The House of Favourite Newspapers

Mapazia ya chumbani-11

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:

“Muda gani?”
“Muda mfupi kabla hujaja na tena nilikutumia mbili.”
“Zilikuwa zinasemaje?”

Mama Kirumba alichukuwa simu yake kisha akamuonesha mzee Mashali meseji alizomtumia. Mzee Mashali alichukua simu yake kuangalia, hakukua na meseji yoyote. Akili ikamruka! ENDELEA NAYO MWENYEWE…

Sasa zitakuwa zimejifuta?” aliongea mzee Mashali kwa kushtuka.
“Zitajifutaje, wewe si unaishi na mkeo mama Dick?”
“Ndiyo”

“Basi atakuwa alizifuta baada ya kusoma!”
Mzee Mashali aliangalia juu kwa muda kisha kichwa chake akakishusha chini.
“Nimegundua kitu.”
“Kitu gani?”

“Kuna muda nilikwenda bafuni kuoga na simu yangu niliiacha chumbani, huenda muda huohuo aliutumia kuzisoma, kwani ulikuwa umendikaje?”
“Niliandika nataka tena!”
“Nyingine?”

“Nyingine niliandika ‘hatukumalizia bado nina hamu!”
“Duhh!”
Mzee Mashali alikuwa hoi kwa mawazo, alishusha fuko lake chini. Nguvu zilimuisha.
“Sasa!”
“Hakuna cha sasa mama Kirumba ulishalikoroga. Kumbe ndiyo maana alikuwa aking’ang’ania na yeye afanye biashara ya kuuza mapazia!”

“Unasemaje mzee Mashali?”
“Nimesumbuana naye sana wakati natoka nyumbani muda huu. Nimeshangaa ghafla tu alibadilika na kutaka eti na yeye aanze biashara za kutembeza mapazia nyumba kwa nyumba kama ninavyofanya mimi.”
“Ukamkubalia?”

“Nani?”
“Si wewe!”
“Weee nimkubalie? Ili akutane na vidume zaidi yangu wafanye yao!”

* * *

Muda wote tangu aondoke mumewe, mama Dick hakuwa na raha hata kidogo. Alihisi kuchanganyikiwa. Hofu ya kuibiwa mumewe nyumba kwa nyumba ilimsononesha sana.
“Lakini, meseji zile kweli mama Kirumba amemtumia mume wangu au zilikuwa zinaenda kwa mume wake?” alijiuliza mara mbilimbili pasipo kupata jibu.
Akili iliyomtuma mama Dick ni kuweka kanga yake vizuri na kwenda moja kwa moja hadi kwa shosti wake, mama Muro.

“Hee mbona juu juu kulikoni!” aliongea mama Muro.
“Wee acha tu!”
“Shemeji huyo?”
“Ndiyo hakuna mwingine?”
“Kalitibuaje tena safari hii?”
“Yaan hii ni zaidi ya kulitibua!”
“Ndiyo uniambie.”

Mama Dick alijisogeza vizuri. Mama Muro akaangalia huku na kule kama kuna mtu anayewaangalia kisha akavuta kigoda na kuketi.
“Haya nipe mchapo!”

“Yaani siongei sana!” alisema mama Dick na kuchukua mkono wake hadi kwenye pochi yake na kuchomoa simu kisha akaanza kutafuta meseji zile alizojitumia kutoka kwenye simu ya mzee Mashali.
“Jionee kwanza hiyo!”
Mama Muro akaisoma akakutana na maneno ‘nataka tena’.
“Sijaelewa!”

“Hujaelewa nini sasa?”
“Nataka tena? Nani sasa huyu katuma!”
“Utaelewa tu, soma na hii ya pili uelewe kabisa.”

Mama Muro akaishika vizuri simu ya mama Dick na kusoma meseji ile ya pili ‘Jamani ujue hatukumaliza’.
“Shemeji yangu huyuhuyu anatumiwa hizi meseji zote!”
“Ndiyo maana yake na ndiyo maana nipo hapa shosti wangu kupata ushauri kwako.”
“Sasa…

“Sasa nini tena?”
“Nani atakuwa amemtumia?”
“Unauliza maembe Kibada? Huyu lazima atakuwa mama Kirumba, akituona anajifanya mtaratibu kumbee!”
“Kama ulikuwa kichwani mwangu hata mimi nilikuwa namuwazia huyohuyo!”
“Cha kufanya hapa hamna kumlazia damu, niruhusu!”
“Nikuruhusu nini?”

“Wee kwanza niruhusu halafu nakwambia ni nini?”
“Haya nimekuruhusu!”
“Ushahidi tunao, cha msingi ni kumvaa tu mama Kirumba au ikiwezekana tumfanyie uhuni ambao hajawahi kufanyiwa maishani!”
“Uhuni gani?”

“Tumkodie hata vijana watano au sita wamfanye, si anajifanya anapenda waume za watu!”
“Hapana! Kwa hilo tutakuwa tumemkosea sana.”
“Lakini si una uhakika ni mama Kirumba!”
“Ndiyo na namba yake ninayo, nilivyoziona tu hizi meseji kwa mzee Mashali cha kwanza kufanya kilikuwa ni kuhakikisha namba iliyotuma ni ya nani ndipo nilipogundua kuwa ni mama Kirumba anayenifanyia mchezo mchafu huu.

“Uhhhf!” Mama Muro akashusha pumzi. Akafikiria kitu.
“Huyu lazima tumfanyie mtego.”
“Mtego wa aina gani?”

“Ila unahitaji uvumilivu wa hali ya juu!”
“Nipo tayari kwa vyovyote!” alisema mama Dick kwa kujiamini.
Wakakubaliana watengeneze kila njia ya kumdhalilisha mama Kirumba.
“Nipo tayari leoleo kumtafuta kijana mwenye umbo kama la shemeji, wewe jipange kwa upande wa meseji, sawa!”

Je, nini kiliendelea hapo? Usikose chombezo hili wiki ijayo.

Leave A Reply