The House of Favourite Newspapers

MAMBO 5 YA JOKATE; FUNDISHO KWA MASTAA BONGO!

MJASIRIAMALI mashuhuri nchini Marekani, Warren Buffett amewahi kusema; tofauti kati ya watu wenye mafanikio na watu wenye mafanikio zaidi ni wale wenye mafanikio zaidi kusema ‘hapana’ katika kila jambo ambalo watu wengine wanadhani hawaliwezi.

 

Kauli hii inajidhihirisha kwa mrembo aliyetokea kwenye kinyang’anyiro cha Miss Tanzania 2006, Jokate Mwegelo ambaye sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Pwani kwani amekataa kubaki na ‘taito’ ya ‘umisi’ pekee, sasa hivi anatoa amri kwa polisi, anapigiwa saluti na wanajeshi, anawaamrisha watendaji wote waliopo chini yake kiuongozi.

 

 

Mkurugenzi, Katibu Tawala (DAS), Kamanda wa Wilaya (OCD), Afisa Elimu, Maganga Mkuu, wote hawa wanachukua maelekezo kutoka kwake na wanapaswa kuyatekeleza maana yeye ndio bosi wa wilaya, mwakilishi wa rais.

Jokate alikataa ile nafsi iliyokuwa inamuambia hawezi, yeye alisema hapana. Alisema anaweza na ndio maana kweli alifanikiwa kuingia kwenye maisha ya ndoto yake.

 

Ingekuwa mwingine kama ambavyo tunawaona mastaa wengi tu hususan wa kike Bongo, maisha yao ni ustaa tu. Hakuna wanachowaza zaidi ya mitoko na kufanya starehe, Jokate alikuwa na ndoto ya kuwa kiongozi, akaiishi ndoto hiyo na hatimaye kweli amekuwa.

Yafuatayo ni mambo matano ambayo yalimbeba Jokate ambayo nina amini, yanaweza kuwa fundisho kwa mastaa wengine kama kweli wanataka kubadalika na kuwa kwenye levo za kuheshimika zaidi.

 

 

ALIJIWEKEA NDOTO

Cha kwanza kabisa, Jokate alikuwa na ndoto ya kuwa mwanasiasa au kiongozi wa umma. Alianza kwa kusoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, akasomea masomo ya Sayansi ya Siasa na Falsafa (Political Science and Philosophy).

Hiyo ikawa hatua ya kwanza, hatua ya pili baada ya kuhitimu degrii yake, akaanza kusaka njia ya kutokea ambapo alijipenyeza na kufikia kwenye Chama cha Mapinduzi (CCM) kupitia Umoja wa Vijana (UV-CCM).

 

 

UVUMILIVU

Akiwa UV-CCM Jokate alikula msoto katika kutafuta namba kabla ya kuinasa nafasi ya Katibu wa Uhamasishaji lakini nafasi hiyo alidumu nayo kwa kipindi fulani kisha akatolewa.

Kuonesha kwamba ni mvumilivu, hakukata tamaa. Licha ya kutolewa kwenye nafasi hiyo, pengine angekuwa mwingine, angeweza kukata tamaa.

Jokate hakukata tamaa, aliendelea kuwa mvumilivu na kukitumikia chama hadi ilipofika Julai mwaka jana, alipoteuliwa na Rais Dk John Pombe Magufuli kuwa mkuu wa wilaya.

 

 

BIDII

Jokate ana bidii katika kufanikisha jambo lake. Ameonesha hilo akiwa shuleni, akaonesha pia alipokuwa CCM na sasa anadhihirisha hilo akiwa kwenye kazi yake kama mkuu wa wilaya.

Anaonekana, akiwa kwenye majukumu yake kwa kuhakikisha anashiriki katika shughuli mbalimbali za wilaya hiyo ikiwemo kulinda misitu.

 

BUSARA/HEKIMA

Kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram, Jokate amedhi

hirisha hilo kwa kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii, akinyenyekea na kuwasaidia watu mbalimbali wenye matatizo.

 

MCHA MUNGU

Kingine kinachombeba Jokate ambacho mastaa wengine wanapaswa kujifunza ni kumtumaini Mungu. Kumtumaini Mungu kuna faida. Jokate amekuwa mstari wa mbele katika hilo tangu alipokuwa anaishi na wazazi wake, Oysterbay jijini Dar.

Alikuwa akiimba kwaya katika Kanisa la Mtakatifu Peter, lakini hadi sasa bado amekuwa mshiriki mzuri wa ibada kanisani. Kumtumaini Mungu katika kila jambo ni silaha kubwa ya mwanadamu.

 

FUNDISHO

Hili ni fundisho pia kwa mastaa wengine, wanapaswa kujifunza kufikiri nje ya boksi. Maisha hayaishii kwenye kujirusha na kubadili mabwana kila uchwao. Ukiwa na nia ya kubadilika, kweli unaweza kuwa yule ambaye unatamani kuwa.

Makala: Imelda Mtema.

 

BREAKING | JPM, Kenyatta, Museveni, Kagame Uso kwa Uso Arusha

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Comments are closed.