MAMBO YA KUFANYA UNAPOGUNDUA MNAELEKEA MWISHO WA PENZI

HAKUNA kitu kinachoumiza moyo kama unapogundua kwamba uhusiano uliopo ndani yake, unaelekea ukingoni. Mmeishi pamoja kwa muda mrefu, mmeoneshana mapenzi mazito, mmeshirikiana kwenye mambo mengi, umeshamzoea na yeye amekuzoea, lakini ghafla unagundua kwamba huwezi tena kuendelea kuwa naye.  Ni hisia zinazochoma sana moyo, hasa kama ulijitoa maisha yako yote kwa ajili ya mtu fulani. Nimeshakueleza kuhusu mbinu mbalimbali unazoweza kuzitumia kuokoa penzi linaloelekea kufa, lakini wasomaji wangu wengi niliozungumza nao, wamenieleza kwamba walishafanya kila kitu kuokoa penzi lisifike mwisho, lakini imeshindikana.

Je, unapofikia katika hatua hiyo, umejitahidi kupigania kadiri ya uwezo wako penzi lisifike mwisho, lakini kila kukicha mambo ndiyo yanazidi kuwa mabaya, unatakiwa kufanya nini? Uendelee kuteseka ndani ya moyo wako ukiamini ipo siku mwenzi wako atabadilika?

Kumbuka pia kwamba mateso ya kuendelea kuwa kwenye uhusiano usiofaa, ni hatari zaidi kuliko kuamua kuchukua uamuzi mgumu. Hakuna anayeshauriwa kuachana na mtu fulani waliyependana, waliyeishi naye pamoja na kufanya mambo mengi, lakini kuna wakati unafika, unakosa cha kufanya zaidi ya kutoa mkono wa kwa heri. Hata hivyo, ni wachache wanaoweza kuwa na uthubutu wa kuvunja uhusiano, hasa pale inapotokea kwamba mmeishi pamoja kwa muda mrefu na kufanya mambo mengi pamoja.

Kuachana siyo jambo rahisi, lakini kama nilivyosema, kuna wakati unafika inakuwa ndiyo njia pekee inayoweza kukunusuru na kukufanya urudi kwenye mstari katika maisha yako. Sasa je, unatakiwa kufanya nini ili kuumaliza kwa amani uhusiano ambao umekuwa tatizo kubwa kwako? Ufanye nini ili kumaliza mateso ya moyo unayoyapata kutoka kwa mwenzi wako?

Jambo la kwanza unalotakiwa kulifanya, ni kufanya tathmini ya penzi lenu, kuanzia mlikotoka mpaka hapo mlipofikia. Hiyo itakupa nafasi ya kuyatambua makosa yako kama yapo na kujifunza kupitia makosa hayo ili hata utakapoingia kwenye uhusiano mpya.

Jambo jingine, ni kuvuta picha ya maisha yako ya baadaye, bila kuwa na huyo anayeusumbua moyo wako. Je, utaweza kusimama imara na kuendelea na maisha yako? Kama jibu ni ndiyo, basi unaweza kuendelea na hatua za kuumaliza uhusiano uliopo ndani yake. Kama unaona hutaweza peke yako, basi unapaswa kuendelea kujipa muda zaidi kwa sababu moyo wako haupo tayari kuthubutu.

Jiulize ni nini hasa unachokitaka, ambacho kwenye uhusiano uliopo unaukosa? Wazungu huwa wanaita ‘soul searching’, kujihoji mwenyewe ndani ya nafsi yako. Ukiona kweli kabisa mwenzi wako amekuwa hakutendei haki, kile ambacho kwa kipindi kirefu umekuwa ukikihitaji hukipati, kama amani ya moyo, mapenzi ya kweli na kadhalika, basi tambua uamuzi wa kuondoka ni sahihi zaidi kwako kuliko kubaki.

Jiandae kisaikolojia. Kama nilivyosema, kuachana siyo jambo jepesi, wengi wamejikuta wakipiga ‘mark-time’ kwa sababu ya kukosa msimamo, leo mnaachana, siku chache baadaye mnarudiana! Hii ni kwa sababu hawakujiandaa na maumivu ya kuachana. Kama kweli unadhani umefika mwisho, lazima ujiandae kisaikolojia kupitia kwenye kipindi kigumu sana cha maumivu makali ndani ya moyo. Tambua kwamba utaumia, lakini hali hiyo itakuwa ni ya muda tu, yote yatapita na utasimama tena, ukiwa imara kuliko mwanzo.

Pambana na hofu ndani ya moyo wako, watu wengi wamejikuta wakiendelea kuishi kwenye uhusiano mbaya, wananyanyasika, wanateseka, wanasalitiwa na kufanyiwa kila aina ya ubaya, lakini bado wapo tu kwa sababu ya hofu ya kuachana. Wanaamini hawawezi tena kusimama imara, wanahisi kama kuachana kutafanya maisha yao yawe ni kama yamefika mwisho, wazungu wanaita ‘the fear of unknown’, yaani unaogopa kitu ambacho hakipo.

Wewe ni wa muhimu zaidi kuliko mtu mwingine yeyote, lazima ujilinde nafsi yako, lazima uhakikishe unaishi maisha ya amani, upendo na furaha. Kama mambo hayo yanakosekana, achana na hofu, songa mbele na Mungu atakujalia kumpata mwingine ambaye ataijua thamani yako. Kwa leo ni hayo tu, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri.

 

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO


Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Loading...

Toa comment