The House of Favourite Newspapers

MAMBO YA KUZINGATIA KABLA YA KUINGIA KWENYE UCHUMBA-2

KUWA na mume au mke bora ni matokeo ya kuwa katika uchumba ulio bora na sahihi. Hakuna kitu kinachokuja kwa wepesi, lazima kutumia muda wa kutosha ili kumpata mwenzi aliye bora na sahihi.  Tayari katika sehemu ya kwanza wiki iliyopita, tumeshaona baadhi ya mambo ya kuzingatia ili kupata mwenzi aliye bora. Nilisema kati ya mambo hayo ni kuchunguza mila na desturi za kabila la mchumba wako. Pili ni kujichunguza binafsi, ndani ya moyo wako kama unampenda kwa dhati. Jambo hili ni la muhimu sana, lazima uwe na uhakika kuwa, msichana/mvulana unayekwenda kuanzisha naye unampenda kwa dhati. Sasa tuendelee na mada yetu.

ANAYEKUPENDA  KIKWELI-KWELI

Hili ni muhimu kuliko la kwanza, ingawa ni vizuri kuishi na mwenzi unayempenda lakini pia ni lazima awe anakupenda! Sio vigumu sana kumfahamu mpenzi anayekupenda, lakini pia inawezekana ukaona anakupenda kumbe ni danganya toto!

Kimsingi katika hili ni lazima utumie akili yako yote uweze kutambua hilo. Nimeshaandika sana kuhusu sifa za mpenzi mwenye mapenzi ya dhati, lakini kwa kuongezea ni kwamba, anayekupenda huwa mvumilivu, anayekusikiliza pia mwenye kuwajali ndugu, marafiki na jamaa zako.

ELIMU ZISHABIHIANE

Suala la elimu ni muhimu sana kuangaliwa kabla ya kuingia kwenye ndoa. Wataalamu wa mambo ya uhusiano na mapenzi wanashauri wanandoa wawe na elimu zinazolingana au mwanaume amzidi mwanamke kwa kiwango chochote.

“Ni vichekesho mwanaume mwenye elimu ya darasa la saba kuoa mwanamke mwenye degree, hata kama watakuwa wanapendana kiasi gani, lazima kutakuja kutokea mikwaruzano tu. “Mwanaume ndiye kichwa cha nyumba, sasa kama mkewe atakuwa na elimu kubwa zaidi yake, ni wazi kwamba atakuwa amezidiwa maarifa na mkewe.

“Katika hali ya kawaida, wakati mwingine mwanaume anaweza akakosea jambo, mkewe akamwambia, ‘hujui chochote wewe, ulikimbia umande.’ Sasa katika hali kama hii kutakuwa na maelewano kweli?” hii ni kauli ya mtalaamu mmoja wa uhusiano alipokuwa akizungumza nami hivi karibuni, tukibadilisha mawazo.

Kauli yake ina ukweli, maana kama mke akiwa na elimu zaidi ya mumewe lazima kuwe na ugomvi wa hapa na pale, chanzo kikubwa hapa huwa ni dharau. Kwa upande wa mwanaume msomi hakuna ubaya wowote kumuoa mwanamke asiye na elimu kubwa, hata kama hajaenda shule kabisa! Tafiti mbalimbali zinaonyesha kwamba, wanaume wasomi wenye elimu ya juu, wakioa wanawake wenye elimu ya chini au wasio na elimu kabisa, ndoa zao hudumu zaidi kuliko wale wenye wake wenye elimu inayolingana.

Hivyo katika uchaguzi wa mchumba mwema na baadaye kuingia katika ndoa ni vyema kuangalia hili. Acha kudanganyika na maneno yake, maana wengine utawasikia wakisema, lakini sisi tunapendana bwana! Pamoja na kupendana huko ikiwa kuna upungufu huu, ndoa yenu haiwezi kufika popote.

MOYO SAFI

Lazima mchumba wako mtarajiwa, ambaye baadaye unatamani awe mwenza wako wa maisha awe na moyo safi. Moyo safi ninaozungumzia hapa ni pamoja na usikivu, uelewa, uvumilivu, kuchukuliana matatizo, moyo wa kusamehe, kutokumbuka makosa n.k Huna sababu ya kuingia katika uchumba na mpenzi ambaye ukimkosea na kumuomba msamaha hataki. Mtu ambaye hawezi kuchukua tatizo lako na kulifanya lake. Hana msaada na wewe hata wa mawazo tu, wa nini?

Suala la kuishi pamoja siyo lelemama, ni jambo linalohitaji kufikiria kwa uwezo wa juu. Siyo la kukurupuka! Kwa hakika kama unahitaji kuishi vizuri katika maisha yako ya ndoa ni lazima umpate mwenzi mwenye sifa hizo. “Kila siku unakosea, juzi tu nilikusamehe, jana tena ukanikosea na leo tena! Ah, mie siwezi jamani, wewe ni mtu wa aina gani?” kauli kama hii inatosha kabisa kukuthibitishia kuwa mwenzi wako atakuja kukusumbua baadaye.

Wiki ijayo nitakuwa hapa katika sehemu ya mwisho, USIKOSE!  Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Uhusiano anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vingi, vikiwemo True Love, Let’s Talk About Love na Maisha ya Ndoa vinavyopatikana kwa oda.

Comments are closed.