The House of Favourite Newspapers

Mambo 9 yaliyosababisha ustaa wa Tiffah!

0

TIFFAH DIAMONDHamida Hassan

Ilikuwa Agosti 6, 2015 pale msanii wa muziki Bongo, Nasibu Abdul ‘Diamond’ na mpenzi wake Zarinah Hassan ‘Zari’ walipojaaliwa kupata mtoto ambaye hatimaye alipewa jina la Latifa lakini wengi wakapenda kumuita Tiffah ambalo ndilo limekuwa maarufu.

ZARI (3)Mtoto huyu juzi Septemba 15, 2015 alitimiza siku 40 tangu kuzaliwa kwake lakini ndani ya kipindi hicho kifupi, amekuwa ni staa kama walivyo wazazi wake. Leo hii ukitaja jina la Tiffah, hata watoto wanajua kuwa ni mtoto wa Diamond tofauti na ukitaja jina la Cookie (wa Aunt Ezekiel).

Katika makala haya nataka nikupe mambo ambayo yalinogesha ustaa wa mtoto huyo ndani ya siku arobaini na kumfanya aweke historia.

 MTOTO WA ZARIKabla hajazaliwa

Ikumbukwe kuwa, siku nyingi sana Diamond amekuwa akitamani mtoto. Amewahi ku-date na wasichana kibao lakini hakuna aliyefanikiwa kumpatia furaha hiyo.

Alipomnasa Zari na kuamua kumzalia, ukawa ni ukurasa mpya kwa mwanamuziki huyo. Zikapita siku chache tu tukasikia tayari Diamond amefanya mambo. Hapo ndipo ustaa wa Tiffah ulipoanzia kwani vurugu za kuitangaza mimba hiyo hazikuwa za kitoto.

Diamond aliizungumzia kila mara mimba hiyo na akawa amefanya jitihada za kujua kuwa ni mtoto wa jinsia gani, alipojua kuwa ni binti, furaha ikaongezeka.

Utata ukaibuka

Katika jambo zuri kama hilo hasa kwa staa kama Diamond, wapo ambao hawakufurahishwa nalo. Wakaibuka watu na kuzusha kuwa, eti mimba hiyo haikuwa ya Diamond.

Yakaandikwa mambo mengi na kuwafanya wazazi, ndugu na marafiki wa msanii huyo kubaki njia panda. Wakati hayo yakitokea, Zari na Diamond waliziba masikio.

Mapenzi shatashata yakaendelea na zaidi ya yote Diamond alimtumia mpenzi wake huyo  kujiingizia mkwanja kwenye shoo. Yaani ikawa ukitaka kwenye shoo ya Diamond aje na Zari, mkwanja unaongezeka.

Wafadhili

Hata kabla mtoto huyo hajazaliwa, wapo watu waliojitokeza kumfadhili. Kuna duka la nguo na vitu vya watoto la Msasani City Mall jijini Dar ambalo lilimpa Diamond ofa ya kwenda kufanya shopping kwa ajili ya mtoto wao.

Shopping za nguvu

 Licha ya ofa hizo, Diamond kwa nyakati tofauti alimfanyia Tiffah shopping ya mamilioni ambayo haijawahi kufanywa na staa yeyote. Ikielezwa kuwa, shopping ya awali kabisa iliyofanyika Uingereza na Dubai ziliteketezwa takriban shilingi milioni 23.

Sura adimu

Imekuwa ni jambo la kawaida kwa mastaa wengi kuficha sura ya mtoto pale anapozaliwa na kuja kumuanika siku anapotimiza siku arobaini. Wengi wamefanikiwa katika hilo wakiwemo Diamond na Zari.

Tofauti ya mastaa hawa na wengine ni kwamba, kuna wakati kama uzalendo ulikuwa unawashinda kwani ilifika kipindi walimuanika na kubakiza macho, kichwa na masikio lakini eneo la chini likawa wazi.

Afunguliwa ‘peji’ Instargram

Siku ambayo mtoto huyo alizaliwa alifunguliwa ukurasa wake wa Instagram na kwa siku moja tu akawa na followers ‘wafuasi’ kibao. Jambo hilo lilimfanya awe gumzo kwani aliwafunika hata baadhi ya mastaa.

Baba feki wakaibuka

Baada ya Tiffah kuzaliwa, akajitokeza jamaa kutoka Uganda, King Laurence na kudai kuwa mtoto huyo ni wake. Mbali na huyo, yakaibuka tena madai kuwa, eti mtoto huyo ni wa mume wa zamani wa Zari, Ivan Semwanga. Hilo nalo likaibua sintofahamu lakini mwishowe likayeyuka.

Azawadiwa gari

Katika kuonesha kuwa mtoto huyo ana thamani, wakaja ndugu wa Zari kutoka Sauzi ambao walimzawadia gari aina ya Mercedes Benz MSL Benz lenye thamani ya dola 100,000 (zaidi Sh. milioni 200) eti kwa ajili ya kuendea kliniki.

Sura yake ‘yauzwa’

Taarifa zilizokuwepo awali zinadai kuwa, sura ya mtoto huyo ilitakiwa kuonekana siku ya 40 yake na kuna kampuni ambayo imetoa milioni 40 ili kuitumia sura hiyo kwenye masuala ya kibiashara. Ambapo inadaiwa kuwa baada ya sherehe yake ya kuonesha sura yake litatengenezwa bonge la bango ambalo litakuwa na sura yake ambalo moja kwa moja litakuwa likitangaza bidhaa za kampuni husika.

Leave A Reply