Manchester United Yatangaza Kumrejesha Antony Kuendelea na Mazoezi
Manchester United imetangaza kumrejesha winga Antony kuendelea na mazoezi kwa ajili ya kuwa fiti kwa mechi zijazo za klabu hiyo. Winga huyo alipewa likizo mnamo Septemba 10 baada ya aliyekuwa mpenzi wake Gabriela Cavallin kumshutumu kwa kumfanyia vitendo vya unyanyasaji huku wanawake wengine wawili wa Brazil wakijitokeza na madai kama hayo.
Taarifa ya Manchester United imebainisha sababu ya kumrejesha Mbrazil kikosini ni kwamba Antony hajakamatwa au kushtakiwa nchini Brazil au England hivyo ana haki ya kuendelea kuitumikia klabu hiyo wakati uchunguzi wa polisi unaendelea.
“Kama mwajiri wa Antony, Manchester United imeamua kwamba ataanza tena mazoezi Carrington, na atakuwa tayari kwa ajili ya kuchaguliwa kucheza, wakati uchunguzi wa polisi ukiendelea. Hili litawekwa chini ya uangalizi ikisubiri maendeleo zaidi katika kesi hiyo.
“Kama klabu tunalaani vitendo vya unyanyasaji na unyanyasaji. Tunatambua umuhimu wa kuwalinda wale wote wanaohusika katika hali hii, na tunakubali athari zinazotokana na tuhuma hizi kwa waathirika wa unyanyasaji.”
Antony anatarajiwa kufanya mazoezi leo Ijumaa na huenda akawa sehemu ya kikosi cha klabu hiyo kitakachoikabili Crystal Palace katika mechi ya Ligi Kuu England leo Jumamosi.