The House of Favourite Newspapers

MANDOJO KUVUNJIWA NYUMBA YA MAMILIONI… KUNA KITU!

BAADA ya msanii mkongwe wa Bongo Fleva, Joseph Francis Michael ‘Mandojo’ kuvunjiwa nyumba yake ya mamilioni iliyokuwa maeneo ya Mbweni jijini Dar, imeelezwa nyuma ya tukio hilo kuna kitu kimejificha, Ijumaa Wikienda.

Mandojo alipata janga hilo Alhamisi iliyopita ambapo alisikika katika vyombo vya habari akielezea tukio hilo ambalo lilimuibua Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi aliyemtaka afike nyumbani kwake ili aone namna ya kumsaidia.

 

Akizungumza na kituo kimoja cha televisheni, Mandojo alisema kuwa, siku ya tukio alikuwa safarini ambapo nyumbani hapo alikuwepo mdogo wake ambaye ghafla alivamiwa na watu wasiojulikana, wakiwa na askari na kuanza kuibomoa nyumba yake hiyo.

Aliendelea kueleza kuwa, watu hao ambao wengine walikuwa wamevalia vitambaa usoni ili wasitambulike, walibomoa nyumba hiyo huku wakichukua vitu kibao zikiwemo kompyuta mpakato ‘laptop’ na vingine vingi.

Wakizungumzia tukio hilo kwa nyakati tofauti, baadhi ya wakazi wa Dar walisema kuwa, nyuma ya tukio hilo huenda kuna kitu kwani haliwaingii akilini na limewaacha na maswali mengi.

“Yaani unajua inaonekana kuna kitu tu kimejificha nyuma ya hili tukio. Haiwezekani mtu umevunjiwa nyimbo halafu katika mahojiano kuhusu tukio, unaonekana una furaha tu kana kwamba umevunjiwa sahani,” alisema Dullah Kikoi, mkazi wa Sinza.

 

Mkazi mwingine wa Mbweni ambaye hakupenda jina lake lichorwe gazetini, alipigilia msumari kuwa kuna kitu kwa kuhusisha na mazungumzo hayo ya Mandojo baada ya kuvunjiwa.

“Wewe angalia mtu anapata hadi ujasiri wa kushusha mashairi yake katika mahojiano hayo unafikiri kuna nini hapo? Yaani ni kama kuna kitu kinafanyika ili tu kutengeza huruma fulani na baadaye ataonekana na maisha mazuri licha ya kuvunjiwa,” alisema mkazi huyo.

 

Mbali na hao, Ijumaa Wikienda lilizungumza na wadau wengi wa masuala ya burudani ambao walieleza kuwa, huenda suala hilo likawa ni la kiki ya kimuziki au pia huenda kuna jambo linafichwa.

“Unajua hawa wasanii siku hizi sasa unashindwa hata kujua ukweli ni upi maana kiki zimekuwa nyingi, huenda kuna jambo pia kalificha katika maelezo yake maana pia tulisikia wale waliombomolea, walifanya vile baada ya kushinda kesi mahakamani.

“Lakini kwa kuwa ameitwa na mkuu wa wilaya, ukweli utajulikana,” alisema mdau mmoja mkubwa wa burudani Bongo.

Mmoja wa majirani alilielezea tukio hilo kuwa kiwanja alichokuwa amejenga msanii huyo kilikuwa na mgogoro kwa muda mrefu ambapo kesi ilikuwa mahakamani na alipokuwa akipelekewa taarifa alizembea kwenda kwenye kesi.

 

“Mandojo aliitwa mara kadhaa mahakamani hakuwahi kufika mpaka kesi inaisha, uamuzi ukatolewa kwamba nyumba ibomolewe kwa kuwa kiwanja hicho siyo cha msanii huyo, lakini kila walipokwenda kwa ajili ya kubomoa walikutana na vitisho kwani walikuwa wakikimbizwa kwa panga na kushindwa kubomoa.

“Naona kutokana na vitisho hivyo ndiyo maana wakaamua waje kwa mtindo mwingine wa kimafia zaidi na kufanikiwa kuibomoa nyumba hiyo,” alisema jirani huyo ambaye hakutaka jina liandikwe gazetini.

Stori: Mwandishi Wetu, Dar

 

MBOWE BAADA YA KUACHIWA: Nimeyaona Mengi Gerezani – Video

Comments are closed.