MAPINDUZI HASI YA MUZIKI, KUTOKA KIPAJI MPAKA KIKI!

picha ya benpol KIKI

Benpol

Mabadiliko ya muziki yametokea duniani kote! Yanayotokea Tanzania ni kivuli chake tu. Mseleleko huu wa mabadiliko, chanzo chake kikubwa ni biashara –  pesa.

Kiki ni uongo kama uongo mwingine. Hutokea mwanamuziki akashupaza shingo yake bila aibu, akatangaza hadharani, “ndugu zangu nipo Marekani nafanya kazi na msanii mkubwa sana.” Wakati huo, kumbe yupo Mbagala-Rangi Tatu akitafuna mapera ya mzee Athumani!

Wakati muziki wa ‘kizazi kipya’ unaanza mwanzoni mwa miaka ya 2000, ‘kiki’ hakikuwa kigezo cha kukutoa. Kilitegemewa kipaji pekee. Kiki haingekuwa na msaada sana, kwanza studio zenye kueleweka zilikuwa mbili. Hapa wanamuziki wa nyakati hizi walitegemea utoaji wa nyimbo zenye kuvutia ili waendelee kubaki katika chati. JANJA YA NYANI HAIKUWAKO!

Kipaji halisi kiliwaibua wengi kiasi kwamba si rahisi kuwataja wote. Ni kupitia nguvu ya kipaji, aliweza kuonekana mwanadada Saida Karoli kutoka Kagera, akajulikana nchi nzima na hata nje, kwa sababu ya kipaji chake tu.

Mb Dogg na Ratifa wake, Dully sykes na Hi,  Professor Jay na Zali la Mentali, Matonya na Vailet wake, Inspector Haroun na Mtoto wa Geti Kali, Z – Anto na Mpenzi Jini, Juma Nature na Mzee wa Busara, H Baba na Mpenzi Bubu, Mr Nice na Fagilia… wote hawa na wengine kibao, walikuwa na vipaji vya uhakika. Kwa sasa wachache wanapumua, wengi wamepotea kwa kukosa kiki. MAIGIZO!

Miaka ya hivi karibuni, mambo yamebadilika kwa kasi ya kimbunga. Kiki ndiye mkombozi wa wasanii. Wapo wasio na fani kabisa ya uimbaji, lakini tumeshuhudia wakipewa muda wa kusikika kwa sababu ni mafundi wa kutengeneza kiki.

Katika kizazi hiki cha kiki, tumeshuhudia kijana wa kiume akikubali kupakwa mafuta akiwa mtupu ili wimbo wake uweze kupenya! Kwa bahati mbaya, wimbo huo japokuwa ni mzuri, umeshindwa kufanya vyema, labda kwa sababu ya ile laana ya utupu! UJINGA.

Wanamuziki waondoe hofu. Wawekeze muda wao katika kufanya kazi nzuri zenye ubunifu wa kutosha. Kiki zinawakasirisha wafuatiliaji wa kazi zao kwani hakuna mwanadamu anayependa kudanganywa. Ukimdanganya leo, kisha ukajasema ulifanya vile kwa sababu ya kuupa nguvu wimbo wako, mtu huyo hatakusikiliza kesho, atajua ni mwendelezo wa ujuha wako wa siku zote. Kutokana na mfululizo huu wa kiki, wanamuziki wamepoteza tunu muhimu – KUAMINIKA. Hawaaminiki tena! RAI yangu hii isipozingatiwa kwa umakini wa kutosha, ataja vunjwa mtu shingo akose msaada kwa umma kudhani ni mazoezi ya kiki mpya.

 


Loading...

Toa comment