The House of Favourite Newspapers

Mambo ya kufanya unapokuwa na stress

0

 

SIKITIKO la mahaba lashinda msiba! Umewahi kusikia maneno hayo ya wahenga? Bora usimuliwe lakini usipitie kipindi cha sikitiko la mahaba (stress). Hakuna kipindi ambacho unaweza kuhisi kama dunia imefika mwisho kama pale unapoumizwa na yule uliyempenda kwa moyo wako wote. Kwa kawaida moyo unapopenda kwa dhati, huwa na kawaida ya kujisahau!

 

Hufikirii kama anaweza kukufanyia kitu chochote kibaya, unampa mapenzi kwa moyo wako wote. Unapopenda sana, ndivyo utakavyoumia sana itakapotokea amekubadilikia. Simaanishi watu wasipende sana bali unapopenda unapaswa kuwa makini ujue huyo unayemkabidhi moyo wako, kweli anayo hadhi hiyo?

Je, atakutunzia heshima yako?

Maana ukikosea lazima sikitiko la mahaba litakuhusu. Kwa mtu yeyote aliyewahi kupenda kwa dhati na baadaye akaja kuumizwa, atakuwa shahidi kwamba hakuna kitu kinachoumiza moyo kama mapenzi. Unajua kuna baadhi ya watu huwa hawajali kuhusu mioyo ya wenzao, anakufanyia jambo kwa makusudi bila kujua madhara atakayokusababishia.

 

Wapo ambao kwa sababu ya kushindwa kuyahimili maumivu ya mapenzi, hujikuta wakiyakatisha maisha yao! Wengine hujikuta wakipoteza kila kitu maishani, kisa kikiwa ni mapenzi. Unakuta mwingine hata kama alikuwa na kazi nzuri, inapotokea amekumbwa na dhoruba ya mapenzi, hawezi tena kufanya kazi
kwa ufanisi, muda wote machozi, muda wote ‘stress’ zimemjaa, matokeo yake anasimamishwa au kufukuzwa kabisa.

 

Wengine hujikuta wakitopea kwenye ulevi wa kupindukia, hiyo yote ikiwa ni kujaribu kutafuta sehemu ya kujificha, matokeo yake wanazalisha matatizo mengine makubwa zaidi na pengine mwisho wao unakuwa ni mauti.

 

Ni kweli mapenzi yanatesa sana lakini inapotokea umeumizwa kisawasawa na mtu uliyempenda kwa moyo wako wote, haimaanishi kwamba huo ndiyo mwisho wa maisha yako. Unaweza kusimama tena, ingawa huwa si kazi rahisi.

 

Kitu ambacho watu wengi huwa hawakikubali kirahisi ni ukweli kwamba mapenzi yanatesa kuliko unavyofikiri. Unaweza kutendwa na mwenzi wako uliyempenda sana, badala ya kushughulikia ‘stress’ zako, unajifanyisha kwamba hujaumia popote, kwamba wewe ni jasiri na utamsahau tu.

 

Matokeo yake, unalimbikiza tatizo ndani ya moyo wako ambalo litaendelea kukusumbua kwa muda mrefu mpaka utakapojua namna ya kulishughulikia. Jambo la kwanza unalopaswa kulifanya inapotokea mwenzi wako uliyempenda kwa dhati, mliyekuwa na ndoto nyingi pamoja, mliyepanga mambo mengi pamoja, amekutenda kwa namna yoyote ile, ameuvunja moyo wako na kukusababishia maumivu makali moyoni, ni kujipa muda wa kuwa peke yako.

Unapopata nafasi ya kuwa peke yako. Hata kama itakuwa ni kujifungia chumbani kwako peke yako, fanya hivyo, tulia kisha zungumza na moyo wako, kama unadhani kulia kunaweza kupunguza uchungu moyoni mwako, lia mpaka moyo wako utulie.

 

Jiulize mara kadhaa kuhusu uzito wa kosa alilokufanyia, jiulize mwenyewe, je, baada ya yote hayo unahitaji kuendelea kuwa naye au huwezi tena kuendelea. Wanachokosea wengi, akishakumbwa na kimbunga cha mapenzi, badala ya kupata muda wa kutosha wa kuwa peke yake, harakaharaka anaanza kuwasimulia marafiki au mashoga zake akitaka wamshauri nini cha kufanya.

 

Hayo ni makosa, unao uwezo wa kufanya uamuzi mzuri ukiwa peke yako kabla ya kuhitaji ushauri wa mtu. Endapo moyo wako unakwambia kwamba japokuwa amekukosea bado unampenda kwa dhati na unamhitaji, fanya kile moyo unachoona kinafaa.

 

Na endapo moyo wako unaona umefika mwisho kabisa na huwezi kuendelea, usikilize pia moyo wako. Ni hatari sana kufanya jambo ili kuwafurahisha watu wakati moyo wako unazungumza lugha tofauti. Yaani japo amekukosea lakini bado unampenda na upo tayari kumsamehe ila watu wako wa karibu wanakushauri uachane naye, usiwe mjinga wa ‘kushikiwa akili’, amua kile moyo wako ulichochagua.

 

Na kama moyo unaona ‘enough is enough’, basi shikilia kile moyo ulichoamua. Wiki ijayo tutaendelea kwa kuangalia nini cha kufanya ili kukabiliana na maumivu makali ya mapenzi inapotokea mwenzi wako amekutenda.

VIDEO: Mikanda ya Ubingwa wa Ndondi wa Global TV Afrika Mashariki na Kati Hadharani

Leave A Reply