The House of Favourite Newspapers

Mambo 4 ya Kujifunza Kuachana Mondi na Tanasha

0

SIYO stori tena kwamba staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’ ameachana na baby mama wake mwingine, Tanasha Donna, raia wa Kenya kwani yameshasemwa mengi.

 

Mwanamama huyo amekata kabisa mawasiliano na familia ya Diamond au Mondi.

Kabla ya bundi kutua nyumbani kwa wawili hao, Mbezi-Beach jijini Dar, yapata wiki mbili zilizopita ambapo Tanasha alibeba mtoto wao, Naseeb JR na kusepa kwao jijini Mombasa, Kenya wakati Mondi akiwa Marekani. ‘Kapo’ yao ndiyo iliyokuwa ikiongoza kufuatiliwa zaidi barani Afrika.

 

Lakini katika kutengana kwa Mondi na Tanasha, kuna mambo kama manne hivi unayoweza kujifunza kwenye kuachana kwao;

KUTUMIA MUDA MREFU KWENYE UHUSIANO KABLA YA ‘KULALA’

Tanasha alithibitisha kuwa na ujauzito wa Mondi mwezi Julai, mwaka jana.

Tayari ujauzito huo ulikuwa wa miezi minne na wakati huohuo uhusiano wao ulikuwa si wa zaidi ya miezi sita. Watu wa hesabu wanaweza kueleza vizuri kwamba, walidumu kwenye uhusiano kwa miezi miwili tu kabla ya ‘kulala wote’ (kufanya mapenzi) na mimba kutungwa. Hapa tunaona kama Tanasha alifanya haraka mno au alikurupuka. Alipaswa kujipa muda zaidi wa kumjua Mondi kiundani.

 

USIACHE KILA KITU NA KUFUATA MATAKWA YA MAPENZI

Unapoanzisha uhusiano wa kimapenzi, usiharakishe kuacha kufanya mambo yako hasa ya kimaendeleo kabla hujaolewa na hata ukiolewa, endelea kutunza mambo yako.

Wakati Tanasha anaingia kwenye uhusiano na Mondi, alikuwa anafanya kazi yake ya utangazaji, lakini ghafla aliacha kufanya kazi hiyo kwenye kituo cha redio cha NRG cha Mombasa nchini Kenya, kazi ambayo aliifanya kwa muda mrefu na kumuingizia kipato, badala yake akakimbilia kwenda kuishi na jamaa huyo.

 

Huko alikojiingiza kwenye muziki, siyo mkubwa au hakuwa anafanya vizuri kama Mondi anayekimbiza na Wimbo wa Jeje, hivyo angeendelea kufanya kazi yake ya utangazaji wakati akisubiri muziki wake ukue au uwe mkubwa zaidi. Wapo wanaodai aliamini angemtumia Mondi kupanda haraka kimuziki, jambo ambalo sasa litakuwa gumu kwa sababu hayupo tena na Mondi ambaye alikuwa anamfanya ‘ku-trendi’. Haikuwa kazi rahisi kama Tanasha alivyofikiri!

 

USIAMINI KAMA UNAWEZA KUMBADILI MWANAUME

“Diamond anajulikana kwa tabia yake ya kucheza na mioyo ya wanawake!” Haya ni maneno ya baby mama wake mwingine, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ alipokuwa akifunguka sababu ya yeye kuachana na jamaa huyo.

 

Pamoja na sifa hizo, wanawake huwa wana tabia ya kuamini kuwa wanaweza kuwabadilisha wanaume na hicho ndicho kilichomtokea Tanasha. Baada ya kuona ishara au dalili za kusalitiwa ambazo zilikuwa zikizagaa mitandaoni, bado hakushtuka kwani aliamini atambadilisha. Kilichofuata, sasa Tanasha amekuwa kama mhamasishaji au mwanaharakati wa haki za wanawake za kimapenzi kwenye mitandao ya kijamii! Watu wanasema; “Kama Zari alishindwa, Tanasha ni nani?”

 

UKIKATALIWA KUBALI

Kukataliwa kunaleta ladha mbaya hata kutamkika mdomoni, ukiachilia mbali maumivu ya moyo. Kwa kinywa chake, Tanasha alisema, kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Mondi ni changamoto kubwa mno. Ukiachilia mbali maneno ya mashabiki kwenye mitandao ya kijamii ambao walikuwa na timu zao za wapenzi waliotangulia wa Mondi, pia familia ya jamaa huyo ilisemekana haimkubali.

 

Dalili zote hizo Tanasha aliziona, lakini akaziba masikio. Akazipuuza ilhali alikuwa na nafasi ya kusepa mapema.

Lakini hata hivyo, kuwa ‘single mother’ hakumuondolei ubinadamu wake. Unaweza ukakataliwa, ukaachwa, ukatengwa na mengine mengi, lakini ubinadamu wako utabaki palepale.

 

Tanasha anayekimbiza na Wimbo wa Gere alioshirikiana na Mondi, kabla ‘maji hayajakorogeka’ anaweza kuogopa kuitwa ‘single mother’ endapo itashindikana kurudiana na Mondi kwani mara nyingi siyo rahisi kufanya hivyo, lakini atapaswa kukubaliana na ukweli ulio mbele yake!

Makala: Neema Adrian, Dar

Leave A Reply