Mapinduzi Yakoleza Mpambano wa Urais 2020

DAR: Wakati Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ikiadhimisha miaka 56 ya mapinduzi visiwani humo, imebainika kuwa, joto la urais katika Uchaguzi Mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika mwisho mwa mwaka huu, limezidi kupanda.

 

Joto hilo limekolezwa na vita ya kuwania mrithi wa rais aliyepo madarakani, Dk Ali Mohamed Shein ambaye anamaliza muhula wake wa mwisho.

Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, kiti hicho cha urais kinapaswa kukaliwa na mtu mmoja kwa muda wa miaka 10 pekee.

 

Kutokana na hali hiyo, duru za kisiasa visiwani humo sasa zimebainisha kuwa baadhi ya vigogo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wameanza kujipitisha na kuandaa mikakati ya chinichini ili kujenga ushawishi kwa Wazanzibar na hatimaye kunyakua kiti hicho, japokuwa wengi wanaotajwa wamekana kujitangaza.

 

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanawatazama zaidi vigogo hao wa CCM, kwa kuwa tayari vyama vya upinzani visiwani humo vimeshanyong’onyezwa hasa ikizingatiwa Chama cha Wananchi (CUF) ambacho kilionekana kuwa tishio kwa CCM, tayari kimesambaratishwa baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad kuhamia Chama cha ACT-Wazalendo.

 

Vigogo hao wanaotajwa ni pamoja na Makamu wa Rais Tanzania, Samia Suluhu, Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa, Waziri wa Ulinzi, Dk Hussein Mwinyi, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni, Balozi Ali Karume, aliyekuwa Waziri wa Fedha wa Zanzibar, Dk Khalid Salum Mohamed, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Abood na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Issa Haji Ussi Gavu.

 

Viongozi wengine wanaotajwa ni waziri kiongozi wa zamani, Shamsi Vuai Nahodha, Mohamed Said Dimo, Mahadhi Juma, Dk Halid Salum Mohamed na Mohamed Hija.

 

WANAOTAJWA WAJITENGA

Licha ya kutajwa mara kwa mara, tayari Makamu wa Rais, Samia amekanusha madai ya kugombea nafasi hiyo.

 

Agosti 26, mwaka jana alisema; “Kuna maneno kwamba Samia anakuja kugombea urais Zanzibar, nataka kuwaambia kuwa si kweli na sina nia hiyo. Ukiangalia ngazi za uongozi ndani ya Tanzania, mimi ni namba mbili, sina kinachonishawishi nije kugombea huku (Zanzibar) niwe namba tatu.

 

“Nimeona niseme huku kwetu (Zanzibar) nilipotoka kwa sababu maneno yamekuwa mengi. Chuki nyingi, ufisadi na majungu ila kwa Samia miye simo,” alisema Samia.

Kwa upande wake, Profesa Mbarawa naye hakubaki nyuma kuruka kihunzi hicho kwa kukanusha madai hayo.

 

“Mimi sina vigezo vya kuwania nafasi hiyo na jukumu langu kwa sasa ni kuhakikisha Watanzania wanapata maji,” alisema.

Naye Masauni alisema bado ana majukumu mazito aliyopewa na wananchi na Rais John Magufuli.

 

“Kwangu hilo ni geni, nafasi nyeti kama hizo huwa haziombwi na wala huwezi kuanza kuzisemea, bali hupangwa na Mungu kupitia wenye mamlaka, mimi waliona nafaa kuwa mbunge wakanipa, lakini mheshimiwa Rais aliona nafaa kumsaidia katika nafasi ya naibu waziri pia akanipa, namshukuru sana,” anasema Masauni.

 

Licha ya vigogo hao kukanusha madai hao, duru mbalimbali zimelieleza IJUMAA WIKIENDA kuwa, baadhi ya viongozi visiwani wameunda makundi maalum yenye kazi moja ya kusuka misingi na mikakati madhubuti ya ushawishi kwa wananchi ili njia iwe rahisi kupita kwenye vikao vya CCM.

 

“Viongozi hao wametumia sherehe hizo za mapinduzi kukusanya yale makundi yao kwenye hoteli mbalimbali zilizojificha hapa Zanzibar kuandaa mikakati yao, kwa sababu kama unavyofahamu viongozi wote wapo hapa hivyo wametumia fursa hiyo kijanja.

 

“Tunawaona… na tunachohitaji ni kiongozi atakayerudisha hali ya demokrasia na kuondoa hii sintofahamu iliyojitokeza kwenye uchaguzi uliomweka madarakani Dk Shein,” kilisema chanzo chetu.

 

PROF MPANGALA

Pamoja na hayo, mmoja wa wachambuzi wa siasa ambaye pia ni Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo kikuu cha Ruaha, Profesa Gaudence Mpangala anasema ni dhahiri joto la urais visiwani humo lazima lipande.

“Kwa sababu Dk Shein anamaliza muda wake, hivyo hawa jamaa lazima wajipange kunyakua kiti.

 

“Ila Rais ajaye lazima atambue kuwa Wazanzibar wana majeraha mioyoni mwao yaliyotokana na Uchaguzi Mkuu 2015, wanahitaji tiba… na tiba pekee ni Katiba Mpya ile iliyopendekezwa na Jaji Warioba. Suala la Serikali tatu lilianza kudaiwa na Rais Aboud Jumbe mwaka 1984, ikaja Tume ya Jaji Nyalali mwaka 1992 na sasa ya Jaji Warioba, hili ni jambo ambalo hawapaswi kulidharau,” anasema Prof Mpangala.

 

DK SHEIN ANGAKA

Kutokana na hali hiyo, Dk Shein mara kwa mara amekuwa akikemea makada hao wanaojipitisha na kuashiria kuanza mapema harakati za kuwani nafasi hiyo.

 

“Nafasi ya urais ndani ya CCM haipatikani kwa kampeni na makundi yasiyo halali, bali kwa utaratibu maalum kupitia vikao vya kikatiba ambavyo vipo kwa mujibu wa Katiba na miongozo na kanuni za CCM,” alinukuliwa Dk Shein.

 

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally aliungana na Dk Shein kukemea hali hiyo na kuwaambia makada hao wakome.

 

“Nafasi ya urais Zanzibar haijatangazwa, bado ina mwenyewe na kutakuwa na utaratibu wa kuijaza, utaratibu huo utasimamiwa na chama si makundi hayo mnayoyapitishapitisha mara kwenye hoteli, mara ofisi za Serikali. Komeni, tabia hiyo acheni,” alionya Dk Bashiru.

Stori: Imelda Mtema, Ijumaa Wikienda

 

 


Loading...

Toa comment