Mambo 5 ya kuzingatia unapowaza kumfungulia mkeo biashara!
Ni wiki nyingine tunakutana kupitia safu hii nikiamini umzima bukheri wa afya na unaendelea vyema na mishemishe za maisha. Mimi niko poa, namshukuru Mungu!
Mpenzi msomaji wangu, kuna katabia f’lani huko mtaani kameshamiri ka’ baadhi ya wanaume kutotaka wake zao kufanya kazi za kuajiriwa lakini pia hawataki kuwa na wanawake magolikipa tu.
Wanachokifanya ili kuwafanya wake zao wawe bize ni kuwapa mitaji ya kuanzisha biashara ambazo mwisho wa siku zinaweza kuwafanya wawe na kipato kitakachowasaidia wao wenyewe pamoja na familia kwa ujumla.
Changamoto ambayo wanaume wengi wamekuwa wakikumbana nayo ni pale linapokuja suala la kumfungulia mke biashara. Ndiyo maana wiki hii nimeona nizungumzie mambo ya kuzingatia pale unapojiwa na wazo hilo.
Ana uzoefu?
Wapo wanawake ambao kwa kuwa wanawaona wenzao wanafanya biashara na wanafanikiwa na wao wanakuwa na kimuhemuhe cha kuwa wafanyabiashara. Unaweza kukuta mahesabu hawajui, mbinu za biashara hawajui lakini wanalazimisha kufanya biashara. Watu kama hao ukiwafungulia biashara utakuwa unafanya kazi bure.
Lakini pia mwanaume unatakiwa kumfungulia biashara mkeo ukijua kabisa ataimudu kwa kujua kuwa huenda huko nyuma alishawahi kuifanya. Hii kulazimisha kumfungulia duka au kumpa mtaji wa kuuza vitumbua wakati hajui aanzie wapi, faida haiwezi kuonekana na itakuwa ni kama kutwanga maji kwenye kinu.
Kwa maana hiyo mke aanzishe au akubali kuanzishiwa biashara pale ambapo ataona anaimudu. Kinyume chake ni bora akafanya kazi nyingine kama kulima au akae tu nyumbani.
Yeye anataka ipi?
Mume kama mume anaweza kuwa na ‘aidia’ ya biashara f’lani ambayo anaamini akimfungulia mkewe wanaweza kujiongezea kipato lakini ni vyema mke akashirikishwa kwa kuulizwa ni biashara gani anahisi akifunguliwa ataiendesha kwa ustadi.
Nasema hivyo kwa kuwa unaweza kuwa na ‘aidia’ ya kumfungulia duka au saluni lakini kumbe yeye hana uwezo wa kuendesha biashara hizo, badala yake yeye anamudu kuuza genge au chapati. Sasa ni vyema ukamuuliza na mkakubaliana kuliko kulazimisha mkeo afanye biashara ambayo haiwezi.
Utakuwa na amani?
Ukifuatilia sana wapo wanaume ambao hawataki wake zao wafanye biashara f’lani wakihisi huenda watasalitiwa. Kwa mfano ni wanaume wachache sana ambao wanaweza kuwakubalia wake zao wafanye biashara za kusafiri mikoani.
Pia ni wanaume wachache wanaoweza kuwafungulia wake zao biashara ya baa, kwa nini? Kwa sababu wanahisi hawatakuwa na amani mioyoni mwao.
Ndiyo maana nikasema biashara ambayo utamfungulia mkeo isije ikaleta migogoro na kuwafanya mkawa ni watu wa kutibuana kila wakati. Itakuwa ni jambo la ajabu kama utakubali mkeo afanye biashara ya kuuza kwa mkopo nguo za kike halafu ukawa hutaki awe ni mtu wa kuzurura kwenye nyumba za watu. Au unamruhusu afanye biashara ya baa halafu unataka awahi kurudi nyumbani, hapo hiyo biashara itafanyikaje?
Atamudu biashara na familia?
Mke ni mtu muhimu sana katika malezi ya familia hivyo unapomuanzishia biashara ujiulize ataimudu pamoja na kulea familia vizuri? Isije ikawa unamuanzishia biashara halafu ukitaka mtafute mtoto anakuambia msubiri kwanza, au kwa kuwa anafanya biashara basi haijali familia, yeye muda wote anakimbizana na pesa, hiyo haitakuwa sawa!
Kwa nini biashara?
Siyo kila mtu anaweza kufanya biashara, wengine ukiwafungulia biashara utakuwa unacheza kamari. Kwa maana hiyo ifike mahali ujiulize ni kwa nini umfungulie biashara mkeo? Jibu la swali hilo litakupa muongozo.
Ni hayo tu kwa leo, naamini ukipata majibu ya mswali hayo hapo juu, utakuwa kwenye nafasi nzuri ya kufanya uamuzi sahihi.