The House of Favourite Newspapers

Mapazia ya chumbani -10

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
“Na ana bahati tu nilimpa kidogo, je tungekesha?”
Mzuka ulikuwa umempanda. Akili ikamtuma moja kwa moja kuchukua simu yake na kuanza kumchokoza mzee Mashali kwa kuandika meseji.“Nataka tena!” ENDELEA NAYO MWENYEWE…

Mama Kirumba alikaa kwa muda mrefu kitandani akiisubiri meseji ya mzee Mashali lakini hakuambulia kitu.

“Au atakuwa bado anakwaruzana na mama Dick nini?”
Alijiuliza pasipo kupata jibu, akaamua kutuma tena meseji nyingine.
“Jamani, ujue hatukumalizia!”

Napo akasubiri zaidi ya dakika tano bila kupata majibu. Usingizi ukampitia huku simu yake ikiwa pembeni.

* * *Mzee Mashali na mke wake hali haikuwa nzuri. Mke wake bado alikuwa katika hofu ya kuchukuliwa mumewe na mama Kirumba. Tatizo kubwa lililomtawala mama Dick ni kutokuwa na ushahidi wa ana kwa ana.

“Mama Dick.”
“Abee mume wangu!”
“Nimechoka sana, leo nimeanza kuuza maeneo ya kuzunguka kwetu kwani waswahili wanasema kizuri kitembeze kwanza kwako.”
“Ni jambo zuri.”

“Sasa niwekee maji nikaoge, nirudi tena mitaani kuuza mapazia,” aliongea mzee Mashali baada ya kutua rambo lake lilojaa mapazia sebuleni.

“Sawa mume wangu.”
Mama Dick aliingia bafuni haraka kisha akatenga maji na kumuacha mumewe sebuleni akiangalia TV.

“Maji tayari mume wangu,” alisema mama Dick.
Kitendo cha mzee Mashali kwenda tu kuoga na kuacha simu yake ilikuwa kosa kubwa sana. Haikupita dakika mbili meseji ikaingia mbele ya mama Dick. Hakufanya kosa, akatumia mwanya huohuo kuichukua ile simu ya mumewe na kukutana na meseji.

“Nataka Tena.” Mama Dick aliiangalia ile meseji ambayo haikuwa imeandikwa jina zaidi ya kuonekana namba tu. Akajiuliza anayetaka tena ni mapazia au mambo mengine. Akatamani kujibu lakini akasita.

Akiwa katika kuwaza na kuwazua tena meseji nyingine ikaingia, akaifungua.

“Jamani, ujue hatukumalizia!”
Mama Dick akashtuka kusoma hivyo. Akajaribu kuunganisha meseji hizo na kazi ya mumewe ya kuuza mapazia, haikuendana. Akaamua kuichukua ile namba ya simu na kuijaribu kuipiga kwenye simu yake, likatokea jina la mama Kirumba.

“Asante Mungu kwa kunionesha mbaya wangu,” alijisemea moyoni kisha akazihamishia zile meseji zote kutoka kwenye simu ya mume wake kwenda kwake.

Mama Dick akiwa katika kuwaza na kuwazua, mara mzee Mashali akaingia kutoka bafuni. Akili yake haikuwa sawa, aliiwahi simu yake na kuanza kuiangalia kama kuna meseji ama simu imepigwa.

Alihisi huenda mama Kirumba angemtafuta. Akakuta patupu, akatuliza moyo na kumuangalia mkewe kwa tabasamu.
“Baba Dick,” aliita mama Dick.
“Naam mke wangu!”

“Nina wazo nahitaji nikushirikishe.”
“Wazo? Wazo gani tena?”
“Nikubalie kwanza nahitaji nikushirikishe.”
“Haya niambie,” alisema mzee Mashali huku akijifuta vizuri mwili wake.

“Fuko lako la mapazia kubwa na hii inaonesha kabisa mtaji ulioanza nao ni mkubwa sana, kwa hiyo…
“Nakusikia endelea, unatakaje?”

“Kuliko niwe mama wa nyumbani kila siku, na biashara ya mapazia kama unavyoijua ya kwenda nyumba kwa nyumba, mtaa kwa mtaa kutafuta wateja ni ngumu kumaliza nusu ya mzigo kwa siku.”

“Kwa hiyo unatakaje, nirudi gereji kama zamani?”
“Hapana sina maana hiyo mume wangu,”
“Haya niambie unatakaje?”
“Nataka tusaidiane, yaani mimi niwe na fuko langu na wewe uwe na fuko lako tunatembeza maeneo tofauti.”

Maneno yale ya mama Dick yalimfanya mzee Mashali amuangalie kwa muda wa dakika mbili huku akitikisa kichwa. Alijua fika lazima ataingia mkenge wa kulala na wanaume kama alivyofanya kwa mama Kirumba
“Mama Dick.”

“Abee!”
“Hilo haliwezekani!”
“Kivipi mume wangu, si ni sehemu ya kazi tunasaidiana?”
“Nimekwambia haiwezekani!”

“Embu jaribu kulifikiria, litasaidia hata kuendesha familia na kuwa na maendeleo ya haraka.”

Mzee Mashali alifikiria kwa mara nyingine, akavaa nguo zake na kulichukuwa fuko lake la mapazia.

“Nikirudi jioni nitakupa jibu,” alimjibu mkewe huku akili yake ikimtuma breki ya kwanza kwenda kwa mama Kirumba kuchukua hela yake.
Je, nini kiliendelea hapo? Usikose chombezo hili wiki ijayo.

Leave A Reply