The House of Favourite Newspapers

Mambo 7 Aliyoyazungumza Rais Samia Misri

0

RAIS Samia Suluhu Hassan ameanza ziara ya siku tatu nchini Misri ambapo katika siku ya kwanza amekutana na kufanya mazungumzio na mwenyeji wake, Rais Abdel Fattah Al Sisi kati maeneo ya diplomasia, elimu, uchumi, michezo, huduma za kijamii, utalii na mambo mengine.

Akizungumza baada ya majadiliano hayo, Rais Samia amegusia mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na:

 

1. Uhusiano wa Tanzania na Misri
Amesema nchi hizo zitaendelea uhusiano ambao uliasisiwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa zamani wa Misri, Hayati Gamal Abdel Nasser.

 

2. Ulinzi na Usalama
Tanzania imeendelea kuwa salama hivyo kutoa nafasi kwa serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo na kijamii. Hata hivyo amesema kutokana na mafanikio makubwa ya kijeshi ya Misri, ameeleza kwamba Tanzania ipo tayari kushirikiana nayo katika mambo mbalimbali ikiwemo kukabiliana na ugaidi.

 

3. Uchumi
Kama nchi nyingine dunia, uchumi wa Tanzania uliathiriwa sana na maambukizi ya Virusi vya Korona, mathalani sekta ya utalii. Amesisitiza kwamba serikali imeendelea kuchukua hatua madhubuti kufufua sekta nyeti na kwamba Pato la Taifa linatarajawa kukua kwa asilimia 4.6 mwaka huu na ujao.

 

4. Elimu
Ameeleza kwamba kwa miaka kadhaa Tanzania imekuwa ikipokea fursa za kimasomo na kujengeana uwezo kutoka serikali ya Misri, na kwamba hilo limeboresha sekta ya elimu na kukuza ujuzi, ufundi na utaalamu. Ameongeza kwamba Tanzania inathamini mchango huo.

 

Aidha, amepongeza uamuzi wa Misri kufundisha lugha ya Kiswahili (lugha ya kimkakati) katika taasisi za elimu ya juu nchini humo, akitanabaisha kwamba lugha hiyo imewaunganisha Waafrika wengi, na kwamba Tanzania itatuma wataalamu kuona namna inavyoweza kushirikiana na Misri.

 

5. Nishati
Rais Samia amesema nchi hizo mbili zinashirikiana katika sekta ya nishati ambapo kampuni mbili za Misri zinajenga bwawa la kufua umeme wa maji wa Julius Nyerere katika Mto Rufiji ambao ukimamilika utazalisha megawati 2115.

 

6. Kilimo, mifugo na uvuvi
Nchi hizo zimekubaliana kushirikiana katika sekta ya kilimo, ambapo Tanzania itanufaika sana katika teknolojia kubwa ya Misri kwenye sekta hizo.

 

7. Masuala ya Kikanda na Kimataifa
Tanzania na Misri zimekubaliana kushirikiana katika masuala yenye maslahi sawa kwa wote, ikiwa ni pamoja na ulinzi na usalama duniani, mabadiliko ya tabianchi, maendeleo ya miundombinu, ufadhili wa maendeleo, utetezi wa haki za binadamu, kukabiliana na ugaidi, ushirikiano wa Afrika, maendeleo endelevu na kusaidiana katika majukwaa ya Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa.

 

Katika ziara ya leo, Rais Samia ameshuhudia utiwaji saini wa hati tatu za makubaliano, na kuahidi kwamba Tanzania itatekeleza makubaliano hayo, na itazungumza na washirika wa Misri kumalizia makubaliano yaliyobaki.

Leave A Reply