The House of Favourite Newspapers

Maonesho ya Wadau wa Afya ya Kinywa na Meno Kufanyika Nchini

Mwenyekiti wa Bodi ya Tanzania Dental Expo 2025 ambaye pia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Afya ya Kinywa na meno katika Wizara ya Afya, Dk Baraka Nzobo akizungumza kwenye mkutano na wanahabari.
Dar es Salaam, Aprili 2025: Maonesho ya kwanza ya wadau wa huduma za afya ya kinywa na meno Tanzania (Tanzania Dental Expo 2025) yatafanyika Mei 30 na 31 kwenye Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Maonesho haya yanatarajia kushirikisha wadau wa afya ya kinywa na meno zaidi ya 2,000 kutoka Tanzania na nje ya nchi.
MC Big Chriss ambaye naye ni Daktari wa meno akiongoza mkutano huo na wanahabari.
Miongoni mwa washiriki hao ni wataalamu wa afya kinywa na meno, watengenezaji wa vifaa tiba, wasambazaji wa vifaa tiba, hospitali za serikali na binafsi, kampuni za bima ya Afya, taasisi za kifedha na mabenki na wadau wengine mbalimbali ikiwemo idara za serikali kama TBS, TMDA, MSD, TRA n.k. ambapo lengo kuu ni kuchochea maendeleo chanya katika sekta ya Afya ya Kinywa na Meno.
Lengo lingine ya maonesho haya ni kupanua wigo wa Kibiashara na kuleta fursa mbalimbali za uwekezaji na ubunifu katika sekta ya Afya ya kinywa na meno.
Picha ya pamoja baada ya tukio
Aidha maonesho haya yatakuwa jukwaa muhimu la kubadilishana maarifa kwa Wataalam mbalimbali wa afya kinywa na meno, watoa huduma za afya na wadau wengine.
Mwenyekiti wa Bodi ya Tanzania Dental Expo 2025 ambaye pia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Afya ya Kinywa na meno katika Wizara ya Afya, Dk Baraka Nzobo, alisema kuwa maonesho hayo yanaenda sambamba na juhudi za kitaifa za kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza (NCDs).
Dk Nzobo pia alisisitiza umuhimu wa kuboresha afya ya kinywa na meno kwa jamii.
“Nia yetu kubwa ni kuendeleza sekta ya afya ya kinywa na  meno hapa nchini huku tukiboresha ubora na upatikanaji wa huduma hizi.
Aidha katika siku hizo mbili kutakuwa na matukio mbalimbali  ikiwemo warsha, vipindi vya mafunzo kwa wataalamu, mikutano ya kibiashara (B2B), na maonesho ya moja kwa moja ya bidhaa zinazohusiana na teknolojia za kisasa za meno za kidijitali,” alisema Dk Nzobo.
Dk Nzobo alisema kuwa maonesho hayo yatakuwa jukwaa pekee la kujadili na kuboresha utoaji wa huduma, kujadili na kutatua changamoto mbalimbali na pia kuleta maendeleo ya kisasa ya teknolojia.
“Ni maonesho ambayo pia yanahamasisha umuhimu wa afya ya kinywa na meno kuelekea mpango wa afya kwa wote (UHC) kufikia 2030,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Dental Expo2025, Dk Ambege Mwakatobe alisema kuwa afya kinywa na meno ni muhimu kwa afya ya mwili kwa ujumla. Lengo kubwa ni kukuza ubora na ufanisi wa huduma hizi nchini kuendana na teknolojia na uwekezaji endelevu katika vifaa tiba, elimu na huduma za Afya.
Dk Mwakatobe alisema kuwa Tanzania Dental Expo 2025 itatoa jukwaa kwa wadau
Wote katika Kukuza biashara, fursa za uwekezaji, teknolojia mpya na uhamasishaji wa Afya bora ya kinywa na meno.
“Washiriki watapata fursa ya kushirikiana na wazalishaji wa vifaa tiba vya meno wa kimataifa na wa kikanda,vyuo vya Afya, mashirika ya serikali, watoa huduma za bima ya afya, na taasisi za kifedha.
Mchanganyiko huu wa wadau unatarajiwa kutoa fursa kubwa za ushirikiano, maendeleo ya biashara, na uwekezaji katika sekta ya meno inayokua kwa kasi nchini Tanzania,” alisema.
Aliongeza kuwa tukio hili litatoa fursa ya kuimarisha ushirikiano wa kimkakati, kuongeza uwekezaji, na kuhimiza ubunifu wa kiteknolojia.
“Tanzania inakabiliwa na changamoto katika sekta hii kama vile upungufu wa wataalamu waliobobea, miundombinu duni, na uhaba wa vifaa vya kisasa vya matibabu.
Ili kukabiliana na changamoto hizi, serikali imejipanga kupanua huduma za afya ya kinywa kufikia asilimia 20 ya vituo vya afya vya msingi ifikapo mwaka 2030.
Tanzania Dental Expo inachukuliwa kuuwa chachu muhimu katika kufanikisha malengo haya,” alisema.
Alisema kuwa uchumi wa Tanzania unakua kwa haraka na kusababisha ongezeko la watu ambao watahitaji pia ya huduma bora za afya ya kinywa na meno.
“Tanzania kwa sasa ina idadi ya watu zaidi ya milioni 60 ambao wanahitaji huduma bora za afya ya kinywa na meno,” alisisitiza Dk Mwakatobe.
Tanzania Dental Expo 2025 imeungwa mkono na mashirika muhimu ya serikali na sekta ya afya, ikiwa ni pamoja na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), Wizara ya Afya, TAMISEMI, wizara ya mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa Afrika ya Mashariki na Chama cha Wataalamu wa Afya ya Kinywa na Meno Tanzania (TDA), na mashirika mengine, jambo linalothibitisha umuhimu wake katika sekta ya afya na biashara nchini.
FURSA ZA UDHAMINI NA MANUFAA
Waandaaji wa Tanzania Dental Expo 2025 wanakaribisha wadhamini kushiriki kama washirika wa msingi wa tukio hili. Hafla hii inatoa fursa ya kipekee kwa wadhamini kuonesha huduma zao na kushirikiana na wadau muhimu wa sekta ya afya ya kinywa na meno huku wakichangia maendeleo ya tasnia hiyo katika ukanda huu.
Jiunge Nasi Katika Kuinua Ubora wa Huduma za Meno Tanzania!
Tunayo furaha kukualika kushiriki katika Tanzania Dental Expo 2025, ambapo tutachunguza fursa za ukuaji, uvumbuzi, na uboreshaji wa huduma za afya ya kinywa. Tunatarajia kushirikiana nawe katika tukio hili muhimu na tunathamini mchango wako katika kuunda mustakabali wa sekta ya meno nchini Tanzania.