The House of Favourite Newspapers

Mapambano ya Ubingwa wa Global TV Kurushwa Mubashara

1
Chichi Mawe akisaini mkataba wa pambano hilo mbele ya Yassin Abdallah ‘Ustaadh’

 

MABONDIA watatu wa Tanzania wanatarajia kupanda ulingoni katika mapambano ya kimataifa ya kuwania Ubingwa wa Global TV, Afrika Mashariki na Kati chini ya Rais wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBO), Yassin Abdallah Ustaadh ambayo yatarushwa mubashara kupitia Global TV Online.

Mabondia wanaotarajiwa kupanda ulingoni katika mapambano hayo yatakayofanyika Julai 22, mwaka huu kwenye Ukumbi wa Dar Live ni Francis Miyeshusho ‘Chichi Mawe’, Idd Pialali na Nasib Ramadhan ‘Pac Man’.

 

Bondia Idd Pialali akisaini mkataba wa pambano hilo.

 

Mapambano hayo yameandaliwa na kampuni ya kupromoti mchezo wa ngumi za kulipwa nchini, Solid Rock Tanzania Promotions ambayo yatasimamiwa na TPBO.

Ustaadh ameiambia Over Ze Weekend kuwa, lengo kubwa kuja na staili mpya ya kuandaa mapambano ya kimataifa ambayo yatakuwa yakirushwa mubashara na kituo hicho ni kuweza kuinua mchezo wa ngumi ambao umeanza kupoteza mvuto wake kwa wadau wa masumbwi chini.

“Tunaamini hii ni hatua kubwa ambayo italeta mapinduzi katika mchezo wa ngumi za kulipwa hapa nchini hasa kwa upande wa mabondia wetu katika upande wa Kimataifa.

 

Chichi Mawe akiweka pozi.

 

“Unajua hili pambano ni la mkanda wa Ubingwa wa Global TV, Afrika Mashariki na Kati, litakwenda kuonyeshwa live kabisa kupitia kituo hicho siku hiyo hivyo lazima wadau wa masumbwi wajue kwamba ni mapinduzi ya kweli.

“Kiukweli ni mapambano yatakayohusisha mabondia kutoka ndani ya Tanzania, DR Congo, Zambia na Malawi ambao watagombania mkanda wa Global TV, Afrika Mashariki na Kati.

“Hakuna ubabaishaji kwa sababu TPBO, waandaaji wa pambano tumechagua mabondia wazuri kutoka nje ambao wataleta upinzani wa kweli kwa mabondia wetu, angalia Miyeyusho atacheza na Mmalawi, Israel Kamwamba mwenye rekodi kali ya kushinda mapambano nane, matano yakiwa ni KO, hawajawahi kupoteza hivyo mashabiki wategemee vitasa vya kweli.

 

 

“Pialali ambaye siyo mgeni kwa watu wa ngumi, huyu ndiye mrithi wa marehemu Thomas Mashali ‘Simba Asiyefugika’ amejaliwa kila kitu na ufundi mkubwa wa kurusha makonde mazito, rekodi yake ya kushinda mapambano 20, 15 ni KO na amepoteza mawili atacheza dhidi ya Regin Champion raia wa DR Congo.

“Regin siyo bondia wa kawaida maana ameshinda mapambano 15, 13 KO na mawili ni ushindi wa pointi na amepoteza manne, Nasibu ‘Pac Man’ atacheza na Mzimbambwe, Tinashe Mwadziwana.

“Ubora wa Pac Man unajulikana kwa wa wadau wa mchezo huo, kwanza siku zote hakubali kushindwa na rekodi zake zinaonyesha wazi, ameshinda mechi 22, 11 KO na mpinzani wake ameshinda 12, sita KO katika mapambano 22.

“Nadhani sasa wadau wa masumbwi watarajie makubwa zaidi na kujua kuwa mabondia wote ni bora na wana uzoefu katika mechi za kimataifa na kila mmoja anataka ushindi siku hiyo,” anasema Ustaadh.

 

 

Kwa upande wadhamini wakuu wa pambano hilo, Global TV kupitia kwa Meneja Mkuu wa Global Publishers, Abdallah Mirisho ‘Abby Cool’ anasema kuwa, pambano halitakuwa na kiingilio kwa mshabiki wa mchezo huo kwa kuwa litakuwa likirushwa mubashara na kituo hicho.

“Haya mapambano ni ya kimataifa lakini hayatakuwa na utaratibu wa mashabiki wote kuja ukumbini kushuhudia zaidi ya watu maalum ambao wataalikwa kwa kupewa kadi ili kuja kuangalia mabondia watakavyokuwa wakipasuana.

 

“Mashabiki wengine ambao hawatabahatika kupata kadi ya mualiko, wanatakiwa kuingia katika website yetu ya www. globaltvtz.com ili kuweza kushuhudia live kabisa au pia kuingia moja kwa moja katika Mtandao wa Youtube kisha andika Global TV Online na uta- subscribe, baada ya hapo pembeni utakutana na alama ya kengele utabonyeza na moja kwa moja utaweza kupata matukio yote ya Global TV papo hapo.

 

 

“Hii itasaidia kwa mtu aliyepo sehemu ya yoyote duniani kuweza kushuhudia mapambano haya kupitia simu ya mkononi kwa sababu hakuna sehemu yoyote yatakayoweza kuonekana zaidi ya Global TV hivyo ni vyema kuanza ku-subscribe mapema ili kuweza kuona jinsi mabondia wetu wanavyoendelea na maandalizi katika kambi zao na matukio mengi yatakayokuwa yanaruka.

 

“Niwaambie kuwa, siri kubwa ya hawa mabondia wetu wa hapa kila mmoja ametangaza kufanya vizuri hivyo siyo kitu cha kukosa ambacho kitapatikana kupitia kwenye simu,” alisema Abdallah Mrisho ambaye ni meneja wa Global Publishers.

 

Na Ibrahim Mussa | Global Publishers

1 Comment
  1. Global Publishers

    […] Kutoka Spoti Hausi Ya Global… Bondia King Class Mawe Atua Bongo Kutoka Ujerumani… Mapambano ya Ubingwa wa Global TV Kurushwa Mubasha… Pichaz + Video: Dokii Ajitofautisha Na Waigizaji W… .yuzo_related_post img{width:138px […]

Leave A Reply