Mapazia Ya Chumbani -7

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:

“Hebu ngoja niende nikajifanye nina shida ya kuazima chochote ili nizione hizo sendozi, kama kweli ni za baba Dick nitazijua tu maana siku hizi ameanza kazi mbaya sana, siipendi,” alisema mama Dick huku akisimama kuondoka kwenda kwa mama Kirumba…   JIACHIE MWENYEWE…

Alipofika mlangoni alipiga hodi kwa sauti ya kuiba, yaani ya chini sana kiasi kwamba, mama Kirumba hakusikia. Akarudia kwa kugonga mlango, lakini pia kwa kuogopa, mama Kirumba hakusikia.

Mama Dick akabaki amesimama akisikiliza ya ndani kwa umakini sana. Aliweza kusikia kwa mbali viashiria kwamba kwa ndani kuna mtu zaidi ya mmoja kwani mama Kirumba mara kwa mara alisikika akicheka. Hapo ni baada ya kumaliza ngwe ya kwanza ya mechi yake na mzee Mashali…

“Itakuwa kweli mbona vicheko kwa wingi?” alijiuliza mama Dick, akabisha tena hodi, safari hii kwa sauti ya juu zaidi.

“Hodi wenyewe hodi humu ndani jamani!”

“Karibu,” sauti iliyokaribisha ilikuwa ni ya mama Kirumba mwenyewe.

Alitoka chumbani bila kujua aliyebisha hodi ni nani na wala mzee Mashali hakuwa makini na sauti hiyo ya mke wake.

“Ngoja nakuja sasa hivi baba Dick. Leo naona nina wageni sana, sijui ndiyo baraka zenyewe au nini!” alisema mama Kirumba akitoka chumbani, akapita sebuleni hadi kuufikia mlango mkubwa, akafungua.

Kukutana macho na mama Dick, mama Kirumba akaanguka chini ghafla…

“Hee! Vipi tena mwenzangu?” aliuliza mama Dick.

Mama Kirumba akasimama chapuchapu huku akijitetea kwamba ameteleza japokuwa eneo lenyewe hakukuwa na kitu cha kumfanya mtu ateleze.

“Pole sana, nina shida na wewe,” alisema mama Dick akiwa amesimama.

Yeye alitegemea mama Kirumba angemwingiza ndani, lakini hali ikawa tofauti. Mama Kirumba alisimama katikati ya mlango akiwa ameushika kila upande na kuuegemea…

“Shida gani mama Dick?” aliuliza mama Kirumba huku akikimbiza macho yake yasikutane na macho ya mke wa mzee Mashali.

Mama Dick alitamani kumwambia ‘sasa si uniruhusu kuingia ndani ili nikusimulie vizuri hiyo shida yangu’ lakini akajikuta akiisema palepale mlangoni na shida yenyewe ilikuwa ya kutunga…

“Mama Muro alikuja kukueleza chochote kuhusu sherehe yake?”

“Ndiyo, tena ametoka sasa hivi!”

“Sasa tutafanyaje kuhusu sare?”

“Sare tutapanga mama Dick, mbona ghafla sana. Nilikuwa nimelala, ngoja nikaendelee kupumzika, nikiamka nitakuja nyumbani kwako, sawa mama Dick?”

“Sawa,” alikubali mama Dick huku macho yakitua chini ya mlango. Alidhani angeziona sendozi za mumewe lakini wapi!

Mama Dick alirudi nyumbani kwake na kumsimulia mama Muro kuhusu mazingira magumu aliyokutana nayo kwa mama Kirumba…

“Mmmh! Kweli! Au atakuwa shemeji kweli?” alihoji mama Muro.

 

***

Mama Kirumba alipoingia chumbani alikaa kitandani huku akijishika kifuani kwa wasiwasi, akamwambia mzee Mashali…

“Unayajua makubwa yaliyonipata?”

“Hapana, umepatwa na nini tena?”

“Nimeanguka mlangoni mwenzako.”

“Kwa sababu gani, uliteleza?”

“Kutokana na mtu aliyebisha hodi.”

“Nani?”

“Mkeo.”

“Si kweli mama Kirumba.”

“Hakyamungu ni mke wako. Lakini sasa naunganisha na ujio wa mama Muro na mkeo, una umoja ndani yake. Wale wametia shaka ya kukuona ukiingia kwangu.”

“Umejuaje?”

“Maana haiwezekani waje kwa dabodabo. Halafu shida yenyewe moja. Mama Muro kaja kunialika sherehe ya binti yake sijui…mkeo naye kaja kuniulizia shughuli hiyohiyo, inawezekana kweli?”

“Mh!” Mzee Mashali aliguna, naye akahisi pana kitu…

“Sasa?” aliuliza mzee huyo…

“Mi sijui, na ukisema utoke kama kweli walikuona ina maana utaonekana zaidi. Na mbaya zaidi ni nyumba yako ilivyo pale, hata mtu akiwa sebuleni anaona mtu anayetoka hapa kwangu,” alisema mama Kirumba.

“Kwa hiyo una maana leo mimi nishinde hapa mpaka giza?”

“Itabidi, sasa utafanyaje? Na kuanzia sasa akija mtu yeyote kuulizia sitoki. Hata akija mjumbe, ni aibu kubwa kwangu kujulikana nimekuchukua wewe. Sijui shetani gani ameniingia leo mimi mama Kirumba…

“Ndiyo mwanzo wa kuishi kwa uadui na majirani zangu! Mh! Sijategemea. Na mama Muro ninavyomjua alivyo mlopolopo, atatangaza kila kona ya mtaa, ‘mama Kirumba si anatembea na baba Dick.’

Maneno hayo ambayo mama Kirumba alikuwa akiyasema kwa sauti ya chini, yalimchoma sana mzee Mashali kwani naye alijenga picha kubwa sana kwenye akili yake.

Mama Kirumba akavuta pumzi kwa nguvu kisha akazitoa na kumwangukia mzee Mashali huku akisema…

“Tumeshaamua kumla nguruwe, basi tumle aliyenona tu.”

Je, nini kiliendelea hapo? Usikose chombezo hili wiki ijayo.


Loading...

Toa comment