The House of Favourite Newspapers

Mambosasa Awaonya Wang’oa Viti kwa Mkapa

0

KUELEKEA mchezo wa watani wa jadi, Yanga dhidi ya Simba, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Lazaro Mambosasa, ametoa onyo kali kwa wale watakaothubutu kung’oa viti na kufanya vurugu kwenye mchezo huo.

 

Yanga inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara unaotarajiwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar, leo Jumamosi.

 

Msimu wa 2016/17, timu hizo zilipocheza zilitoka sare ya bao 1-1, lakini bao la Yanga lililofungwa na Amisi Tambwe, lilisababisha mashabiki waliodhaniwa kuwa ni wa Simba (kutokana na upande waliokuwa wamekaa na rangi za nguo zao) kung’oa viti.

 

Akizungumza jijini Dar, Kamanda Mambosasa alisema kuwa kwenye mpira wa miguu kuna matokeo matatu, hivyo mashabiki wakubaliane na lolote litakalotokea.

 

“Mpira una matokeo matatu, kuna ushindi, kushindwa na kutoa sare na wajiepushe na mihemko ya kishabiki, mara nyingi baada ya kushindwa watu wanahangaika kung’oa viti kwani viti vina kosa gani?

 

Leo umeshindwa na kesho utashinda, suala la kuharibu mali na kufanya vurugu ni uchwara kwenye ushabiki, niwaombe wawe watulivu, wanadi timu zao na wajiandae kwa matokeo,” alisema kamanda huyo.

Leen Essau, Dar es Salaam

Leave A Reply