The House of Favourite Newspapers

MAMBO YA KUMFANYIA MWANAUME WAKO AWE NA FURAHA

KWA hakika Mungu ni mwema. Tunakutana tena Jumamosi nyingine kwenye kilinge chetu cha kupeana elimu ya masuala ya uhusiano. Kama mada inavyojieleza hapo juu, leo tutaangazia zaidi kuhusu mambo ya kumfanyia mwanaume wako ili awe na furaha.  Japo wapo wanadamu wanaopenda karaha, lakini naweza kusema, asilimia kubwa ya wanadamu wanapenda kuwa na furaha. Wanapenda mioyo yao iwe na amani siku zote. Hakuna mwanadamu anayependa ugomvi labda awe na tatizo la akili. Hivyo basi, katika suala zima la uhusiano, furaha ni kitu cha msingi sana. Furaha inawawafanya wapendanao wazidi kustawisha penzi lao. Furaha inaleta maendeleo katika uhusiano na hata katika maisha ya kawaida.

Unapomfurahisha mwenzi wako, akili yake inawaza vizuri. Kama ni biashara ataifanya kwa kiwango kikubwa. Kama ni kazi ya kuajiriwa basi ataifanya kwa ufanisi wa hali ya juu hivyo ukimpa furaha mwenzi wako, unayakaribisha maendeleo ya penzi na maisha kwa jumla. Leo nazungumza zaidi na wanawake japo hayahaya yanaweza kufanywa na wanaume na yakaleta tija vilevile. Mambo haya si mageni na si makubwa, lakini unapoyafanya yanakuwa na maana kubwa japokuwa wengi wetu tumekuwa hatuyafanyi.

MUONESHE NI WA MUHIMU (COMPLIMENT)

Hili ni jambo la msingi sana katika uhusiano. Unapomuonesha mwanaume wako kwamba unathamini uwepo wake, unamthamini na

kumshukuru, hii humfanya ajisikie faraja. Wanaume wanapenda kuthaminiwa na kuonesha kwamba unampa kipaumbele. Muoneshe mwanaume wako kwamba yeye ndiye kila kitu kwako, unathamini mchango wake kwako. Kile anachokupa, anachokufanyia, muoneshe kwamba unakitambua. Unaguswa kutoka moyoni na mchango wake katika maisha yako, hii inastawisha sana penzi.

MSHUKURU KWA AJILI YAKO NA FAMILIA (APPRECIATE)

Shukurani ni jambo la msingi sana. Unapaswa kumshukuru mwanaume wako kwa yale yote mema anayoyafanya kwako na kwa familia yako. Mnapokuwa kwenye uhusiano, hususan uchumba au ndoa, faida ya uhusiano huo haiishii tu kwenu bali huvuka mipaka hadi kwa familia zote mbili. Kuna vitu ambavyo anaweza kukufanyia mwenza wako, unaona kabisa vinaigusa hadi familia yako, basi ni vyema kumshukuru. Shukurani inamfanya aliyekufanyia au kukupa jambo fulani aone umetambua mchango wake hivyo unaposema ‘asante’ inampa furaha zaidi moyoni.

TENGA MUDA MZURI WA FARAGHA (MAKE TIME IN THE BEDROOM)

Wengi wetu huwa tunajisahau katika eneo hili hususan wale wanandoa ambao wanakuwa wamedumu muda mrefu. Hatulipi kipaumbele jambo hili, tunaliona kama ni la ziada au litokee tu kama bahati mbaya. Kwa nini iwe bahati mbaya? Tunakosea sana!

Tunapaswa kutenga muda kwa ajili ya kukaa na wenza wetu chumbani. Tunapaswa kubadilishana mawazo chumbani, kupeana kampani nzuri faragha. Umpe ushirikiano wa kutosha kwenye faragha. Kuwa mbunifu wa mambo siyo kufanya mambo yaleyale kila siku. Weka simu zako pembeni, kuwa bize na mwenza wako faragha. Muangalie machoni kimahaba, lifanye tendo la faragha likate kabisa kiu ya mwenzi wako.

MFANYIE KITU (GET SOMETHING FOR HIM)

Hili pia ni jambo zuri sana, unapofanya jambo kwa ajili yako, basi mkumbuke pia mwanaume wako. Nunua kitu hata kama ni kidogo kwa ajili yako, lakini pia nunua kitu kwa ajili yake. Fanya jambo kwa kujipenda, mfanyie pia na yeye.

Muunge mkono kwenye kipindi ambacho anakuwa hayupo sawa kimawazo. Mrudishe, ungana naye kwenye nyakati ngumu. Kwa leo inatosha, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri. Unaweza kunifuata kwenye mitandao yangu ya kijamii, Instagram na Facebook natumia Erick Evarist, Twitter napatikana kwa ENangal

Comments are closed.