The House of Favourite Newspapers

Mambo 3 ya Kumtengenezea Mwanao Njia ya Mafanikio!

0
Wapenzi

 

NAMSHUKURU Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema ambaye ameniwezesha kuwa na afya nzuri na nguvu za kutosha kiasi cha kunifanya niweze kutimiza majukumu yangu kwa ufanisi na kwa ujasiri mkubwa licha ya wakati mwingine kuwepo kwa vipingamizi vya hapa na pale.

 

Nikushukuru pia wewe msomaji wangu ambaye umekuwa ukifuatilia kila ninachoandika na nikuahidi tu kwamba nitakuwa naandika makala ambazo zitakuwa na nafasi nzuri ya kuyabadili maisha yako. Wiki hii mpenzi msomaji wangu nataka kuzungumza na wazazi hasa wale waliojaaliwa kupata watoto lakini pia wanaotarajia kuitwa wazazi.

 

Iko hivi; unapojaaliwa kuitwa mama au baba, hiyo ni heshima kubwa kwako na unatakiwa sana kumshukuru Mungu kwa kuwa, wapo ambao wanatamani kufikia hatua hiyo lakini mpaka leo hawajafanikiwa.

 

 

Lakini sasa, ukishaitwa mzazi unakuwa na jukumu zito la kuhakikisha huyo mwanao anakuwa katika mazingira mazuri na hatimaye naye kuja kuwa mama au baba bora katika jamii anayoishi.

 

Ndiyo maana wazazi wamekuwa wakishauriwa kuwa makini sana katika malezi ya watoto ili wasije wakawa wanaandaa majambazi, machangudoa na watu wengine wenye tabia za ajabu.

 

Ndiyo! Ukikosea kidogo tu mwanao anaweza kuwa mtu mbaya sana kwenye jamii, akakuchafua hadi ukajuta na kukufuru kwamba heri Mungu asingekupa mtoto huyo. Lakini majuto hayo yanaweza kutokana na wewe kushindwa kumlea vyema mwanao.

 

Rai yangu kwako wewe unayesoma makala haya ni kwamba, hakikisha unamlea mwanao katika msingi bora na kwa kukusaidia leo nimeona nikupe mambo matatu ambayo ukiyafanyia kazi kwa mtoto wako yanaweza kukuweka katika nafasi nzuri ya kumjengea ms ingi imara.

MPATIE ELIMU BORA

Tunajua kwamba elimu ni ufunguo wa maisha, hivyo basi hakikisha kwamba unafanya kadiri uwezavyo kumpatia elimu ya kutosha ili aweze kuja kuyaendesha maisha yake vizuri baadaye na asije kukulaumu kwa kuwa na maisha mabaya ambayo yametokana na kushindwa kwako kumpatia elimu inayofaa.

 

Usimpeleke mwanao shule ili mradi umempeleka, zingatia ubora wa shule bila kujali gharama. Elimu ni kitu muhimu sana kwa mwanao hivyo hakikisha hubahatishi katika hilo.

 

MAZINGIRA YA KUJIAMINI!

Kitu ambacho wazazi wengi wanakosea kwa watoto wao bila kujua kwamba kitakuja kuwaathiri hata watakapokuja kuwa wakubwa, ni kuwajengea mazingira ya kuwa wanyonge.

 

Suala la kujiamini ni la msingi sana kwa kila binadamu ili aweze kufanikiwa katika maisha yake na kujiamini hujengeka kuanzia utotoni. Mtoto anatakiwa apewe uhuru wa kueleza hisia zake na kumsikiliza pale ambapo anadhani anastahili kuzungumza mbele ya wazazi wake.

 

Kitendo cha kumtamkia mwanao neno NYAMAZA pale anapotaka kuzungumza jambo, kinamfanya ajisikie kwamba yeye si lolote wala si chochote, hali ambayo inaweza kumuathiri hata katika kufanya maamuzi juu ya maisha yake.

 

Kama utashindwa kumpa uhuru mwanao wa kuongea mbele yako unaweza kumjengea mazingira ya woga hata atakapokuwa mbele ya wenzake. Atakuwa akijiuliza; ‘Kama wazazi wangu wanashindwa kunisikiliza, watu wa pembeni wanaweza kunisikiliza kweli?’

 

Matokeo yake mtoto anaanza kujijengea mazingira ya kujiona mnyonge, asiye lolote mbele ya wengine, asiyeweza hata katika kile ambacho anaweza kukifanya, hali ambayo ni mbaya sana katika maisha ya mtu yeyote duniani.

 

Kwa maana hiyo, mjengee mwanao mazingira ya kujiamini ili aweze kuja kupambana vilivyo katika dunia hii ambayo bila kuwa na moyo wa kujiamini huwezi kufanya lol ote likaonekana.

 

TABIA NZURI!

Tabia nzuri ndiyo silaha ya maisha. Waswahili wanasema samaki mkunje angali mbichi, huku methali nyingine ikisema asiyefunzwa na mamaye hufunzwa na ulimwengu.

Methali zote hizo zinaonesha umuhimu wa kumfundisha mtoto tabia nzuri kuanzia udogoni.

 

Jaribu sana kumfundisha mwanao ajue lipi zuri, lipi baya. Hiyo itamuongoza katika kufanya mema na kuepukana na mabaya ambayo yanaweza kumfanya aishi maisha ya kumpendeza Mungu.

 

Mwandae mwanao ili aje kuwa kioo kwa wenzake watakaofuata kwa kuhakikisha kwamba unampa malezi sahihi kwa kuzingatia haki zake kama mtoto ili baadaye aje kuwa baba ama mama mzuri ambaye atatoa mchango mzuri kwa familia yake na jamii yake nzima kwa ujumla.

Ni imani yangu umepata mambo ya kuyafanyia kazi. Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine!

 

Amran Kaima| GAZETI LA AMANI| MAISHA |+255 658 798787

Leave A Reply