The House of Favourite Newspapers

MAPYA YA MTOTO ALIYEKARIRI VIONGOZI WOTE

Itham Mahfudh

KAGERA: Mtoto aliyewahi kutikisa kwenye vyombo vya habari na mitandao mbalimbali nchini Itham Mahfudh (4) kutokana na kipaji chake cha kukariri viongozi mbalimbali duniani alipokuwa na umri wa miaka miwili, baada ya kimya kingi mapya yameibuka.  

 

Risasi Jumamosi lilimfungia safari hadi nyumbani kwao Mafumbo, Manispaa ya Bukoba na kubaini mapya ambapo amekuwa mtoto mwenye ufahamu mkubwa zaidi ya awali kwani anatambua mambo yote yanayofanywa na serikali ya awamu ya tano.

Wakizungumza wazazi wa Itham walisema mtoto wao kwa sasa ana mabadiliko makubwa tofauti na vile alivyokuwa miaka miwili iliyopita kwani sasa ameongeza uelewa wa mambo mengi hasa yanayofanywa na serikali ya awamu ya tano pamoja na mambo ya shule kwani kwa sasa yupo shule ya awali ‘chekechea’.

 

“Kadiri Itham anavyokua amekuwa akiongeza uelewa wa mambo makubwa yaliyofanywa na serikali ya awamu ya tano, chini ya Rais Dk John Pombe Magufuli pamoja na teuzi mbalimbali za viongozi ambapo mambo hayo ni pamoja na ununuzi wa ndege mpya, ujenzi wa reli, ujenzi wa barabara za juu, ujenzi wa ukuta Mererani na  vinginevyo, vitu ambavyo si rahisi kwa watoto wenye umri kama huo kuvifahamu, ingawa wapo hata watu wazima pia hawajui,” alisema baba wa Itham.

 

Kwa upande wa mama mzazi wa Itham, Warda alisema mwanaye huyo kwa sasa amekuwa mtoto anayependa shule na anajua maneno mengi ya Kingereza, hii ni kutokana na yeye kama mama amekuwa karibu naye sana na kumjali kwani si rahisi kumkuta akicheza na watoto hovyo. “Mwanangu amekuwa na uelewa mkubwa siku hadi siku kwa sababu nimekuwa naye karibu sana, huwa simruhusu kucheza na watoto hovyo na kwa hili nawasihi wazazi ambao wanaona mtoto ana kipaji flani kukaa naye karibu zaidi,” alisema mama huyo.

 

Cha ajabu ni kwamba Itham amepata mdogo wake anayeitwa Macknoun ambaye naye ameanza kuvaa viatu vya kaka yake kwani naye ana uelewa sawa na Itham. Itham ni mtoto wa pili kuzaliwa katika familia ya watoto watatu, uwezo wake umetokana na malezi ya wazazi wake, mafundisho na maelekezo lakini zaidi ikiwa ni kufuatilia masuala mbalimbali kwenye runinga ndiyo humfanya kutambua mambo zaidi.

STORI: Abdulatif Yunus, Dar es Salaam

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Comments are closed.