Maneno mabaya, makali ni sumu kwenye mapenzi-2
Mpenzi msomaji wa XXLove ni Jumatatu nyingine murua tunakutana hapa jamvini kwa ajili ya mwendelezo wa mada yetu ya wiki iliyopita iliyokuwa na kichwa cha; ‘Maneno Mabaya, Makali ni Sumu Kwenye Mapenzi’.
Wiki iliyopita nilizungumza kwa upande wa maneno ambayo wanaume huwaambia wapenzi wao wa kike lakini leo nitanena maneno hatari au mabaya ambayo mwanamke humwambia mpenzi wake wa kiume au mumewe kisha kukutana na balaa.
Baadhi ya wanawake wanapokuwa wamekwazika na makwazo ya wapenzi wao, hujisahau na kuanza kupayuka, jambo linalomsababisha kutokwa na maneno kama vile; ‘kwanza mwanaume mwenyewe suruali, huna lolote, mwanaume hujali familia, hujiwezi faragha na kwa taarifa yako huyu siyo mwanao ana baba yake’.
Ni kosa kubwa kumwambia mwanaume maneno hayo. Kwamba, mtoto mliyejaliwa siyo wake, inawezekana ni kweli au umeongea kwa sababu ya jazba lakini ukweli ni maneno makali na ya hatari sana ambayo huuchoma vilivyo mtima wa mwanaume na kujiona si lolote mbele yako.
Hilo ndilo tusi kubwa na baya kwa mwanamke kumtukana mwanaume, kwani ni kama kumvua nguo na kumbakiza mtupu mbele ya kadamnasi ni kuonesha umemdharau vya kutosha.
Nimebaini kuwa maneno hayo husababisha chuki kubwa sana kwa mwanaume dhidi ya mtoto, haijalishi ni ukweli au la. Uvumilivu wa kufuatilia hilo ni mgumu sana hivyo mwanaume mwenye msongo wake wa mawazo, akifikiria namna alivyohangaika kulea mimba, mtoto na hata kumsomesha halafu leo unamtamkia wazi kuwa kumbe mtoto mwenyewe siyo wa kwake, basi ujue hapo unakaribisha shetani na hatari ndani ya uhusiano wako.
Na ndiyo maana kuna matukio kadha wa kadha ambayo tumeshuhudia yakiandikwa au kuoneshwa na vyombo mbalimbali vya habari, kuwa baba amemchinja mama na mtoto au mke tu. Mara nyingi hiki huwa ni kisasi cha yale maneno makali ya mwanamke kwa mume au mpenzi wake.
Kimsingi wapenzi mnaopokuwa mmefarakana ni muhimu sana kuchunga, kuangalia au kufikiria maneno ambayo unayatoa kwa mwenza wako ili kuepusha mtafaruku mkubwa zaidi ambao unaweza kusababisha athari kubwa zaidi na mara nyingine mauaji ya kinyama. Nina imani mmenielewa wapendwa!
Usikose wiki ijayo kwenye mada nyingine nzuri zaidi. Pia usikose kutembea ukurasa wetu wa Mimi na Uhusiano kwenye Mitandao ya Kijamii wa Facebook, Insta:mimi_na_uhusiano au jiunge kwenye group letu la WhatsApp kwa namba iliyopo hapo juu.