The House of Favourite Newspapers

Mambo ni Moto Yanga… Kaze na Injinia Hersi Wamshusha Bigirimana kwa Mil 400

0
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Injinia Hersi Said (katikati) akiwa na Kocha Msaidizi, Cedric Kaze.

WAKATI Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Injinia Hersi Said na Kocha Msaidizi, Cedric Kaze wakienda Rwanda kukamilisha usajili wa Obed Bigirimana, inaelezwa ili kumpata kiungo huyo, watalazimika kutoa shilingi milioni 400.

 

Juzi Ijumaa, Kaze na Injinia Hersi walikuwa uwanjani kumshuhudia kiungo huyo wa Kiyovu akicheza mechi ya Ligi Kuu ya Rwanda dhidi ya Gosigo iliyomalizika kwa Kiyovu kufungwa 2-0.

 

Yanga ambayo imeanza harakati za usajili mapema kujiandaa na msimu ujao ambapo wana asilimia kubwa za kushiriki michuano ya kimataifa, pia wanatajwa kuiwania saini ya kiungo mwingine wa timu hiyo, Nshimiyimana Ismael ‘Pitchou’.

Obed Bigirimana.

Taarifa za uhakika kutoka Rwanda, zinasema kuwa, Injinia Hersi akiwa na Kaze, juzi baada ya mchezo huo kumalizika, usiku walikutana na Bigirimana na kufanya kikao kizito kwa ajili ya kumshawishi atue Yanga.

 

Mtoa taarifa huyo alisema kwamba, endapo Yanga wanataka kuwasajili viungo wote hao ambao ni raia wa Rwanda, basi watalazimika kununua mikataba yao ya mwaka mmoja ikiwa na thamani ya shilingi milioni 400.

 

“Sina uhakika sana kwamba watakuwa wanamtaka na Pitchou, nafahamu kwamba tageti yao kubwa ipo kwa Bigirimana ambaye tayari wamefanya naye mazungumzo jana (juzi) usiku baada ya mechi.

 

“Hawakumaliza mazungumzo hayo, wakaomba kuongea naye tena Jumamosi (jana) kwa sababu baada ya mechi alikuwa amechoka ukizingatia kwamba matokeo hayakuwa mazuri kwa timu yake.

 

“Mabosi wa Kiyovu wapo tayari kuwaachia wachezaji wote hao ikiwa watafikia makubaliano kwa sababu wana mikataba ya mwaka mmoja, hivyo Yanga watalazimika kuinunua kwa shilingi milioni 400,” alisema mtoa taarifa huyo.

STORI NA IBRAHIM MUSSA NA MUSA MATEJA

Leave A Reply