NI saa 12 asubuhi, Jumamosi Februari 17, sipeleki watoto wangu shuleni, hivyo bado nipo kitandani, mkononi mwangu nimeshika simu yangu, ninaitumia kama kompyuta kusoma taarifa mbalimbali za hapa nyumbani na duniani.
Moyo wangu unauma sana pale ninaposoma habari za binti Akwilina Akwilini, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Usafirishaji (NIT) cha jijini Dar es Salaam ambaye amepoteza maisha yake kwa kupigwa risasi na polisi waliokuwa wakiwatawanya waandamanaji wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambao walikuwa wakiandamana kuelekea ofisini kwa Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Kinondoni kudai viapo vya mawakala wao vya kusimamia upigaji kura.
Sikutarajia kabisa uchaguzi huu wa marudio ya ubunge wa Jimbo la Kinondoni ungeondoka na maisha ya mtu, binti huyu aliyekuwa na ndoto zake maishani, amezimika ghafla, kibaya zaidi, kama ilivyoandikwa binti huyo wala hakuwa kwenye maandamano, yeye alikuwa ndani ya daladala akielekea Bagamoyo akitokea katikati ya jiji.
Nikisema sikuumia nitakuwa mwongo, kama mzazi, machozi yalinitoka, nilipovaa viatu vya wazazi wa mtoto huyo, kwamba walimsomesha tangu chekechea hadi chuo kikuu, bila shaka kama mzazi yeyote wa Kiafrika, walikuwa na matarajio makubwa kwa mtoto wao, kwamba ipo siku angekuja kuwapunguzia shida na mahangaiko waliyo nayo.
Lakini sasa amekufa, tena ghafla, afadhali wangemuuguza, halafu kafa kifo cha kupigwa risasi na polisi! Unakujaje nyumbani kwangu kuniletea taarifa kwamba mwanangu amepigwa risasi na polisi na kufa? Nina uhakika kama wazazi wa binti huyu hawatapewa nasaha za kutosha, maisha yao yote, wao na familia zao watalichukia jeshi la polisi kwani limewaondolea mtu waliyempenda kupindukia.
Tukio hili linanifanya niifikirie Tanzania yangu kwa mara nyingine tena, ilikotoka, ilipo na inakoelekea! Mungu atusaidie, dalili hii hakika si nzuri, uchaguzi wa jimbo moja umeondoka na maisha ya mtu? Je, hali hii ikiachwa iendelee itakuwaje huko tunakoelekea 2020? Moyoni mwangu ninaogopa, wasiwasi mkubwa unaniingia, lazima tujifunze jambo kutokana na uchaguzi wa marudio katika Majimbo ya Kinondoni na Siha, tupende, tusipende lipo jambo la kujifunza.
Kwangu mimi nimetoka na somo moja kubwa, kwamba, kama nchi hii kesho itaingia kwenye machafuko na damu za watu kumwangika itakuwa ni kwa sababu ya watu wafuatao, hawa wanawajibu mkubwa wa kuinusuru nchi yetu na hatma mbaya iliyoko huko tunakoelekea:
WANASIASA:
Hili ni kundi la watu lenye ushawishi mkubwa sana katika nchi yoyote, wanaweza kuipeleka nchi kulia au kushoto wapendavyo wenyewe. Wamegawanyika katika makundi mawili; wanasiasa wa chama tawala ambao huunda serikali na kuongoza nchi na wapo wa upinzani, kundi jingine dogo ambalo sitaliongelea sana ni la wanasiasa wa katikati, hawa ni wakosoaji wa pande zote mbili nilizozitaja hapo juu.
Lengo la mwanasiasa yeyote huwa ni kukamata dola, awe wa upinzani au wa chama tawala, hicho ndicho kitu kikubwa huwa kinatafutwa kwa udi na uvumba, kwa mvua au jua, katika kutafuta dola mwanasiasa huwa yuko tayari kupoteza chochote ilimradi aingie ikulu, kushika dola na hatimaye kuunda serikali.
