The House of Favourite Newspapers

MAMBO YA KUZINGATIA KABLA YA KUINGIA KWENYE UCHUMBA-3

HUU ni uwanja wa boyfriend and girlfriend ambao hutoa mwanga kwa wasichana na wavulana walio kwenye uhusiano na ambao wanatarajia kuingia kwenye uhusiano ili waweze kupata mwongozo sahihi.

 

Naamini mnanufaika na mafundisho yanayopatikana hapa. Somo ambalo tunamalizia leo ni kuhusu mambo ya msingi ya kuzingatia kabla ya kuamua kumpa mtu moyo wako na kuingia kwenye uhusiano naye moja kwa moja. Tayari tumeshaona mambo kadhaa katika matoleo ya awali, leo wakati tunamalizia, tuangalie vipengele vilivyosalia…

 

IMANI YA DINI…

Vijana wengi wakianzisha uhusiano huwa wanakwepa au hawaangalii kabisa suala la dini. Huambiana wanapendana na kuanza mapenzi huku wakijua wazi wana imani mbili za dini tofauti.

Mwisho wa siku mapenzi yakikolea, fikra za kuanza kuishi pamoja zinapokuja ndipo wawili hao watakapoanza kukulizana kuhusu dini! Hili ni kosa kubwa sana, ni vyema kuwa na mpenzi ambaye mna imani moja ya dini! Haijakatazwa watu wa imani mbili tofauti kuwa wapenzi, lakini mtakapofikia katika mchakato wa ndoa tatizo hili mtaliona na litakuwa kubwa sana kwa wakati huo.

 

Hapo kila mmoja atataka mwenzake ahamie katika dini yake ili waweze kufunga ndoa, lakini mwisho wa yote ni kwamba mtaishia kufunga ndoa ya Bomani. Si vibaya sana, lakini unatakiwa kufahamu kwamba ndoa ya Bomani ina athari zake, kubwa zaidi ni kwa watoto wenu; watafuata dini ya nani?

 

Hata hivyo wakati mwingine mtakapokuwa na matatizo katika ndoa yenu itakuwa rahisi zaidi kumaliza mambo hayo Kanisani au Msikitini kulikoni Bomani. Hili ni jambo la msingi ambalo wewe kijana unayetarajia kuoa unatakiwa kuwa makini kuliangalia.

 

Mnapoanza tu uhusiano wenu, kati ya vitu vya kwanza kabisa ambavyo mnapaswa kuvizu-ngumzia ni pamoja na dini. Kama mna imani mbili tofauti basi ni vyema mka-fanya shauri la mmoja wenu kuingia katika dini ya mwenzake mapema. Ikiwezekana jambo hili wazazi washirikishwe, hii itawasaidia kuepuka migogoro isiyo ya lazima pindi mtakapoamua kufunga ndoa. Mkiliweka wazi mapema, itawapunguzia mzigo mzito hapo baadaye.

BARAKA ZA WAZAZI

Ni tatizo kubwa sana kuwa na uhusiano na mpenzi ambaye wazazi hawamkubali. Katika kizazi cha sasa, ambacho vijana wamepewa jukumu la kuchagua wenzi wanaowataka, hili limekuwa tatizo kubwa. Utakuta mwingine anasema: “Ah! Mpenzi wangu nimempenda mwenyewe lakini wazazi wangu wananizuia kumuoa, mimi simsikilizi mtu, nausikiliza moyo wangu bwana! Ndoa nafunga hata kama wazazi wangu hawajaridhika, mimi ndiyo nimeamua!” Hili ni kosa kubwa sana.

 

Hakuna kitu cha msingi kama kupata baraka za wazazi katika ndoa. Ikiwa wazazi wako wanamkataa mchumba wako, zungumza nao taratibu, waulize polepole, nini tatizo na kwanini hawataki ufunge naye ndoa. Bila shaka watakueleza sababu za wao kumkataa. Lazima ukumbuke kwamba, kuna koo nyingine zina matatizo, sasa inawezekana wazazi wako wanaijua vyema familia hiyo na wanakuepushia matatizo, ndiyo maana wanakataa usiishi na mpenzi wako.

 

Wazazi ni kila kitu, usipowasiliza na kuwaheshimu wao, unatarajia nini kama siyo laana? Jambo hili unaweza kuwa nalo makini kuanzia mwanzoni, tengeneza mazingira ya mpenzi wako kukubalika na wazazi pamoja na ndugu zako, lakini pia na wewe inakubidi ufanye jitihada za kukubalika kwao, ili mwisho wa siku muweze kuishi katika ndoa safi, yenye baraka za wazazi wa pande zote mbili.

 

Usikubali kuutesa ubongo wako, naamini inawe-zekana. Fanya mabadiliko kijana ili utakapoingia kwenye ndoa hapo baadaye, iwe yenye amani na furaha na matarajio chanya! Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Uhusiano anaye-andikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vingi, vikiwemo True Love, Let’s Talk About Love na Maisha ya Ndoa vinavyopatikana kwa oda.

Maoni/Ushauri  Simu 0718 400146

Na Joseph Shaluwa

 

Comments are closed.