The House of Favourite Newspapers

MAMISI KUVAMIA GEMU LA MUZIKI SABABU HIZI !

Image result for amber lulu
Amber Lulu’

KWA miaka ya hivi karibuni tumekuwa tukiona warembo wengi wa kike wakijiingiza katika kuuza nyago ‘video queen’ kwenye video za Bongo Fleva akiwemo Gift Stanford ‘Gigy Money’, Lulu Euggen ‘Amber Lulu’, Lulu Abbas ‘Lulu Diva’, Haitham Kim na wengine wengi. 

 

Lakini wauza nyago haohao, sasa hivi wameona kuwasaidia wasanii wenzao kuuza nyago kwenye video haiwaingizii kitu zaidi ya kupata sifa tu! Wapo waliowahi kujitokeza hadharani akiwemo Gigy na Amber Lulu na kulalamika kulipwa kiduchu (shilingi elfu 20) kwa video moja ya Bongo Fleva.

 

Leo hii wauza nyago hao ndiyo wanaotikisa kwenye Bongo Fleva, huwezi kutaja kumi bora ya wasanii wa kike wanaotikisa Bongo usiweke majina yao. Mbali na hao waliokuwa wauza nyago kisha kuhamia kwenye Bongo Fleva, wapo pia warembo waliowahi kushiriki na wengine kushinda katika mashindano ya urembo Tanzania kama vile Genevieve Emmanuel, Hamisa Mobeto na wengineo ambao leo hii ni wasanii pia wa Bongo Fleva. Star Showbiz limechambua sababu hasa za warembo wengi (mamis) kukimbilia kwenye muziki huo.

 

MUZIKI BIASHARA

Ni moja kati ya sababu kubwa inayowasukumua mamis wengi kuingia katika muziki wa Bongo Fleva. Kutokana na ishu ya urembo kuwa hailipi kivile mara baada ya kushinda taji, wengi wao wanaamua kujiingiza kwenye muziki kwa kuamini watapata chochote. Ni ukweli usiopingika kuwa muziki huu kwa sasa unalipa, kama siyo kwenye shoo basi kwenye mitandao ya kijamii (Youtube), ukiwa na channeli yako kisha kazi zako ukawa unaziweka humo, malipo yanakufuata kwa njia ya idadi ya views utakaokuwa unaipata.

Image result for lulu diva

KUJITANGAZA

Wapo mamis wanaoingia kwenye muziki kama njia ya kujitangaza tu na siyo kufaidika na chochote. Kwa kuwa amegundua mbali na urembo ana kipaji cha kuimba, anaingia kujitangaza mashabiki wamtambue kama anajua pia muziki.

 

Mfano mshiriki wa Miss Kinondoni 2014, Haitham Kim mara baada ya kushiriki mashindano hayo aliamua kujikita moja kwa moja kwenye Muziki wa Bongo Fleva, alianza kuwa kama video Queen na baadaye akaamua kusaini mkataba na Lebo ya MJ Records na kujitangaza rasmi kipaji chake cha kuimba na sasa amekuwa hasikiki kivile kama ilivyokuwa awali.

 

Mwingine ni Miss Tanzania namba mbili 2006 ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo. Jokate naye  aliingia kwenye muziki kama njia ya kujitangaza kwa mashabiki wake watambue kuwa mbali na shughuli za urembo na ujasiriamali pia ni msanii wa Bongo Fleva. Wimbo wake wa kwanza uliomtambulisha ulikuwa Kaka na Dada aliomshirikisha Prodyuza Lucci pamoja na Leo Leo aliomshirikisha msanii kutoka Nigeria, Ice Prince. Baada ya kuachia nyimbo hizo, aliingia ‘mitini’ hadi alipotangazwa kuwa ni mkuu wa wilaya.

 

HESHIMA

Hii nayo inachangia kwa kiasi kikubwa, kuna wanaoona kwa kuwa wameshafanya mashindano ya urembo, video queen na kutambulika, wanaona wakifanya na muziki itawajengea heshima kubwa na pia itawafanya kuaminiwa na jamii na hata kusaidiwa kupitia muziki watakaokuwa wakiufanya. Mfano, Hamisa Mobeto ambaye ni mshindi wa pili wa Miss Dar Indian Ocean 2011 na mshindi wa Miss Kinondoni kwa mwaka huo aliyefanikiwa kufika hadi nusu fainali ya Miss Tanzania, alianza kujiingiza kwenye muziki kama muuza nyago kwenye video za Bongo Fleva kisha akajikita kwenye ujasiriamali na sasa naye ni msanii wa muziki.

Mobeto anasema kuwa, lengo la kuingia kwenye muziki ni kujiwekea heshima na kuaminiwa kupitia kazi zake ikiwemo Mobeto Foundation. Kwa sasa anatamba na Wimbo wa Madam Hero ambao anasema lengo la kuimba wimbo huo ni kuwafikia wanawake wote na kuwatia nguvu ya kupambana wasikate tamaa. “Pesa ya mauzo nitakayopata kupitia wimbo huu wa Madam Hero yataenda kwa wakina mama wote wanaowalea watoto wao kwenye mazingira magumu na kwa wanojifungua katika hali ngumu.”

 

USHAWISHI

Ni sababu nyingine kubwa inayosa babisha baadhi ya mamis wengi kukimbilia katika muziki huu kwa kushawishika. Kuna wengine wakiona f’lani alikuwa miss akaingia kwenye muziki na kufanikiwa basi na yeye anaingia, au nyuma yake kuna watu wanamshawishi kuwa akifanya muziki atang’aa.

 

Mfano, Miss Tanzania 2010, Genevieve Emmanuel ambaye licha ya kuwa na kipaji lakini anakiri kuwa alishawishiwa kujaribu Bongo Fleva “Muziki ni kipaji changu na ni moja ya kitu nilichokuwa nikikipenda sana tangu zamani. Kuna watu walikuwa wakiniha masisha na kuniambia muziki utanifanya niwe huru na kuniletea mafanikio nikaamua kujiingiza na mimi nijaribu,” anasema Genevieve ambaye alitoa Wimbo wa Nana.

Image result for hamisa mobeto

NDOTO

Baadhi ya mamis waliovamia muziki huu, waliwahi kukiri kuwa ndoto zimechangia kwa kiasi kikubwa kufika walipo. Lulu Diva ambaye ni mshindi wa pili Miss Pwani 2013 na mshindi wa Miss Kibaha kwa mwaka huo anasema kuwa, wakati anaanza kushindania urembo, ndoto yake kubwa ilikuwa kuja kufanya muziki wa Bongo Fleva.

 

“Nilikuwa natamani nitambe kwenye muziki niweze kuwa kama K-Lyinn na wengine waliokuwa mamis, lakini leo hii ndoto yangu imetimia na natambulika kama msanii wa Muziki wa Bongo Fleva niliyekuwa mrembo wa mashindano ya umiss,” anasema Lulu Diva.

Comments are closed.