Sote tumeshasikia habari za wanasiasa ambao huingia msituni na kuwa waasi, wakapigana na wanasiasa walioko madarakani na kuua maelfu ya watu ili mwisho wa siku tu, waingie ikulu na kushika madaraka, hii inadhihirisha kabisa kamba mwanasiasa anachokitaka ni dola, hata kama atapoteza maelfu ya maisha ya watu.
Wanasiasa siku zote wana “moja kichwani” wataongea hili mbele za watu ili wapate kibali cha kukamata dola, wako tayari kudanganya ili kuwaaminisha watu kwamba wao wanafaa, wakishaingia madarakani, waliobaki nje nao kazi yao ni moja tu; kuhakikisha walioko madarakani wanaokana hawafai na hivyo kuchukiwa.
Wanasiasa wapo tayari kupandikiza chuki kuwagawa watu waliokuwa wakiishi pamoja kwa misingi ya dini, kabila na hata siasa ilimradi tu wajipatie kuungwa mkono mwisho wa siku waingie madarakani, hicho ndicho kitu ambacho wanasiasa wanakitaka usiku na mchana, hata kama kitagharimu maisha ya watu ambao mara nyingi huwa si watoto au wake zao.
Ombi langu kwa wanasiasa wote wa upinzani na chama tawala ni kuwa tayari kutofautiana kwa hoja, kupeana nafasi ya kufanya siasa na kukubali matokeo wanaposhindwa uchaguzi na mwisho kuunganisha nguvu, watu na kuendelea kujenga nchi yao.
Kupandikiza chuki na kujeruhi mioyo ya wengine, inaweza kuliingiza taifa katika machafuko na kuharibu kabisa historia, jambo ambalo binafsi sitaki kabisa kulishuhudia na nisingependa kukabidhi nchi hii kwa watoto na wajukuu tofauti na nilivyoipokea kutoka kwa wazazi wangu, ikiwa yenye amani na utulivu, kila Mtanzania akiwa na haki ya kufanya apendacho bila hofu.
VYOMBO VYA HABARI:
Nimefanya kazi kwenye vyombo vya habari kwa miaka karibu ishirini, nimejifunza kwamba vyombo vya habari visipojitambua na kuweka maslahi ya taifa mbele, vinaweza kuiingiza nchi kwenye machafuko makubwa, historia ikabadilika, taswira ya nchi ikaharibika na maelfu ya watu wakapoteza maisha.
Siku zote yapasa vyombo vya habari kuwa huru, maana hiyo ni sauti ya umma, havipaswi hata kidogo kubanwa! Lakini kama vyombo vya habari vitashindwa kuutumia vizuri uhuru huu, vikaweka maslahi binafsi mbele, lazima vitaanza kuegemea upande mmoja na kugandamiza upande mwingine, jambo ambalo ni hatari kubwa.
Wote tunafahamu yaliyotokea Rwanda wakati wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, vyombo vya habari ndiyo vilichochea sana mauaji hayo, pale vilipohamasisha kundi fulani la watu kuchinja wengine! Hata kama vyombo vya habari vitakuwa huru kiasi gani, uhuru wake hautakiwi kuvuka mpaka na kufikia hatua ya kuhatarisha usalama wa taifa.
Vyombo vya habari vinatakiwa kusimama kwenye nafasi yake, bila hofu, woga wala upendeleo wa aina yoyote, visikubali kutumiwa na wanasiasa au vikundi fulani vya watu na kuchochea chuki miongoni mwa Watanzania, bali visimame katikati na kuhamasisha amani, vikisimamia maslahi ya taifa, hili likifanyika, hakika mwisho wa taifa hili utakuwa mzuri.
VYOMBO VYA USALAMA:
Ni kweli kabisa vyombo vya usalama vinatakiwa kutii amri ya mtawala na ndiyo maana halisi ya kuwa mkuu wa nchi, vyombo vyote vya usalama huapa kutii amri za mkuu wa nchi.
