The House of Favourite Newspapers

Mambo 10 ya kuepuka yanayoweza kuvuruga uchaguzi

0

MUNGU ni mwema, nitumie nafasi hii kuwakumbusha Watanzania kwamba wakati huu ni kipindi muhimu kuombea taifa letu amani, hasa kipindi hiki cha uchaguzi.

Baada ya kusema hayo niseme wazi kuwa mataifa mengi na hasa ya Kiafrika yamekuwa yakiingia katika vurugu na machafuko makubwa unapofika uchaguzi.

Katika kipindi hicho, vyama vya upinzani vinaomba ridhaa ya wananchi kuchaguliwa kushika dola, huku vyama tawala vikiomba kuendelea kupewa ridhaa hiyo.

Katika kipindi hiki, migogoro mingine ya kikatiba huibuka kwenye mataifa mengi. Wakati tukitafakari hayo, Watanzania tutaingia katika uchaguzi mkuu mwaka huu katika mazingira tofauti kabisa na chaguzi zilizopita.

Nasema mazingira ni tofauti kutokana na kuwepo na uelewa mkubwa wa mambo ya kisiasa kwa Watanzania wengi hasa kutokana na harakati kubwa za kisiasa tangu kumalizika uchaguzi mkuu mwaka 2010.

Katika kampeni za uchaguzi wa mwaka huu, hoja nyingi zimeibuliwa na zitakuwa ni ajenda kwenye mikutano ya vyama vya siasa kwa kuwa baadhi majibu yake ni magumu sana.

Miongoni mwa hoja hizo kuu, ni suala la Katiba Mpya. Hapa vita imekuwa kati ya maoni yaliyokusanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Jaji Joseph Warioba na kilichoandikwa katika Katiba Inayopendekezwa.

Hoja nyingine tata ni hatua walizochukuliwa watuhumiwa wa ufisadi wa escrow na wezi wengine, suala la uandikishwaji wapigakura na hata sifa za wagombea wa urais, ubunge na udiwani.

Leo niyaseme mambo ambayo yakishindwa kupatiwa ufumbuzi, uchaguzi unaweza kuwa na vurugu, hivyo jitihada zifanyike ili tuepuke.

Mosi, vyama vya siasa na wananchi wazingatie maelekezo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi chini ya Jaji Damian Lubuva na raia wasiburuzwe na wanasiasa.

Pili, wanasiasa wengi wamezungumzia suala la jeshi la polisi chini ya mkuu wao nchini, IGP Ernest Mangu kutumia nguvu kubwa kupita kiasi kukabiliana hasa na vyama vya upinzani, lisifanyike.

Tatu, katika mkutano wa wanasiasa walikubaliana na jeshi la polisi kuwa lazima lithibiti matumizi mabaya ya makundi ya ulinzi ya vyama na chama tawala kisitumie vyombo vya serikali katika kampeni zake.

Nne, mengine yaliyotajwa kuweza kusababisha vurugu ni pamoja na kutotolewa kwa elimu ya kutosha ya wasimamizi wa uchaguzi, wapiga kura, viongozi wa kisiasa kufanya kampeni katika majumba ya ibada, hii ni mbaya isifanyike.

Tano, mambo mengine yanayoweza kuvuruga uchaguzi ni vituo vya kupigia kura kutoandaliwa vizuri, sita, kuchelewa kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi na saba, wanasiasa kutohubiri amani wakati wa uchaguzi huo. Muda uliobaki wanasiasa wahubiri amani katika kampeni zao. Bila amani hawawezi kupata kura.

Nane, vyombo vya habari pia vinaweza kuchochea vurugu kama visipofuata maadili ya kazi zao, vizingatie hilo na sina haja ya kufafanua kwa sababu wana wataalamu katika vyumba vyao vya habari.

Uchaguzi Mkuu 2015 unaweza kuwa wa amani na utulivu kama kila chombo kitatimiza wajibu wake.Tume ikiwa huru, polisi wakiwa huru, wanasiasa na viongozi wa dini tukihubiri amani, sidhani kama tutakuwa na matatizo.

Nisisitize kama Tume ya Uchaguzi ikiwa huru na haitaingiliwa, uchaguzi utakuwa salama na amani itadumu. Tisa, kila chama ni lazima kitendewe haki kwani  kama haki ikifuatwa katika kila hatua amani na utulivu itadumu.

Kumi, tukumbushane tu kwamba uchaguzi sio kazi ya Tume ya ya Taifa ya Uchaguzi pekee, ni ushirikiano wa wadau wote, tutekeleza wajibu wetu licha ya mapungufu ya kisheria yaliyopo.

Natoa wito kwa wadau wa uchaguzi kuhakikisha amani na utulivu vinashamiri wakati na baada ya uchaguzi mkuu. .

Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

Leave A Reply