DAR ES SALAAM: Siku chache tu tangu kufariki dunia kwa mke wa pili wa aliyekuwa Mfalme wa Taarab Bongo, Alhaj Mzee Yusuf aitwaye Chiku Khamis, mapya yameibuka huku dada wa mume na mke mkubwa, wakiwachefua wanandugu, Risasi lina habari kamili.
Mwili wa Chiku na kichanga chake ulizikwa Jumapili iliyopita katika Makaburi ya Kisutu ambapo kabla ya kuzikwa uliagwa nyumbani kwa wazazi wake Mtaa wa Livingstone, Kariakoo ambako kuliibuka mambo ya kushangaza.
NYUMBANI KWA WAZAZI WA MAREHEMU
Chanzo makini ambacho kilikuwa msibani hapo kilieleza kuwa, mke wa kwanza wa Mzee Yusuf ambaye pia ni mwimbaji wa Taarab katika Kundi la Jahazi Modern, Leilah Rashid na wifi yake, Khadija Yusuf walizua minong’ono baada ya wifi huyo kukataa kupokea mkono wa pole.
“Unajua pale msibani ndugu wa Chiku na wa Mzee Yusuf, yaani mama yake na dada zake walikuwa karibukaribu hivyo baada ya mwili wa marehemu kupelekwa makaburini, watu wakawa wanatoa mkono wa pole.
“Cha kushangaza Khadija alivyoona wifi yake Leilah anakwenda kumshika mkono, akajifunika na juba lake usoni na hata alipotikiswa na kumpa mkono, aliukataa ikabidi aendelee na watu wengine kuwashika mikono hali ambayo iliwashangaza waombolezaji wengi walioshuhudia tukio hilo,” kilisema chanzo hicho.
VIKAO VYAWEKWA KUWAJADILI
Chanzo hicho kiliendelea kutiririka kuwa kutokana na tukio hilo la Khadija kukataa kupokea mkono wa wifi yake, familia iliweka kikao na kujadili kwani lilionesha picha mbaya kwa watu.
“Familia ya Mzee Yusuf ilikerwa sana na tukio hilo ambapo iliweka kikao na kujadili kwa kina nini kifanyike lakini mpaka sasa muafaka waliofikia bado haujajulikana,” kilisema chanzo.
UTATA CHANZO CHA KIFO WAIBUKA
Bado utata ni mkubwa kuhusu chanzo cha kifo cha Chiku aliyefariki dunia baada ya kufanyiwa upasuaji wa kujifungua ambapo Mzee Yusuf alisema baada ya kumfikisha katika Hospitali ya Amana, aliambiwa asubiri kidogo kwani wataalamu hawakuwepo kwa muda huo.
“Tulifika Amana wakati tunasubiri madaktari, Chiku akaniambia anahisi kama chupa imepasuka lakini kumbe ni damu zilikuwa zinamtoka.
“Wakati wa watu kuondoka wodini ulipofika tukatolewa nje na manesi wakaniambia ndiyo anapelekwa chumba cha upasuaji kutokana na kuanza kuvuja damu hivyo tukaondoka na kwenda kuzungukazunguka.
“Baadaye nikarudi ambapo niliitwa na daktari na kuniambia wamehangaika kuokoa maisha ya mtoto lakini hawakufanikiwa kwa sababu kondo lilikuwa limeshapasuka, pia mama yake alifanyiwa upasuaji na kuamka vizuri na kuzungumza lakini baada ya dakika chache hali ilibadilika naye akafariki dunia.
“Nakumbuka maneno yake ya mwisho wakati ninambeba kumpeleka wodini alikuwa akiniambia pumzi zinakata nikawa namwambia aendelee kusali na kutaja jina la Allah yaani naumia sana ila naomba Mungu anipe subira na naomba watu waniombee subira katika kipindi hiki kigumu,” alisema Mzee Yusuf.
WASINDIKIZAJI WENGINE NAO
Baadhi ya watu waliokwenda pamoja na Chiku hospitalini hapo, walisema wakiwa chumba cha uzazi (Leba) walikaa muda mrefu kabla ya marehemu kuanza kuhudumiwa, kitu ambacho wanaamini kilichangia kifo chake.
“Tulikaa sana kwa kweli, maana mara wakasema hawawezi kumhudumia tumpeleke Muhimbili, mara wakasema tusubiri hadi hali yake ikaanza kuwa mbaya, hatujui mambo ya Mungu, lakini nadhani angewahishwa, angetibiwa mapema,” alisema mtu huyo na kukataa kutajwa jina.
HUYU HAPA DOKTA AMANA
Risasi Mchanganyiko baada ya kufika Hospitali ya Amana na kushindwa kumuona Daktari Mkuu, kwa maelezo kuwa linapaswa kuanzia kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, ambako nako kiongozi huyo hakuwepo ofisini, lilifanikiwa kuzungumza kwa njia ya simu ya ofisini hospitalini hapo na mtu al iyej i tambul isha kama Daktari Mkuu wa Amana.
“Siwezi kukujibu lolote hapa hadi nijue alikuja hapa akitokea hospitali gani, maana hapa ni hospitali ya rufaa, huenda wao ( h o s p i t a l i aliyotibiwa awali) ndiyo w a n a j u a zaidi tatizo lilikuwa ni nini na huenda ndicho kilichosababisha kifo chake, huwezi kusema alicheleweshwa kuhudumiwa bila kupata maelezo hayo,” alisema daktari huyo baada ya kuelezwa kuwa kucheleweshwa kuhudumiwa ndiko kulikosababisha kifo hicho.
MZEE YUSUF APEWA JUKUMU
Kutokana na yaliyojitokeza msibani, ya dada Khadija kukataa kushikwa mkono na mke wa kaka yake huyo, Leilah wadau mbalimbali wamempa jukumu la kushughulikia tatizo hilo ili liishe.
“Huu ni wakati muafaka wa Mzee Yusuf kuwapatanisha mkewe na dada yake maana kifo humaliza tofauti hivyo atumie kipindi hiki kumaliza bifu la wawili hao kwani ni muda mrefu hawapendani wala hawaongei,” alisema mmoja wa wadau.
TUJIKUMBUSHE
Leilah na Khadija ni mahasimu wa muda mrefu ambapo kila mmoja amekuwa mgumu kuweka wazi chanzo cha bifu lao.
GLADNESS MALLYA | RISASI MCHANGANYIKO