The House of Favourite Newspapers

Maneno ya Mwakasege Wakati wa Kuaga Mwili wa Mwanaye

MCHUNGAJI Mwalimu Christopher Mwakasege jana Jumanne Oktoba 16, 2018 aliongoza maombi ya ibada ya kuaga mwili wa mwanaye wa pekee wa kiume, Joshua aliyefariki dunia Oktoba 11, 2018 baada ya kuugua ghafla akiwa kazini, Ibada iliyofanyika  katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Mbezi Beach na kuhudhuriwa na mamia ya watu, akiwemo Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.

Akiongoza maombi hayo, Mwakasege alisema; “Kabla ya kifo, niliwasiliana na Joshua, nilimuahidi kuwa tungezungumza tena jioni baada ya kumaliza semina. Nilipomaliza semina nilimpigia simu lakini iliita bila kupokelewa. Baadaye mlinzi wa kazini kwao alipokea na akatueleza kuwa Joshua amekimbizwa hospitali.

 

“Nilipigiwa simu na daktari, akaniambia kuwa mwanangu amefariki dunia. Ilikuwa ngumu kupokea taarifa ya daktari aliyenieleza kuwa walijitahidi kumuhudumia lakini ilishindikana. Kitu cha kwanza niliwaza namna ya kumshirikisha mke wangu kwa sababu wakati huo alikuwa akimuombea Joshua.

 

“Kwa kuwa taarifa za kifo zilikuja usiku tulikaa hoteli tuliyokuwa tumefikia hadi usiku tulijiuliza tutamueleza nini Mungu katika hali ile. Tuliwaza watu zaidi ya 10,000 waliokuja kuhudhuria semina na tukaona tufikilie zaidi semina.

 

“Haijalishi sehemu tunapita tunataka kukuhakikishia Mungu pamoja na jambo hili gumu utabaki kuwa Mungu kwetu. Tutaendelea kukutumikia na hatutakukasirikia. Siku ya mwisho ya semina ndipo nilitangaza kuhusu kifo cha Joshua, nilikuwa namuita bwana mdogo. Nina ujumbe mwingi sikuweza kusoma. Niwaombe tu radhi wote walionitumia ujumbe nikitulia nitasoma,” alisema Mwakasege.

 

Mwakasege alimaliza kwa kumshukuru Mungu kwa kuwa tangu wakianza huduma hiyo waliahidi kuwa watamtumikia Mungu siku zote za uhai wao. Maziko ya Joshua yatafanyika Jumatano Oktoba 18, 2018 Tukuyu jijini Mbeya.

INASIKITISHA! Abomolewa Nyumba Akiwa Ndani

Comments are closed.