The House of Favourite Newspapers

Mapema tu… Ndoa Ya Wolper Shakani Mashabiki Wafunguka “Historia ni Mwalimu”

0
Nyota wa filamu Bongo, Jacqueline Wolper alivyofunga ndoa na Rich Mitindo.

MUDA mfupi baada ya nyota wa filamu Bongo, Jacqueline Wolper kufunga ndoa na Rich Mitindo, mtu mmoja aliandika kwenye mtandao wa kijamii:

“Hatimaye Rich Mitindo amekumbatia bomu lake na tutarajie lolote ndani ya muda mfupi!”

Uchunguzi wa Ijumaa umebaini kuwa, watoa hoja na komenti kwenye mitandao ya kijamii wameitia shakani ndoa hiyo kwa matarajio kwamba, itavunjika muda wowote.

Unaweza kujiuliza kwa nini watu wamejawa na fikra hasi juu ya maisha ya ndoa ya msanii huyo?

Jibu jepesi linaweza kuwa “historia ni mwalimu mzuri.”

Uchunguzi unaonesha kuwa wasanii na mastaa wengi siyo Bongo tu, bali duniani kote ndoa zao huwa hazidumu.

Wolper ambaye alifunga ndoa mwishoni mwa wiki iliyopita aliwahi kubadili dini na kupewa jina la Ilham

ili aolewe na Abdallah Mtoro ‘Dallas’.

Hata hivyo, kazi hiyo ilikuwa ya bure kwani uhusiano wake ulivunjia mapema na yeye kurejea tena kwenye dini yake ya zamani ya Kikristo.

Inaelezwa kuwa, miongoni mwa vitu vigumu kwa mastaa wa kike na wakiume kuvimudu ni ndoa.

Mwigizaji Flora Mvungi, alijaribu kuishi kwenye ndoa na msanii H. Baba akashindwa.

Mkali wa filamu nchini, Rose Ndauka alifurukuta kuishi na msanii wa muziki wa Bongofleva, Malick Bandawe akashindikana.

Historia inakumbusha kuwa msanii wa filamu, Jacqueline Pentzel maarufu kama Jack wa Chuz aliamua kuachana na imani ya Kikristo na kuingia kwenye Uislamu ili afunge ndoa na jamaa anayefahamika kwa jina la Gadna Dibibi lakini ndoa ilibuma mapema.

Mwigizaji mkongwe Michael Sangu naye hakutoka kwenye kapu la walioshindwa kumudu ndoa kwani alibadili na kumuoa mwigizaji mwenzake, Kuruthum Mpalu ‘Ummy’, lakini ndoa yao ilivunjika.

Orodha ambayo  ni ndefu inamwangukia mwigizaji Aunt Ezekiel aliyejitapa enzi hizo kufunga ndoa na Sunday Demonte naye alijikuta mikono mitupu baada ya mumewe kufungwa jela.

Hawa kwa uchache ni kwa upande wa mastaa wa filamu na lakini hata upende wa mastaa wa nyimbo za Injili nako hali ni ileile.

Ukimtaja; Janet Mrema, Bahati Bukuku, Flora Mbasha na wengineo kibao ndoa zimekuwa mtihani mgumu kwao.

Mtaalamu wa masuala ya saikolojia ya mapenzi wa Ujerumani, Robert Stenberg anasema duniani kuna aina nne kuu za mapenzi lakini aina ifaayo kuwa ndoa imara ni PENZI TIMILIFU.

Stenberg anazitaja sifa za Penzi Timilifu kuwa ni mtu kujitolea kwa ajili ya mwenzake, kuujenga ukaribu utakaowafanya wana ndoa kuwa pamoja kimwili na kiroho na kuupa nguvu mzizi wa mapenzi ambao ni  Tendo la Ndoa.

Inaelezwa kuwa; katika mambo hayo matatu mawili ni mepesi kuyamudu lakini kubwa ambalo ndiyo msingi wa ndoa ni mtu kujitolea maisha kwa mwenzake ndilo linalowashinda wengi na kunjikuta ndoa zao zinavunjika mapema.

Kujitolea kunakotajwa hapa ni hali ya mtu kuweka kando namna yoyote ya kujipendelea nafsi yake katika jambo lolote badala yake muhimu ni kwa kila jambo kujitolea kwa ajili ya kumfanya mwenza wake afurahi na kuona yuko huru tena kwenye mikono salama.

Pengine kwa vigezo hivi, mastaa wengi ambao ni watu wa kujirusha, kupenda kurukaruka kama “sungura” katika uhusiano wa kimapenzi, kutoshiba anasa na mambo kama haya ndiko kunakozifanya ndoa zao zisidumu.

Salamu kwa Wolper na mumewe ni kwamba, wengi wanawatabiria mabaya katika ndoa yao; jukumu la kuwaambia wenye mitazamo hasi “dua la kuku halimpati mwewe” wanalo wao, Ijumaa linabaki kusikiliza na kutazama.

Stori Na Richard Manyota

Leave A Reply