Mamilioni Ya Kanumba Yazua Tafrani Tena – Video
NGOMA nzito! Ndivyo unavyoweza kutamka kutokana na mamilioni ya aliyekuwa staa wa filamu Bongo, marehemu Steven Kanumba kuzua tafrani tena kwa mama yake, Flora Mtegoa na baba, Charles Kanumba.
Mamilioni hayo ya shilingi ambayo yanatarajiwa kutolewa na kampuni ambazo ziliwahi kufanya kazi na Kanumba enzi za uhai wake yanatarajiwa kutoka hivi karibuni ambapo baba mzazi ambaye anaishi mkoani Shinyanga naye anahitaji haki yake, yaani wagawane nusu kwa nusu na mama Kanumba.
Akizungumza kwa njia ya simu baba Kanumba alisema tayari ameshaweka pingamizi kuhusu fedha hizo asipewe mama Kanumba pekee kama zilivyokuwa zile za mwanzo bali wanawatakiwa wapewe wote kama wazazi.
“Mama Kanumba hakumpata Kanumba peke yake bali mimi kama baba nahitaji haki yangu na mimi, inakuwaje mama Kanumba amechukua zile fedha za mwanzo zilizotolewa na makampuni mbalimbali yaliyofanya kazi na Kanumba, amekula mwenyewe? Sasa sikubali,” alisema baba Kanumba.
TAFRANI TENA
Licha ya mwanzoni kuzua gogoro na baba Kanumba kutokuambulia chochote, hivi sasa tafrani imezuka upya kwani tayari baba Kanumba ameshakubaliwa pingamizi aliloweka na fedha haziwezi kutoka kwa mtu mmoja ambaye ni mama Kanumba bali ni mpaka wote wawepo.
Akizungumza na Amani, mdogo wa Kanumba, Mjanaeli Kanumba alisema fedha za Kanumba awamu ya pili zilitarajiwa kutoka hivi karibuni ambapo kutokana na pingamizi la baba yao bado hazijatoka.
“Baada ya kuweka pingamizi, lilikubalika na baba aliitwa na Bodi ya Filamu afike Dar au atume mwakilishi kwenye kikao ambacho kingefanyika Februari 11, mwaka huu ambapo alinituma mimi nimwakilishe.
“Nilifika bodi ya filamu lakini cha kushangaza nikaambiwa kikao cha wajumbe wanaoshughulikia suala la fedha za Kanumba walikaa jana yake wakiwa na mama Kanumba na mama huyo kukubali kuwa atampa mgao mzee Kanumba lakini kidogo kama sadaka.
“Baba kusikia hivyo akakataa na kushikilia kwamba lazima wagawane sawa na mama Kanumba maana ni vitu vingi vya Kanumba ametumia mwenyewe bila kumshirikisha,” alisema Mjanaeli.
Mjanaeli aliendelea kusema kuwa walikubaliana na watu wa bodi ya filamu kuwa kikao kijacho kitakachofanyika baada ya mtu anayehusika na fedha kwenye kampuni husika kurejea kutoka safarini watakuwepo pande zote mbili na hapo ndipo zitajulikana mbivu na mbichi.
“Tunasubiri tuitwe kikao cha makubaliano kati ya mama na baba Kanumba ikishindikana tunapeleka kesi hii mahakamani,” alisema Majanaeli. Alipotafutwa mama Kanumba kuhusu suala hilo, simu yake iliita bila kupokelewa. Jitihada zinaendelea.
Stori: Gladness Mallya, Amani