The House of Favourite Newspapers

MAPYA YAIBUKA! SERIKALI YAMRUDISHA TIDO KORTINI

IKIWA ni siku tatu tu tangu aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Tido Mhando,  aachiwe huru baada ya kukutwa hana hatia, upande wa Jamhuri umekata rufaa Mahakama Kuu kupinga hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

 

Mahakama hiyo ilimwachia huru Mhando na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi ambaye alisema sababu za kumwachia huru kuwa ni mikataba minne aliyoingia Tido haikuwa na nguvu ya kisheria kwani haikusainiwa na wahusika akiwamo Mwanasheria Mkuu wa Serikali, lakini Jamhuri wanadai mashtaka yao ni hayohayo kwamba mikataba hiyo iliingiwa bila kufuata utaratibu.

 

Wameongeza kudai kwamba kuingiwa kwa mikataba hiyo isiyofuata utaratibu kulisababisha Kampuni ya Channel Two Group kufungua kesi na Serikali ikalipa mawakili Sh milioni 887.1 ambayo ni hasara iliyosababishwa na mshtakiwa.

 

Tido ambaye alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Januari 26, 2018, alikuwa akikabiliwa na mashtaka matano; mashtaka manne ni ya kutumia madaraka vibaya na moja la kuisababishia serikali hasara ya Shilingi milioni 887.1.

 

Hukumu hiyo ilitolewa Ijumaa iliyopita, Januari 25, 2019 na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi baada ya upande wa mashtaka kushindwa kudhibitisha mashtaka yake.

 

Agosti 27, 2018 Mahakama hiyo ilimkuta Tido na kesi ya kujibu baada ya Hakimu Shaidi kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi watano wa upande wa mashtaka na baada ya kukutwa na kesi ya kujibu, alianza kujitetea ambapo katika utetezi wake, alidai kuwa mchakato mzima wa kuingia ubia wa kuhamisha TBC kutoka katika mfumo wa analojia kwenda digitali ulifanywa na bodi ya TBC.

 

Akihojiwa na wakili wa Takukuru alidai kuwa hakuna kitu alichokifanya bila ridhaa ya bodi na bodi ndiyo iliyomuagiza afanye mchakato wa awali na ulipokamilika aliwasilisha kwao, mwaka 2009. Alidai kwamba hadi anaondoka TBC hakuna mtu yeyote aliyezungumzia suala hilo, si serikali wala bodi.

 

Tido alipoulizwa na wakili wa Takukuru juu ya tofauti za mkataba aliongia na kampuni ya Channel 2 Group na ule wa Startimes alidai aliandikishiana nao mkataba wa makubaliano ya awali kwa sababu walikuwa wakitaka kuhakikishiwa kama wangeitwa na bodi ya TBC na kwamba aliusaini yeye peke yake.

 

Aliongeza kuwa katika mkataba halisi walioingia na kampuni ya Startimes aliusaini yeye na mwanasheria wa TBC. Alibainisha kuwa mkataba wa Startimes ndiyo mkataba halisi ambao waliandikishiana baada ya bodi kuridhia na kwamba kutokana na sheria na taratibu za manunuzi, mkataba halali wa TBC lazima usainiwe na watu wawili ambao ni mkurugenzi na mwanasheria na pia lazima uwe na mhuri wa shirika.

 

Oktoba 30, 2018, Tido kupitia mawakili wake Martin Matunda (marehemu kwa sasa) na Dk Ramadhani Maleta walifunga ushahidi wa upande wa utetezi. Miongoni mwa mashahidi wa upande wa mashtaka waliotoa ushahidi katika kesi hiyo ni pamoja na ofisa uchunguzi wa Takukuru, Victor Lesuya, Mwanasheria wa TBC, Gwakisa Mlawa na Mkurugenzi Mkuu mstaafu wa TBC, Clement Mshana.

 

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Comments are closed.