The House of Favourite Newspapers

Mameneja 9, Mkurugenzi Mstaafu Dawasco Watumbuliwa

0
Kikao kikiendelea.
WAZIRI wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge amewasimamisha kazi mameneja tisa wa Shirika la Majisafi na Majitaka la Dar es Salaam (Dawasco), akiwamo mkurugenzi aliyestaafu kwa tuhuma za kulisababishia shirika hilo hasara ya Sh2.8 bilioni.
Awali utumbuaji majipu, ambao unalenga kuondoa ufisadi na uzembe katika utumishi wa umma, ulikuwa ukihusisha watendaji walio kazini, lakini jana Waziri Lwenge alisema aliyehusika kwenye tuhuma hizo za ufisadi wa kitaasisi atachukuliwa hatua hata kama ameshaachia nafasi yake.
Akizungumza katika mkutano wake na watendaji wakuu wa shirika hilo, Waziri Lwenge alisema kusimamishwa kwa watumishi hao ni kutokana na kutuhumiwa kushiriki katika njama za kuiunganisha maji kampuni ya Strabag bila kufuata utaratibu.
Aliwataja watumishi waliosimamishwa kuwa ni Peter Chacha, Regnald Kessy, Theresia Mlengu, Josper Kilango, Fred Mapunda, Mvano Mandawa, Emanuel Gulupa, Raymond Kapyela na Jumanne Mapunda.
Waziri Lwenge pia ameagiza aliyekuwa mkurugenzi wa shirika hilo ambaye alistaafu, Jakson Midala naye achunguzwe ushiriki wake katika njama hizo kwa kuwa zilifanyika wakati wa uongozi wake.
Sambamba na maagizo hayo, waziri huyo wa maji ametoa siku 14 kwa Strabag kulipa kiasi hicho cha pesa kilichokwepwa vinginevyo hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya kampuni hiyo.
Strabag ni kampunii ya ujenzi inayoshughulikia utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Mabasi yaendayo Haraka (BRT).
Waziri alisema kampuni hiyo kwa kushirikiana na wafanyakazi wasio waaminifu wa shirika hilo la maji walifanikisha kuunganisha maji bila kupata vibali na kufuata utaratibu.
Alisema baada ya kuunganishiwa maji, Strabag walianza kuyatumia katika ujenzi wa barabara hizo bila kuyalipia na kulikosesha shirika mapato yake.
Alisema uunganisho huo ulifanyika mwaka 2014 kutoka kwenye mabomba yenye vipenyo vikubwa (DN 100 na DN 400).
Alisema ukubwa wa mabomba yaliyotumika kuunganisha maji ni ushahidi kuwa watumishi wasio waaminifu wa Dawasco walishiriki katika mpango huo.
Alisema kutokana na matumizi hayo ya maji yasiyolipiwa, Serikali imekosa mapato ya shilingi 2.887,577,134.
Waziri pia aliagiza bodi ya Dawasco kusimamia menejimenti ya shirika hilo na kusaidia kumaliza tatizo la upoteaji wa maji linalosababishwa na kupasuka kwa mabomba pamoja na wizi.
Pia aliagiza bodi isaidie kutatua kero za wananchi, hususan kusambaza maji kwa wananchi wasiopata huduma hiyo, usomaji mbaya wa mita za maji unaosababisha wananchi kulipia ankara kubwa zisizolingana na matumizi halisi.
“Naiagiza bodi vilevile iweke mipango endelevu itakayohakikisha asilimia ya wananchi wanaopata huduma ya majisafi inafika 95 ifikapo mwaka 2020,” alisema.
Mtendaji Mkuu wa Dawasco, Mhandisi Cyprian Luhemeja alisema changamoto kubwa inayolikabili shirika hilo ni upotevu wa maji ambao mbali na wezi, pia unasababishwa na uchakavu wa mitambo ambayo mingi ni ya miaka 1970.
Naye mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Dawasco, Meja Jenerali Samwel Kitundu alimuomba waziri kulisaidia shirika hilo kuweza kukusanya madeni yake inayozidai taasisi za Serikali ambazo bila kuzitaja alisema zinadaiwa madeni makubwa.
Pia, Kitundu aliitaka serikali iweke sheria kali dhidi ya wezi wa maji ili waweze kuwabana wanaokamatwa kuhusika na vitendo hivyo vinavyochangia kulikosesha shirika hilo mapato yake.
Akizungumzua tuhuma hizo, ofisa uhusiano wa Strabag, Yahaya Mkumba alisema si kweli kuwa hawakufuata taratibu zote zinazotakiwa ili waunganishiwe maji, ingawa alisema maji hayo yalikuwa hayatoshelezi mradi na kuwalazimu kununua ili kukidhi mahitaji yao.
Alikiri kuwapo kutokuelewana kwa kampuni yake na shirika hilo katika gharama za maji wanazopelekewa lakini akasema suala hilo walilimaliza kisheria.

“Wamekuwa wakituletea bili zisizoeleweka, hata hivyo tuliamua kulishughulikia suala hili kisheria,” alisema Mkumba.

Pichani ni Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Inj. Gerson Lwenge (katikati) akiongozana na Mwenyekiti wa bodi ya Shirika la Maji taka na Maji safi Dar es Salaam (DAWASCO), Meja General (mstaafu), Samuel Kitundu (kushoto) na Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASCO, Cyprian Luhemeja , wakati Waziri huyo alipoitembelea Dawasco jana na kisha kutangaza watumishi tisa ambao ameiagiza bodi kuwasimamisha kazi kupisha uchunguzi dhidi yao kufuatia tuhuma mbalimbali.
Mameneja wa DAWASCO wakiwa katika mkutano huo. Baadhi yao walisimamisha kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazo wakabili.
Leave A Reply