Lakini vyombo hivi wakati mwingine hutekeleza majukumu yake mpaka unafika mahali unashindwa kuelewa kama matendo yanayofanywa na vyombo hivyo kama ni maelekezo ya mkuu wa nchi au ni ya mtu fulani mahali fulani anayetaka kuchafua jina la mkuu wa nchi.
Vyombo hivi ili nchi iendelee kuwa na amani vinapaswa kuwa na hekima na busara ya hali ya juu sana katika utendaji wa kazi zake, maana mkuu wa nchi huwa hayuko na vikosi vyake wakati wote. Hili lisipofanyika, vyombo hivi vinaweza kujikuta vinaingiza chuki katika mioyo ya wananchi dhidi ya serikali na mtawala wake na kupoteza amani na utulivu katika taifa.
Kwa nini risasi za moto mahali ambapo hazihitajiki? Kwa nini wanajeshi waingie mitaani kupiga wananchi kwa sababu tu mmoja wao kaibiwa simu? Hivi haya kweli ni maagizo ya mkuu wa nchi? La hasha, siamini, matendo haya yakiachwa yaendelee, mwisho wa siku yanaweza kutikisa usalama wa taifa letu na kutupeleka tusikotakiwa kwenda.
VIONGOZI WA DINI:
Pamoja na kuongozwa na mtawala wa nchi na sheria zilizopo, asilimia kubwa ya watu katika nchi yoyote wanazo dini zao, hivyo wanao viongozi wao wa dini wanaowaheshimu na kusikiliza maelekezo yao. Waislam wanao mashehe na maimamu. Wakristo wanao maaskofu, mapadri, wachungaji na kadhalika na dini zingine na viongozi wao.
Viongozi hao wa dini wana ushawishi mkubwa sana kwa waumini wao, yawapasa kuwa watu wenye hekimu na busara katika utendaji wa kazi zao, maana kila wanachokisema mwisho wa siku huchukuliwa kwa uzito mkubwa sana na waumini wao.
Wajiepushe na matamko ya kugawa na kupandikiza chuki miongoni mwa watu wao, siku zote wasimame katika nafasi zao na kukemea maovu bila kujali yametendwa na nani, hiyo ndiyo kazi yao! Wajiepushe na kuwa sehemu ya serikali au watawala kwa maslahi yao binafsi, huo utakuwa ni usaliti mkubwa sana kwa watu ambao Mungu amewakabidhi kwao ili wawaongoze.
WANANCHI:
Hawa ndiyo wamiliki wa nchi, wenye mali, waajiri wa wanasiasa wanapokuwa madarakani! Hawa ndiyo hufanya uamuzi juu ya nini kifanyike katika taifa lao na nani awaongoze kwa kupiga kura.
Walio wengi hawalifahamu jambo hili, siku zote wakishamweka mtu madarakani hubaki kutupa lawama bila kuchukua hatua yoyote, wakidanganywa kwa vitu au ahadi za uongo na kujikuta wamefanya uamuzi usio sahihi.
Wengi wamekuwa wakisikillza na kufanyia kazi kila wanachoambiwa na wanasiasa wakati mwingine bila kutumia akili zao za ziada na kufanya mambo ya kuhatarisha usalama wa nchi, wanafanywa ngazi za wanasiasa kufikia malengo yao kisiasa ambao wakati mwingine wakiingia madarakani huwasahau.
Ambacho nimejifunza katika uchaguzi huu wa wa marudio Kinondoni na Siha ni kwamba Watanzania wanatakiwa kujitambua, waielewe nafasi yao na wawe na uwezo wa kufanya uamuzi sahihi wakati unapofika, kamwe wasikubali kutumiwa na wanasiasa kwa faida zao binafsi, wafanye uamuzi ambao utakuwa na faida kwa vizazi zilivyopo na vijavyo.
Mambo haya matano ndiyo niliyojifunza katika uchaguzi wa Kinondoni na Siha, Mungu ibariki Tanzania na pia uwabariki Watanzania wote.
Ahsanteni kwa kunisoma.
ERIC SHIGONGO – Kumbukumbu za Kweli za Maisha Yangu-233
Comments are closed.