Manara: Kila Mwezi Simba Inalipwa Sh 130M Kutoka Fedha Za Mo Dewji

MSEMAJI wa Simba, Haji Sunday Manara alifanya ziara ya kutembelea chumba kikubwa zaidi cha habari nchini cha Global Group kujionea namna kazi ya uchakataji habari kupitia magazeti, radio na runinga unavyofanyika.
Wakati akiwa katika ziara hiyo juzi, Manara alipata nafasi ya kuzungumza mambo kadhaa wakati wa mahojiano maalum na moja ya jambo alilolizungumzia ni kuhusiana na Simba kuwa inaingiza fedha zaidi ya Sh milioni 130 kila mwezi kama gawiwo kutoka kwenye fedha ya mwekezaji.
MALIPO YA MWEKEZAJI MO DEWJI:
Fedha inayotakiwa kutolewa na mwekezaji ni Sh bilioni 20 ili amiliki sehemu ya 49% ya klabu hiyo na Manara amesema fedha hizo kama walivyokubaliana zimeingizwa benki ambako watakuwa wakipata gawio ambalo tayari wameanza kulipata kwa kuchukua zaidi ya sh milioni 130 kila mwezi.
“Simba ishaanza kupokea sehemu ya gawio au ziada lakini kuna fedha tunapata kutoka katika fixed account. Mfano ukiweka milioni 100 kuna kiasi fulani unapata, sasa kwa fedha iliyowekwa sisi tunapata na inatusaidia katika masuala ya mishahara.
“Sisi niseme nia ya mabadiliko ipo na kubwa sasa Simba inakula fedha ya gawio kutoka katika fedha tuliyokubaliana iwekwe kama sehemu ya manunuzi ya Simba,” anasema Manara.
“Nimesikia hili limeibuliwa na haya ndiyo majibu yake na huenda wengi hawajui kwa kuwa hatujasema. Tunapata fedha hizi nyingi na kwa mwaka kupitia gawio hilo tunaweza kupata angalau Sh bilioni 1.5.
“Nilimsikia kiongozi mmoja anasema bajeti ya mwaka ni Sh bilioni 5 au 6 hivi, ndio maana nasema hii yetu haitoshi, ndio maana tunaendelea kujiboresha kwa lengo la kutunisha mfuko na kuifanya klabu iweze kujiendesha kwa uhakika.
“Angalia tunafanya na Equity Bank kwa lengo hilohilo, ile kadi moja ya mwanachama inauzwa Sh 22,000. Hapo Simba inapata Sh 14,000 na hapa lengo ni kutunisha mfuko utakaoweza kujiendesha lakini hata kununua wachezaji hao wakubwa.
ZIARA YAKE BARANI ULAYA:
“Kwanza nilikwenda kama balozi wa La Liga, hii ilikuwa ni Hispania. Baada ya nikaanza ziara ya nchi mbalimbali kuhusiana na masuala ya kampuni yangu.
“Nina kampuni inayojishughulisha na masuala ya promosheni, lengo ni kuungana na mawakala kwa ajili ya kupeleka vijana barani Ulaya.
“Nilianza Ufaransa nikakutana na mawakala wakubwa na baadaye nikaenda Ubelgiji ambako sikufanikiwa sana kutokana na Corona kuwa imekolea,” anasema Manara na kuongeza.
“Ujerumani sikufanikiwa sana lakini nilialikwa na klabu ya Hamburg sikufanya, lakini nilialikwa kwenda kuzungumza na Rais wa Bayern Munich, Karl-Heinz Rumminegge lakini sikuweza kukutana naye kutokana na suala la Corona hivyo tumekuwa tukiwasiliana zaidi kwa email.
“Katika mazungumzo yetu, inaonekana wao hawajawalenga hawa wanaocheza sasa, badala yake ni watoto wanaocheza leo kwa malengo ya kuwakuza. Mfano Lyon ya Ufaransa, mkurugenzi wa michezo aliniambia hakuna namna yoyote kuleta wachezaji wakubwa wanaocheza sasa lakini wanachoangalia ni hao vijana kuanzia watoto hadi kufikia miaka 16.
“Walitaka kuja hapa kutafuta watoto watano, wao Lyon. Walitaka niandae michuano ya watoto ya Knockout kwa ajili ya kupata hao watoto ambao wako tayari kuwachukua.
“Pia nimezungumza na mawakala wa hapa Tanzania, wana hamu ya kuungana na mimi katika hili. Kuna ile timu aliyocheza baba yangu kule Uholanzi nayo iko tayari kuchukua watoto lakini walikuwa na masharti magumu kidogo kwa kuwa wanataka ukiwapeleka kule watoto basi uwahudumie kwa maana ya makazi na malazi,” anasema Manara.
Stori: Na Mwandishi Wetu




