanumba alifariki dunia Aprili 7, 2012 ambapo kifo chake kiliacha wingu zito katika familia yake na tasnia ya filamu chini, huku mali alizoacha zikibaki mikononi mwa mama yake ambaye ndiye aliyekuwa na ukaribu naye.

Loading...

Toa comment