MAMBO YANAYOJITOKEZA MIEZI 7 MPAKA 9 YA UJAUZITO

MIEZI saba hadi tisa ya ujauzito huwa kwa kiasi kikubwa salama bila ya kuwa na dhoruba zozote na wakati huo tumbo linakuwa limeshakuwa kubwa na umeshasikia mtoto akicheza tumboni.  

 

Ndani ya miezi 7-9 ya ujauzito, mtoto hupata mabadiliko makubwa yanayohitimisha ukuaji wake. Huongezeka uzito kutoka kilo moja mpaka kilo tatu kwa wastani, viungo hukamilisha ukuaji ili aweze kuhimili ukuaji nje ya tumbo la mama.

 

Katika kipindi hiki cha tatu cha ujauzito (third trimester), baadhi ya dalili za mwanzo za ujauzito zinaweza kurudi au kujitokeza zaidi. Ni kipindi ambacho unaweza kuwa umechoka, ukitamani wakati ufike haraka ujifungue. Mjamzito anaweza kutegemea yafuatayo katika kipindi hiki:

 

MTOTO KUCHEZA

Kipindi cha pili cha ujauzito (second trimester) mjamzito huanza kuhisi mtoto akicheza tumboni, katika kipindi hiki atasikia zaidi mtoto akizidi kucheza kwani hujigeuza, kukunjua mikono na miguu. Wakati mwingine anaweza kuwa anacheza kiasi cha kukuamsha kutoka usingizini au kusababisha ukose usingizi.

 

MATITI KUKUA NA KUTOA MAZIWA

Muda wa kujifungua unapokaribia, mwili wa mjamzito nao huwa unajiandaa kuweza kumlea mtoto. Matiti ya mama yataendelea kukua, ili kuwa tayari kuanza kunyonyesha. Yanaweza kuanza kutoa maziwa ya njano hivi, haya ni muhimu kwa siku za mwanzo za mtoto akizaliwa.

 

TUMBO KUWA KUBWA ZAIDI

Mtoto tumboni anaendelea kukua mpaka kufikia wastani wa kilo 3.2 katika wiki ya 37. Kukua huku husababisha tumbo kuendelea kuwa kubwa, likikua kuelekea juu na baadaye kushuka chini wakati wa kujifungua unapokaribia.

MIKAZO KWENYE TUMBO

Mjamzito ataanza kupata mikazo ya tumbo isiyouma ambayo hujulikana kama Braxton Hicks Contractions, hutokea kwa muda mfupi na kuacha. Tofauti na mikazo ya uchungu (labor contractions), mikazo hii huwa haiumi na hujitokeza bila wakati maalumu. Endapo mjamzito anapata mikazo inayouma na kuongezeka kadiri muda unavyoenda awahi kituo cha afya mapema.

 

Mabadiliko ya kihomoni katika kipindi hiki huchangia kuongezeka kwa majimaji ya uke. Huwa ni ya kawaida yasiyowasha wala kuwa na harufu mbaya. Mjamzito aonane na daktari wake haraka endapo maji mengi yatatoka kwa ghafla, yenye damudamu au kuwasha.

 

KUUMWA MGONGO, KIUNO

Mtoto anavyozidi kukua, homoni hulegeza misuli ya mifupa ya kiuno na uzito wa mtoto kuja maeneo ya kiunoni. Mjamzito akae kwenye kiti chenye support nzuri, aepuke kuvaa viatu virefu na apate godoro zuri la kulalia yaani lisibonyee. Ikiwa maumivu ni makali yakiambatana na dalili nyingine, aonane na daktari mapema.

 

HAJA NDOGO MARA KWA MARA

Kipindi hiki atapata hali ya kukojoa mara kwa mara, na wakati mwingine mkojo kuvuja polepole bila kujua. Inatokana na tumbo la uzazi kukandamiza kibofu cha mkojo na hivyo mkojo kutoka mara kwa mara.

 

Ni vizuri ukavaa nguo za ndani za pamba na kufanya mazoezi ya Kegel ili kudhibiti mkojo unaovuja. Endapo mjamzito unapata maumivu wakati wa kukojoa, maumivu chini ya tumbo, homa na kukojoa mara nyingi zaidi ya kawaida, onana na daktari kwani zinaweza kuwa dalili za U.T.I.

 

Katika kipindi hiki tumbo la uzazi hukua kuelekea juu na hivyo kulisukuma tumbo la chakula kutoka katika nafasi yake, hivyo kusababisha asidi ya tumboni kurudi kwenye mrija wa chakula na kusababisha kiungulia. Mjamzito pata mlo kidogo lakini mara kwa mara, punguza juisi zenye machungwa, ndimu au malimao. Kiungulia kikikusumbua sana onana na daktari wako juu ya dawa.

HEWA YA KUTOSHA

Kutopata hewa ya kutosha au kushindwa kupumua vizuri ni hali inayojitokeza mara kwa mara katika kipindi hiki. Hii inatokana na tumbo la uzazi kusukuma mapafu na kuongezeka kwa mahitaji ya oksijeni. Mazoezi ya kutembea na kulalia mito inaweza kusaidia kupunguza hali hii. Endapo mjamzito unapata shida kupumua kiasi cha kushindwa kutembea au kufanya shughuli nyepesi, onana na daktani wako.

 

MISHIPA YA DAMU

Kuongezeka kusambaa kwa damu mwilini kunaweza kusababisha mishipa ya damu kujitokeza kwenye ngozi za sehemu za tumboni, miguuni na utumbo mpana. Hujulikana kama varicose veins kwa kitaalamu. Mishipa inayojitokeza sehemu ya chini ya utumbo mpana (rectum) huweza kusababisha kupata choo chenye damu. Hakikisha unapata maji ya kutosha na chakula chenye kambakamba kwa wingi.

 

USHAURI UKIONA DALILI HATARI

Mjamzito ukiona mojawapo ya dalili hizi wakati huu wa ujauzito onana na daktari wako haraka. Kutokwa na maji au ute mwingi ukeni, kutokwa na damu ukeni, maumivu makali ya tumbo, kutokwa na majimaji au ute mwingi zaidi ya kawaida ukeni, mtoto kuacha kucheza tumboni.

Toa comment